*Ashiriki mbio za mwenge kijijini kwao
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewataka Watanzania waendelee kushikamana na wazingatie ujumbe wa mbio
za mwenge za mwaka huu unaohimiza umuhimu wa maji, uchaguzi wa Serikali
za mitaa, vita dhidi ya rushwa, malaria, UKIMWI na dawa za kulevya.
Ametoa wito huo leo asubuhi
(Jumatano, Oktoba 9, 2019) wakati akizungumza na viongozi wa Halmashauri
za Lindi na Ruangwa na wananchi wa kijiji cha Nangumbu kwenye uwanja wa
shule ya msingi Nangumbu ambako mwenge huo ulipokelewa saa 1:44 asubuhi
ukitokea Nyangao wilayani Lindi.
Waziri Mkuu ambaye ni mbunge
wa jimbo la Ruangwa, aliwasili wilayani Ruangwa jana jioni, ili
kushiriki mbio za mwenge. Kesho (Alhamisi, Oktoba 10) mwenge huo
utaelekea Nachingwea, ambapo Ijumaa (Oktoba 11) utaenda Liwale, Jumamosi
(Oktoba 12) utaenda Kilwa na Jumapili (Oktoba 13) utakuwa Manispaa ya
Lindi ambako utahitimisha mbio hizo na kuzimwa Oktoba 14, mwaka huu.
Waziri Mkuu amewataka wananchi
wote wajiandikishe kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili Tanzania
iweze kupata viongozi bora. “Tuitikie kaulimbiu ya mwaka huu kwa
kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Hapa Ruangwa, hadi jana jioni watu 28,000 walikuwa tayari
wamejiandikisha. Tukachague viongozi wachapakazi na waadilifu
watakaoleta maendeleo kwa nchi yetu,” amesisitiza.
Mapema, akizungumza baada ya
kupokea mwenge huo saa 2:21 asubuhi, Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Bw.
Hashim Mgandilwa alisema utakimbizwa kwenye kata saba na vijiji 17
ambapo miradi mitatu mikubwa yenye thamani ya sh. bilioni 2.9
itazinduliwa.
Katika kijiji cha Nangumbu,
mwenge ulizindua mradi wa mabweni na klabu ya kupiga vita rushwa kwenye
shule ye sekondari ya Hawa Mchopa. Ukiwa njiani, mwenge huo ulipitishwa
kijiji cha Nandagala ambako Waziri Mkuu alizaliwa. Pia aliupokea na
kuukimbiza kidogo akiwa na wanakijiji wenzake, kisha mwenge huo
ukaendelea kukimbizwa kuelekea kata ya Likunja ambako watazindua mradi
wa maji wa Kitandi. Pia mwenge huo utazindua mradi wa barabara ya lami
kwenye kata ya Nachingwea, iliyoko Ruangwa mjini.
Akizungumza kabla ya kuanza
kwa mbio za mwenge wilayani Ruangwa, kiongozi wa mbio za mwenge Kitaifa,
Bw. Mzee Ali Mkongea alimshukuru Waziri Mkuu kwa kujumuika na wananchi
kushiriki ratiba ya mapokezi ya mwenge wilayani humo.
Alisema Serikali ya awamu ya
tano, ndani ya miaka mitatu (2015-2018) imekamilisha kwa wakati miradi
124 ya maji ambapo aliitaja baadhi yake kuwa ni miradi mikubwa ya
Chalinze, Bagamoyo, Arusha, Tabora na Musoma. Pia alisema Serikali
imeendelea na uchimbaji wa visima virefu na vifupi vya maji kwa gharama
ya sh. bilioni 14.
“Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzana kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
zimeingia mkataba na Serikali ya India wa dola za Marekani milioni 500
kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji kwenye miji 28 ya Tanzania. Lakini
kuna changamoto nyingi kwenye miradi hii ikiwemo matumizi mabaya ya
fedha za umma na wakandarasi kujenga baadhi ya miradi chini ya kiwango.”
“Pia kumekuwa na shughuli za
kibinadamu karibu na vyanzo vya maji. Wananchi tusaidiane kuvilinda
vyanzo hivi kwa sababu kazi ya kuvitunza si ya Serikali peke yake bali
inaanza na mimi na wewe,” alisema.
Aliwasihi wananchi hao
wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa
ili waweze kuchagua viongozi wazalendo ambao wana calibre ya Rais, Dkt. John Pombe Magufuli.
Akitoa takwimu za ugonjwa wa
malaria nchini, Bw. Mkongea alisema mkoa wa Kigoma unaongoza kwa
maambukizi ya ugonjwa huo kwa asilimia 24, ukifuatiwa na Geita (asilimia
17), Mtwara (asilimia 15) na Lindi wenye asilimia 12.
“Niwasihi wananchi tumieni
vyandarua vinavyotolewa bure na Serikali hasa akinamama wajawazito na
watoto walio na umri chini ya miaka mitano. Kuna maeneo tumekuta baadhi
ya watu wakivitumia kuvulia samaki na kufungia bustani ili kuku
wasiingie. Haya si matumizi yake hata kidogo,” alisisitiza.
0 comments:
Post a Comment