Na Ismail Ngayonga,MAELEZO
DAR ES SALAAM
KILIMO ni uti wa mgongo wa
uchumi wa Tanzania, hii ni kutokana na ukweli kuwa sekta hii huzalisha
nusu ya uchumi wa nchi, robo tatu ya mazao yote yanayouzwa nje ya nchi
na ni tegemezi la chakula na kutoa ajira ya karibu asilimia 80 ya
Watanzania.
Hata hivyo kwa kipindi cha miongo
miwili iliyopita, jumla ya uzalishaji wa bidhaa na huduma kitaifa kwa
sekta ya kilimo ya kilimo imekuwa ikiongeza kwa wastani wa asilimia 3.5
tu kwa mwaka.
Inaelezwa kuwa ukuaji huu umekuwa
ukiathiriwa zaidi na teknolojia duni ya kilimo, hali ya hewa
isiyotarabiriwa na kushuka kwa kiwango uzalishaji upande wa ardhi,
kutokana na asilimia 70 ya maeneo ya kilimo nchini kutegemea kilimo cha
jembe la mkono.
Kuna baadhi ya vikwazo vinavyozuia
kuenea kwa kwa matumizi ya teknolojia ya kisasa za kilimo na hivyo
kukwamisha uwezo uliopo wa kuongeza uzalishaji katika kilimo, ikiwemo
gharama kubwa za kupata huduma za zana za kisasa za kilimo kwa kukodi na
ukosefu wa utaalamu na huduma za kufanyia matengenezo zana husika.
Aidha wakulima wadogo wadogo kwa
ujumla hawana uelewa, umoja na ari ya kujipanga ili kushughulikia
mahitaji yao na changamoto mbalimbali ili waongeze uzalishaji katika
Kilimo.
Katika jitihada zake za kukuza
matumizi ya zana bora za Kilimo, Serikali imekuwa mstari wa mbele katika
kuwahamasisha wakulima katika kubuni mbinu mpya za matumizi ya utafiti,
elimu na teknolojia mpya ili kuwa na shughuli za biashara zinazohusiana
na kilimo zenye faida ya kuridhisha.
Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio
ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2019/2020, Waziri wa kilimo,
Japhet Hasunga anasema takwimu zinaonesha kwamba matumizi ya zana bora
za kilimo yanaongezeka miongoni mwa wakulima nchini ambapo kwa mwaka
2018 wastani wa kitaifa umeongezeka hadi kufikia asilimia 20 kwa
matrekta na asilimia 27 kwa wanyama kazi.
Naongeza kuwa kutokana na ongezeko
hilo, matumizi ya jembe la mkono yamepungua na kufikia asilimia 53 kwa
mwaka 2018 ikilinganishwa na asilimia 62 kwa mwaka 2013, juhudi
zilizotokana na Serikali kuhamasisha sekta binafsi kuingiza matrekta na
zana zake nchini.
“Kati ya mwaka 2016/2017 na
2017/2018, jumla ya matrekta makubwa 2,476 na matrekta madogo 586
yaliingizwa nchini, na Wizara kwa kwa kushirikiana na Shirika la
Maendeleo la Taifa (NDC), TIB Corporate Bank na Benki ya Maendeleo ya
Kilimo Tanzania (TADB) imetoa mafunzo kwa waendesha mitambo 76 kuhusu
uendeshaji na matengenezo ya matrekta aina ya URSUS” anasema Waziri
Hasunga.
Waziri Hasunga anasema viongozi
108 wa Vyama vya Msingi na 53 wa Vyama vya Mazao (AMCOS) wamepatiwa
mafunzo ya usimamizi na uendeshaji wa matrekta na kati ya AMCOS hizo, 50
ni za Mkoa wa Mwanza na 3 za Wilaya ya Bunda Mkoa wa Mara.
Anaongeza kuwa Wizara ya Kilimo
kwa kushirikiana Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) imetoa mafunzo ya
uendeshaji wa mitambo ya kuvunia na mashine za kukoboa mpunga kwa
maopareta 28 na mafunzo ya usimamizi na uendeshaji mradi wa zana kwa
wakulima viongozi katika skimu 14 za umwagiliaji.
Anazitaja Skimu hizo kuwa ni
pamoja na Skimu za Mbuyuni, Uturo, na Ipatagwa (Mbarali), Nakahuga
(Songea), Magozi (Iringa), Mkindo (Mvomero), Kilangali (Kilosa),
Bagamoyo BIDP (Bagamoyo), Mombo (Korogwe), Kivulini (Mwanga), Musa
Mwinjanga (Hai), Lekitatu (Arumeru), na Muungano (Babati).
Aidha Waziri Hasunga anasema
Serikali kupitia Mfuko wa Taifa wa Pembejeo za Kilimo (AGITF) Wizara
yake inaendelea kutoa mikopo ya pembejeo na zana za kilimo ambapo tangu
kuanzishwa kwake mwaka 1994 jumla ya mikopo yenye thamani ya Tsh Bilioni
82 imetolewa.
Akifafanua zaidi Waziri Hasunga
anasema katika kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019, mikopo 33 yenye
thamani ya Shilingi 1,495,362,060 ikiwemo 22 ya mitambo ya mashambani,
sita (6) ya pembejeo za kilimo na mitano (5) ya umwagiliaji imetolewa na
vilevile Serikali imeendelea na ufuatiliaji wa marejesho ya mikopo ya
nyuma ambapo katika mwaka 2018/19 jumla ya Tsh Bilioni 1.8 zimerejeshwa.
Matumizi ya zana bora za kilimo
unasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufanisi na faida pamoja na
kupunguza gharama za muda na rasilimali fedha ambazo kwa kiasi kikubwa
zimewasaidia wakulima wengi kuongeza ukubwa wa mashamba yao angalau kwa
robo hekta hadi kufikia hekta 1 hadi 4.
0 comments:
Post a Comment