*******************************
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amekagua shamba la mfano la korosho lenye ukubwa ekari
12,000 lililopo kijiji cha Misigati, wilayani Manyoni na kusema kuwa
ameridhishwa na uamuzi wa wilaya hiyo kuwa na zao mbadala la biashara.
Akizungumza
na wananchi na baadhi ya watumishi wa Halmashauri hiyo waliokuwepo eneo
hilo jana (Ijumaa, Oktoba 4, 2019), Waziri Mkuu alimpongeza Mkuu wa Mkoa
wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi kwa kulibeba wazo hilo na kuhakikisha
linatimia.
“Nimpongeze
Mkuu wa Mkoa wa kulibeba jambo hili, lakini nikuombe wewe na viongozi
wenzako mhamasishe wengine walime zaidi zao hili kwa sababu korosho ni
zao kubwa duniani na tena zao hili lina bei nzuri kimataifa,” alisema.
Alisema
anatambua kwamba timu ya wataalamu kutoka kituo cha utafiti wa kilimo
cha Naliendele, Mtwara imeshawasili Manyoni ili kufanya utafiti za zao
hilo na jinsi linavyoweza kuzaa mara mbili kwa mwaka.
“Kwa kawaida,
mkorosho mmoja hutoa kilo 40 za korosho kwa msimu mmoja, kwa hiyo kwa
misimu miwili mtapata kilo 80. Ninawasii limeni korosho kwa ajili ya
watoto wenu ambao wako darasa la pili au la tatu. Mkulima ukianza
kuvuna, utaendelea kuvuna kwa miaka 20 mfululizo na kwa hiyo hao watoto
hawatahitaji kulipiwa ada wakiwa chuo kikuu sababu korosho itakuwa
inawalipia,” alisema.
Katika hatua
nyingine, Waziri Mkuu amewataka wakulima wanaolima zao hilo wilayani
Manyoni, waunde Ushirika wao ambao utawasaidia kuagiza dawa kwa pamoja
ama kuuza kwa pamoja.
Hivyo, amemwagiza Afisa Ushirika wa Wilaya hiyo, Bi. Yusta Philipo ahakikishe anasimamia jambo hilo kuanzia sasa.
Mapema, akitoa
taarifa juu ya mradi huo, Meneja wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT)
Kanda ya Kati, Bw. Ray Mtangi alimweleza Waziri Mkuu kwamba mradi wa
kilimo cha korosho unajumuisha mashamba makubwa mawili ambapo shamba la
Misigati lina ukubwa wa ekari 7,000 na lile la Mikwese lenye ukubwa wa
ekari 5,000.
Alisema watu
mbalimbali wakiwemo viongozi wa kitaifa wamekuwa wakifika shambani hapo
ili wajifunze mbinu mpya za kuzalisha korosho kwenye maeneo yao. “Wiki
mbili zilizopita, Mheshimiwa Spika na madiwani wa Kongwa walipita hapa
ili kujifunza zao hili,” alisema.
Pia alisema
Halmashuri yao imetenga eneo la ujenzi wa viwanda na kwamba hadi sasa
wanazo ekari 50 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kubangua korosho.
Mapema,
Waziri Mkuu alikagua shamba hilo na kujionea hali halisi ya shambani
ikoje. Pia alioneshwa mabibo na korosho ambazo zimevunwa kutoka kwenye
shamba hilo la mfano, kutoka kwenye mashamba ya wakulima ambao walipanda
miche tangu Januari, mwaka jana.
0 comments:
Post a Comment