METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, September 9, 2019

MAKALA: WAZIRI JAPHET HASUNGA AMALIZA ZIARA YA KIKAZI YA SIKU SITA NCHINI ISRAEL, ASEMA UTAFITI WA KILIMO NA TEKNOLOJIA ZA ISRAEL UTAINUFAISHA TANZANIA

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiagana na mwenyeji wake Balozi wa Tanzania nchini Israel Balozi Job Daud Masima katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Ben Gurion Jijini Tel Aviv, nchini Israel baada ya kumaliza ziara ya kikazi ya siku sita. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) jana alfajiri tarehe 8 Septemba 2019 amerejea nchini baada ya kumaliza ziara ya kikazi ya siku sita nchini Israel iliyoanza tarehe 1 Septemba 2019 na kumalizika tarehe 7 Septemba 2019.

Katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Ben Gurion Jijini Tel Aviv, Mhe Hasunga ameagwa na mwenyeji wake Balozi wa Tanzania nchini Israel Balozi Job Daud Masima.

Katika ziara hiyo Mhe Hasunga alishiriki mahafali ya mafunzo ya Kilimo ya Agro Studies yaliyofanyika Jijini Jerusalem, Mahafali hayo yalijumuisha vijana 1600 kutoka mataifa zaidi ya 12 ambapo kati ya hao vijana 45 ni watanzania, Pia alitoa vyeti kwa vijana hao wa Tanzania 45 waliohitimu.

Waziri wa Kilimo nchini Tanzania Mhe Japhet Hasunga (Mb) akimkabidhi Cheti Dayana Novat wakati wa mahafali ya mafunzo ya Kilimo ya Agro Studies yanayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ICC (Jerusalem International Conventional Center) Jijini Jerusalem nchini Israel, Tarehe 2 Septemba 2019.

Akizungumza na vijana hao 45 mara baada ya mahafali ya mafunzo ya Kilimo ya Agro Studies, Mhe Hasunga aliwahakikishia kuwa Serikali imeridhia ombi lao la kuwapatia ardhi kwa ajili ya kuwekeza kwenye sekta ya Kilimo.

Alisema kuwa serikali ya Tanzania ina ardhi nzuri yenye rutuba ambayo haijaguswa kwa ajili ya kilimo hivyo huo ni muda mwafaka kwa vijana hao kupatiwa ardhi kwa ajili ya kuonyesha kwa vitendo waliyofundishwa wakati wa masomo yao nchini Israel.

Mhe Hasunga alisema kuwa ni wakati muafaka kwa wanafunzi hao kutumia ujuzi walioupata wa kujifunza mbinu bora na teknolojia za kisasa za kuendeleza kilimo cha umwagiliaji ili kutoa elimu ya kilimo hicho nchini mwao pindi watakaporejea.

Amesema kuwa nafasi hizo za masomo ya kilimo nchini Israel zimetoa fursa kwa wataalamu hao kuongeza ufanisi katika Sekta ya kilimo hivyo watakaporejea nchini wanapaswa kukibadilisha kilimo kuwa na tija zaidi katika uzalishaji.

Aidha, alisema kuwa, tatizo kubwa la Sekta ya Kilimo nchini ni uzalishaji mdogo usiokuwa na tija ambapo wakulima hutumia nguvu kubwa lakini matokeo yanakuwa madogo. hivyo, alisisitiza kuwa, watakaporejea nchini Tanzania wanatakiwa kutoa elimu kwa wakulima ya kuzingatia mbinu bora za kilimo, matumizi sahihi ya pembejeo, mbolea na pia kutumia mbegu bora ili kuweza kumnufaisha mkulima.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akizungumza na vijana waliohitimu mahafali ya mafunzo ya Kilimo ya Agro Studies yaliyofanyika jijini Jerusalem nchini Israel, tarehe 2 Septemba 2019.

