
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akitazama Pamba wakati alipotembelea maghala ya Kiwanda cha Kuchambua
Pamba cha Chama Kikuu cha Ushirika cha Chato mkoani Geita, Septemba 21,
2019. Kushoto ni Meneja wa Chama hicho, Charles Nyasi. (Picha na Ofisi
ya Waziri Mkuu).
********************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewataka wakulima wa zao la pamba nchini wasikubali kuuza pamba yao
chini ya bei elekezi ya sh. 1,200.
Hata hivyo, Waziri Mkuu
amewashauri wafanyabiashara wa zao hilo waungane na kuanzisha viwanda
vya kutengeneza nyuzi na nguo ili kuongeza thamani kabla ya kuuza pamoja
na kuwahakikishia wakulima soko.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo
(Jumamosi, Septemba 21, 2019) wakati akizungumza na viongozi na
wananchama wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Chato (CCU) pamoja na
wananchi kwenye kiwanda cha kuchambua pamba cha Chato kinachomilikiwa na
CCU mkoani Geita.
Amesema wakulima waendelee
kuwa na subira kwa sababu wanunuzi hao wamepewa fedha za kutosha kununua
pamba yote kwa bei ya 1,200 na si vinginevyo.
“Hata mkiwa na shida msikubali
kuuza pamba yenu chini ya sh. 1,200 kwa kuwa haitachukua muda mrefu
mtakuwa mmeshapata fedha zenu. Tuna taarifa kuwa kuna wanunuzi wamepata
fedha na wanawatumia watu kwenda kuwalaghai wakulima kwa kutaka kununua
kwa bei ya sh. 800, msikubali na mkiwaona mtupe taarifa.”
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema
viwanda vya nyuzi na vya nguo vikijengwa nchini vitakuwa na uhakika wa
soko kwani hivi sasa Tanzania haina viwanda vya kutosha vya
nguo. Amesema Serikali ipo tayari kuwaunga mkono Watanzania wote au
mwekezaji yeyote atakayekuwa tayari kuanzisha viwanda vya aina hiyo kwa
sababu mahitaji ni makubwa.
“Tuna shule zaidi ya 18,000
Tanzania na wanafunzi wote wanavaa sare zinatokanazo na pamba, tukisema
majora ya sare yasukwe humu humu ndani na kisha kusambazwa mikoa yote
bado nguo za watu wanaovaa mitaani. Watapata faida tu.”
Pia, Waziri Mkuu amewaagiza
viongozi wote wa vyama vya ushirika katika maeneo yanayolima pamba
kuwaelimisha wakulima kuhusu umuhimu wa kuzalisha pamba safi ili walinde
heshima ya pamba ya Tanzania ambayo duniani inasifika kuwa ni dhahabu
nyeupe.
Awali, Meneja wa CCU, Charles
Nyasi alimwambia Waziri Mkuu kuwa makampuni ya METEL, KCCL na FRESHO
yamejitokeza kununua pamba kupitia AMCOS na tayari kilo 9,611,860
zimenunuliwa kati ya kilo 11, 140,529 zilizokusanywa.
Alisema kampuni ya FRESHO imenunua kilo 4, 869, 960, KCCL imenunua kilo 3, 025,051 na METEL imenunua kilo 1,716, 420.
Pia Meneja huyo aliiomba
Serikali isaidie kuwalipia deni la sh. 696,854,475.20 ili kumaliza
tatizo la madai ya watumishi na wadai wengine. Pia aliiomba Serikali
isaidie kuilipia CCU deni la sh. 102, 942,300.00 la ardhi waliyotumia
kujengwa kiwanda chao.
Akijibu maombi hayo Waziri
Mkuu alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John
Magufuli haiwezi kulipa deni hilo hadi itakapopewa maelezo ya kina ni
nani aliyesabaisha deni, mazingira yaliyosababisha deni hilo.
0 comments:
Post a Comment