Zahanati ya Mwamakiliga wilayani
Nyang’hwale ni moja ya sehemu za huduma za kijamii zinazosambaziwa umeme
kupitia mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu mzunguko wa
kwanza (REA III)
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa
Nishati Vijijini (REA), Wakili Julius Kalolo (kulia) akizungumza na
watendaji kutoka kampuni ya Whitecity Guangdong JV na TANESCO wakati
alipofanya ziara ya kukagua kazi ya kusambaza umeme kwenye Kijiji cha
Mwamakiliga wilayani Nyang’hwale.
Wajumbe wa Bodi ya Wakala wa
Nishati Vijijini (REA), watendaji kutoka kampuni ya Whitecity Guangdong
JV na TANESCO na REA wakiangalia jinsi kazi ya kuvuta nyaya
inavyofanyika katika Kijiji cha Mlange wilayani Mbogwe Mkoa wa Geita.
Aliyenyoosha mkono ni Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Wakili Julius Kalolo
Kazi ya kufunga transfoma
ikifanyika katika Kijiji cha Nyasato wilayani Mbogwe Mkoa wa Geita ikiwa
ni utekelezaji wa mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu
mzunguko wa kwanza (REA III)
…………………..
Na Teresia Mhagama, Geita
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa
Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga ameeleza kuwa wakandarasi
wa umeme vijijini wanaosuasua katika utekelezaji wa mradi wa usambazaji
umeme vijijini wa Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza (REA III) hawatapewa
kazi katika miradi inayofuata.
Aliyasema hayo wilayani Mbogwe,
Mkoa wa Geita mara baada ya ya Bodi ya REA ikiongozwa na Mwenyekiti
wake Wakili Julius Kalolo kufanya ziara ya kukagua kazi ya usambazaji
umeme vijijini wilayani Bukombe na Mbogwe.
” Tuko katika ziara hizi si kutoa
maelekezo tu bali pia tunafanya tathmini za wakandarasi kwani tutakuwa
na kanzidata itakayoonesha wakandarasi wanaotekeleza miradi kwa wakati
na viwango vinavyotakiwa na wale wanaosumbua katika utekelezaji wa mradi
unaoendelea.” Alisema Mhandisi Maganga.
Aliongeza kuwa, kanzidata hiyo
itasaidia kuwatambua wakandarasi wote wasiofaa kupewa tena nafasi ya
kutekeleza miradi ya umeme vijijini inayofuata hivyo aliwataka
wakandarasi hao wajipange kufanya kazi vizuri.
Aidha, aliwataka wakandarasi wote
kuzingatia agizo la Serikali la kuhakikisha kuwa ifikapo Disemba 31
mwaka huu, vijiji vyote vilivyo katika mradi wa REA III, mzunguko wa
kwanza vinapelekewa umeme.
Kuhusu mkandarasi anayesambaza
umeme mkoani Geita, kampuni ya Whitecity Guangdong JV, alimuagiza kuwa
ifikapo tarehe 31 Disemba awe amepeleka umeme kwenye vijiji
alivyopangiwa na kuwasilisha mpango kazi utakaoonesha pia kazi
alizopanga kufanya katika kila Wiki.
Bodi ya REA kwa upande wake,
ilimuagiza mkandarasi huyo kutekeleza ratiba za upelekaji umeme katika
maeneo yote ambayo Bodi hiyo imetembelea mkoani Simiyu na Geita na
kumweleza kuwa haitaacha kufuatilia utekelezaji wa ahadi hizo ili
wananchi wapate nishati ya umeme.
Aidha, Bodi hiyo ilimuagiza
mkandarasi kuhamasisha matumizi ya vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) ili
kuwaondolea wananchi gharama kufanya wiring ndani ya nyumba na kwamba kipaumbele kiwe ni wajane, wazee na walemavu.
Pia Bodi hiyo iliwaasa viongozi wa
vijiji katika maeneo mbalimbali nchini ambapo miradi ya umeme vijijini
inaendelea kutekelezwa, kuwahamasisha wananchi ili waunganishiwe na
huduma ya umeme hivyo miradi hiyo kuwa na tija.
Bodi hiyo pia ilikagua kazi ya
usambazaji umeme wilayani Nyang’hwale mkoani Geita ambapo mkandarasi
alieleza kuwa ndani ya Wiki hii atawasha umeme katika Vijiji Saba.
0 comments:
Post a Comment