Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akizindua mashine ya kukoboa Mpunga katika kijiji cha Mkindo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ambayo ni moja ya mashine kubwa nne zilizonunuliwa na kusimikwa kupitia mradi huo, Jana Tarehe 2 Disemba 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua mashine kukoboa mpunga katika kijiji cha Mkindo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, Jana Tarehe 2 Disemba 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akizindua mashine ya kukoboa Mpunga katika kijiji cha Mkindo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ambayo ni moja ya mashine kubwa nne zilizonunuliwa na kusimikwa kupitia mradi huo, Jana Tarehe 2 Disemba 2019.
Na
Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Morogoro
Serikali imelipongeza Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa-FAO,
Serikali ya Venezuela, Halmashauri za Wilaya za Kilosa, Mvomero na Kilombero
kwa utekelezaji wa mradi wa ubia wa maendeleo ya mifumo ya uzalishaji
endelevu wa mpunga Afrika chini ya jangwa la Sahara.
Pamoja na majukumu mengine mradi huo ulikuwa
na majukumu ya kuwafundisha vijana kilimo shadidi cha mpunga ambacho kinatumia
mbegu kidogo zenye ubora na maji kidogo huku kikiwahakikishia wakulima mavuno
zaidi.
Mradi huo pia ulitoa na kuwafundisha vijana
kutumia zana za kilimo zenye kujali masuala ya jinsia, kurahisisha kazi na
kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno.
Waziri wa
Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ametoa pongezi kwa taasisi hizo jana tarehe 2
Disemba 2019 wakati akizindua mashine ya kukoboa Mpunga katika
kijiji cha Mkindo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ambayo ni moja ya
mashine kubwa nne zilizonunuliwa na kusimikwa kupitia mradi huo.
Amesema kuwa lengo la serikali kwa
kushirikiana na taasisi hizo ni kuhakikisha kuwa wakulima katika eneo hilo wanatunza
ubora wa mazao yao na kupunguza upotevu wa mazao yao baada ya mavuno ikiwa pia
ni kuyaongezea thamani ili kupata faida zaidi.
Amesema
kuwa Sanjali na jitihada hizo, Wizara ya Kilimo imeanzisha kitengo cha masoko
ya mazao ya kilimo ambacho kinahusika na kutafuta masoko ndani na nje ya nchi
kwa mazao mbali mbali yanayozalishwa hapa nchini ili mbegu zitakazozalishwa na
kuwa na mafanikio makubwa katika kilimo uweze kuimarisha kipato cha wananchi.
Takwimu
zinaonesha kwamba wastani wa kitaifa wa matumizi ya zana bora za kilimo
umeongezeka hadi kufikia asilimia 20 kwa matrekta na asilimia 27 kwa wanyama
kazi ikilinganishwa na asilimia 14 ya matrekta na asilimia 24 ya wanyama
kazi mwaka 2013.
Amesema
kuwa Kutokana na ongezeko hilo, matumizi ya jembe la mkono yamepungua na kufikia
asilimia 53 kwa mwaka 2018 ikilinganishwa na asilimia 62 kwa mwaka 2013.
Aidha, kupitia Mfuko wa Taifa wa Pembejeo za Kilimo (AGITF) Wizara imeendelea
kutoa mikopo ya pembejeo na zana za kilimo.
Waziri
Hasunga amesema kuwa mradi huo umekuwa ukitekeleza kwa vitendo Mkakati wa
Kitaifa wa Kuwahusisha Vijana katika Kilimo wa mwaka 2016 pamoja na Awamu ya
Pili ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP-II), Sera na Miongozo
mbalimbali ya kilimo hapa nchini.
Alisema
kuwa kupitia miongozo hiyo mbalimbali, Wizara ya Kilimo imeendelea kuratibu
utekelezaji wa mikakati ya maendeleo ya kilimo hapa nchini kwa kuimarisha
huduma za utafiti, upatikanaji na utumiaji wa pembejeo na zana za kilimo,
udhibiti wa visumbufu vya mazao, huduma za ugani, uongezaji wa thamani na
upatikanaji wa masoko.
“Nafarijika
kutambua kuwa vijana walionufaika na mradi huu pia walipata mafunzo ya kuongeza
thamani kwa mavuno yao, ufikiaji na upatikanaji wa masoko ili kuweza kuuza
mazao yao kwa faida” Alikaririwa Mhe Hasunga
Alisisitiza
kuwa zao la mpunga ni la pili kwa umuhimu hapa nchini linapokuja suala la
chakula likifuatia kwa mahindi ambayo ndio zao kuu la chakula kwa Watanzania
wengi. “Kama ilivyo kwa mazao mengine, Serikali imeweka mikakati kadhaa ya
kuhakikisha uzalishaji wake unaongezeka. Kwa sasa nchi yetu inazalisha karibu
asilimia mia moja ya mahitaji yetu ya mchele kwa mwaka tukiwa ni nchi ya pili
kwa uzalishaji wa mpunga Afrika baada ya Madagascar” Alisema
Alisema
kuwa kukosekana kwa miundombinu dhabiti ya umwagiliaji, zana na teknolojia duni,
athari mabadiliko ya tabia nchi pamoja na mbegu zenye ubora hafifu ni miongoni
mwa sababu zinazotuzuia tusizalishe zaidi na
kwa tija, hivyo serikali imeweka msisitizo madhubuti katika kukabiliana
nazo.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment