Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akikagua skimu ya umwagiliaji ya Kiwalala katika Halmashauri ya Mtama
Mkoani Lindi, Oktoba 17, 2019. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya
Lindi, Shaibu Ndemanga na wa tatu kushoto ni Mbunge wa Mtama, Nape
Nnauye.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………………..
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
amewaagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtama na Mkurugenzi wa
Umwagiliaji wa Kanda ya Kusini, wafike ofisini kwake Dar es Salaam kesho
asubuhi na taarifa kuhusu skimu wa umwagiliaji wa Narunyu.
Ametoa agizo hilo leo mchana
(Alhamisi, Oktoba 17, 2019) wakati alipoenda kukagua skimu hiyo ambayo
imekuwa ikilalamikiwa tangu 2017. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtama ni
Bw. Warioba Gunze na Mkurugenzi wa Umwagiliaji wa Kanda ya Kusini, ni
Mhandisi Mndeme.
Amechukua uamuzi huo baada ya
kufika eneo la mradi na kupokea malalamiko ya wanajumuiya ya umwagiliaji
kutoka kwa Mwenyekiti wao, Bw. Bakari Awadhi juu ya kusuasua kwa mradi
huo lakini alipotaka apate maelezo ya wataalamu hakuna hata mmoja ambaye
alikuwepo.
“Nilitaraji niwakute hapa
Mkurugenzi wa Halmashauri, Afisa Umwagiliaji wa Wilaya na Mkurugenzi wa
Umwagiliaji wa Kanda. Nimeagiza wanikute uwanja wa ndege Lindi au Dar es
Salaam na kesho asubuhi waje ofisini kwangu wanipe taarifa kamili ya
mradi huu. Nataka nijue fedha zilizobakia zaidi ya sh. milioni 240 ziko
wapi.”
“Walipaswa niwakute hapa
wananisubiri kwa sababu nilitoa taarifa tangu jana kwamba nitapita hapa.
Nimepata taarifa kwamba wamesafiri kutoka Mtwara na leo asubuhi
walikuwepo Lindi mjini. Waje ofisini kesho, wakishindwa, nitachukua
maamuzi mengine,” amesema.
Akielezea umuhimu wa mradi huo
wakati akizungumza na baadhi ya wanaushirika waliokuwepo, Waziri Mkuu
amesema ni wa muhimu kwa sababu unatiririsha maji wakati wote. “Huu ni
mradi wa kuringia. Mradi huu unatiririsha maji wakati huu wa kiangazi,
tena mengi tu.”
Amesema kutokana na umuhimu wa
mradi huo, hivi sasa wangekuwa wanazalisha mazao ya kila aina. “Hapa ni
mahali pa kuzalisha mazao mengi, leo unalima mahindi, ukivuna unapanda
matikiti, ukitoa unapanda nyanya. Sasa nitapasimamia mwenyewe,”
amesisitiza.
Amewataka wanaushirika
wanaounda jumuiya ya umwagiliaji wahakikishe kila mmoja anatambua eneo
lake na mara kazi ikianza wawe tayari kuanza kilimo. “Huu mradi una
manufaa kwa watu wa Ruo, Mahumbika hadi Mnazi Mmoja. Lazima
tuung’ang’anie kwa sababu kuna idadi kubwa ya wakulima wanaoutegemea.
Huu mradi lazima tuuvalie njuga.”
Waziri Mkuu alipofika uwanja
wa ndege wa Lindi, maafisa hao walikuwa hawajafika kwa sababu simu zao
hazikupatikana, na akaagiza waje Dar es Salaam kesho asubuhi.
Mapema, Mkuu wa Wilaya ya
Lindi, Bw. Shaibu Ndemanga alimweleza Waziri Mkuu kwamba katika mafaili
aliyoyapitia ofisini kwake alibaini kwamba mradi huo ulitengewa sh.
milioni 788 ambapo mkandarasi wa kwanza Chest Investments Company
alilipwa sh. milioni 121 lakini akashindwa kazi.
“Mkandarasi wa pili ambaye ni D
& L naye alilipwa zaidi ya shilingi milioni 400 naye pia akashindwa
kazi ya kuondoka tope. Kwenye ripoti, inaonesha zilibakia sh. milioni
249,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa wanajumuiya
ya umwagiliaji ya Narunyu, Bw. Bakari Awadhi alisema skimu hiyo yenye
ukubwa hekta 1,200 imekuwa ikijaa maji na kufunika mitaro na hatimaye
kujaa mchanga.
Alimwomba Waziri Mkuu awasaidie kuifufua skimu hiyo kwa sababu inawanufaisha wakazi wa mikoa ya Lindi na Mtwara.
0 comments:
Post a Comment