METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, November 9, 2019

JAFO:RUFAA ZA UCHAGUZI S/MITAA ZAIDI YA 13,500 ZIMEWASILISHWA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo ofisini kwake jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusiana na vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa zilipelekwa rufaa kwenye kamati za maeneo yao.
Sehemu ya waandishi wa habari wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma.
…………….. Na Alex Mathias Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo amesema zaidi ya rufaa 13,500 zimewasilishwa na vyama vya siasa kwenye kamati za rufaa za uchaguzi wa serikali za mitaa.

Aidha, amesema kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi huo jina la mgombea likiteuliwa linabaki kwenye katarasi za kupigia kura hata kama amejiengua kushiriki.

Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dodoma, Jafo amesema vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki kwenye uchaguzi huo zilipelekwa rufaa kwenye kamati za maeneo yao.

“Vyama vyote vimewasilisha rufaa ikiwemo CCM,CUF, NCCR, ACT na rufaa zilizowasilishwa si chini ya 13,500 kamati zinaendelea kufanya maamuzi na tayari zikingine zimeshatoa majibu ya rufaa, kesho tutapata sura halisi ya mchakato mzima wa uchaguzi,”amesema.

Amefafanua kuwa baada ya mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu kukamilika, kulikuwa na nafasi ya kushughulikia mapingamizi mbalimbali ambayo yamewasilishwa kwenye kamati za rufaa za maeneo husika ambapo mwisho wa kupitia rufaa hizo ni leo.

“Kuna ngazi za mapingamizi na jambo hili ni la kidemokrasia huwa linafanyika, ibara ya 23 ya kanuni zetu inasema kamati za rufaa zinamajukumu ya kupitia rufaa zote zinazojitokeza,”amesema.

Aidha amesema katika ziara yake aliyoifanya mikoa mbalimbali kukagua shughuli zinazofanywa na kamati za rufaa kwenye mikoa mbalimbali Singida, Dodoma, Manyara, Iringa na Njombe alipitia baadhi ya fomu zilizokuwa zimepitiwa na kamati hizo na kubaini kuna makosa kwenye ujazaji fomu.

“Kama vile mtu ameandika umri amezaliwa mwaka 2019, sehemu zingine mtu ameandika hata halmashauri yenyewe haiitwi hiyo msaidizi wa uchaguzi afanye nini?, mwingine sehemu ya saini ameweka tarehe halafu sehemu ya tarehe ameweka saini, fomu zingine mtu amejidhamini mwenyewe, wasimamizi walifanya kazi yao kwa mujibu wa kanuni,”amesema.

Ametaja mapungufu mengine ni kutofautiana majina kwenye fomu na daftari la wapiga kura wa uchaguzi.

“Hivi vyote ni vigezo sehemu zingine ni kama mtu mmoja alichukua fomu akawapa watu wengine ‘wadese’ yaani fomu moja iliyokosewa kundi lote limekosea, hii ni kutokana na viongozi hawakufanya kazi yao vizuri ili fomu zijazwe vizuri,”amesema.

Ameongeza kuwa “Nilishasema malalamiko yote yapelekwe kamati za rufaa kwa kuwa zinafanya kazi kwa mujibu wa kanuni na hizi kamati hazifungwi na mtu, nashukuru baadhi ya vyama vimewasilisha na kazi inaendelea ya kupitia rufaa hizo ikiwa leo ni mwisho.”
Jafo amesisitiza uchaguzi wa mwaka huu hauna ujazaji holela wa fomu, na kamati za rufaa zitaendelea kupitia na kutoa maamuzi sahihi.

“Kesho tutatoa taarifa ya rufaa zilizopita na watu walioteuliwa kushiriki uchaguzi huo, tunaendelea vizuri tunatarajia leo jioni zitakamilisha kazi kamati za rufaa na zinafanyia kazi rufaa zote kwa kuwa ziliwasilishwa na wagombea, na watatoa matokeo kwa vyama vyote lakini kamati ya rufaa itakuwa imetimiza wajibu wake,”amesema.

Kuhusu mchakato wa uchukuaji na urejeshaji fomu, Jafo amesema uchaguzi wa mwaka huu kwa mara ya kwanza ukiwa na kanuni bora zaidi ili kila jambo lifanyike kwa utaratibu.
“Wananchi waliochukua walikuwa 555,036 na waliorejesha 539,993 sawa na asilimia 97.29 na asilimia 2.7 hawakurejesha kwasababu mbalimbali,”amesema.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com