RAIS
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amewataka
watanzania kutumia fursa zilizopo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kwa
ajili ya kuliletea maendeleo ya taifa.
Aliyasema
hayo jana Jijini Dar es Saalam wakati wa mkutano wake na Wahariri wa
vyombo vya habari nchini katika kuadhimisha mwaka mmoja wa Utawala wake,
ambapo alisema kuwa ipo haja ya kuzungumza na kuelimisha watanzania juu
ya fursa zilizopo katika taasisi hizo.
“Katika
Jumuiya hizo zipo fursa nyingi kwa ajili ya maendeleo ingawa
inahitajika elimu ya kutosha kwa watanzania kuona fursa zilizopo ikiwemo
ufundishaji wa lugha ya Kiswahili nchi za nje” alisema Rais Magufuli.
Mbali
na hayo, akizungumza kuhusu suala la kupambana na Rushwa nchini Rais
Magufuli alitoa wito kwa vyombo vinavyohusika na kupambana na rushwa
kufichua watu wote wanaojihusisha na vitendo hivyo.
Rais
Magufuli alisema kuwa vita ya Rushwa ni ya kila mwananchi, ambapo
alitoa wito kwa watanzania wote kwa ujumla kujiepisha na masuala ya
rushwa kwani rushwa ni kansa ya maendeleo nchini.
“Taifa
litakwama tukiacha suala la rushwa liendelee, tumeumia kweli kweli
katika hili hivyo nitoe wito kwa watanzania wote kwa ujumla kujiepusha
na masuala haya kwa ajili ya maendeleo ya nchi kwani kesi ya rushwa ni
yetu sote” alifafanua Rais Magufuli.
0 comments:
Post a Comment