Katika ziara hiyo nchini Israel Waziri wa Kilimo wa Tanzania Mhe Japhet Hasunga (Mb) alikutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo na Maendeleo Vijijini wa Israel Mhe Uri Yehuda Ariel HaCohen na kuridhia kwa kauli moja kuwa serikali za nchi hizo mbili kuingia makubaliano ya kuendeleza kilimo hususani katika utafiti, Tija katika uzalishaji, na Teknolojia.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania nchini Israel Mhe Job Daud Masima, Mhe Hasunga ametoa shukrani kwa Serikali ya Israeli kuipatia Tanzania nafasi 100 za kujifunza kuhusu sekta ya kilimo kwa vijana kupitia programu inayosimamiwa na Agrostudies.

Waziri Hasunga alieleza katika mkutano huo dhamira ya Serikali ya Tanzania inayoongoza na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli, ya kuwasaidia vijana waliorudi nyumbani baada ya mafunzo hayo kwa kuanza kuwapatia mahitaji ya msingi ikiwemo ardhi ambayo ipo eneo litakalowawezesha kujiendeleza.

Sambamba na hayo Waziri Hasunga alizungumzia kuhusu maeneo yanayoweza kuwavutia wawekezaji kutoka Israeli ili kuwekeza nchini Tanzania kwa kutoa takwimu za ukubwa wa ardhi yenye rutuba, uwepo wa maji na hali ya hewa inayoruhusu ukuaji wa aina nyingi za mazao.


Akizungumza kwa niaba ya Serikali ya Israeli Waziri wa Kilimo na Maendeleo Vijijini wa nchi hiyo Mhe Uri Yehuda Ariel HaCohen alimuhakikishia Waziri Hasunga kuwa Serikali ya Israeli ipo tayari kusaini hati ya makubaliano ya kilimo (Memorandum Of Undarstanding-MOU) hivyo Serikali ya Tanzania itatakiwa kuwasilisha haraka mahitaji hasa kwenye mazao ambayo muhimu ya kuanza nayo kwa ajili ya soko la Israel.
Waziri wa Kilimo wa Tanzania Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza na Waziri wa Kilimo na Maendeleo Vijijini wa Israel Mhe Uri Yehuda Ariel HaCohen wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika Ofisi za wizara hiyo eneo la Bet Dagan 50250 nchini Israel, tarehe 5 Septemba 2019.

Pia, Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) alikutana na kufanya mazungumzo na Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Innovation Africa Bi Sivan Ya’ari katika kikao kilichofanyika kwenye Ofisi za kampuni hiyo zilizopo Jijini Tel Aviv.

Mhe Hasunga alimualika Bi Sivan kutembelea nchini Tanzania ili kuwekeza kadhalika kusaidia katika maeneo mbalimbal. Alisema kuwa kampuni hiyo inatakiwa kuongeza mshikamano na serikali ya Tanzania ili kuendelea kutatua sehemu ya matatizo ya wananchi sambamba na kuimarisha mpango wao wa kutoa suluhisho la Israeli na ujuzi kwa wale wanaohitaji kuishi katika vijiji vya Kiafrika.

Waziri Hasunga amemuhakikishia Bi Ya’ari kuwa Tanzania ni nchi nzuri katika uwekezaji na sehemu salama ya kuishi huku serikali inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli ikiendeleza juhudi za kuboresha maisha ya watanzania na kuimarisha uchumi wa nchi.

Hata hivyo ameipongeza kampuni hiyo kwa kazi nzuri wanayoifanya katika nchi za Afrika katika sekta ya nishati ya jua ikiwa ni pamoja na mchango wao katika kutekeleza miradi ya maji safi, na Kusaidia vituo vya watoto yatima.

Alisema kuwa Tanzania ni sehemu salama na imara katika uwekezaji, kwani serikali imeanzisha kituo cha uwekezaji (TIC) ambacho ni Taasisi ya msingi ya serikali yenye jukumu la kuratibu, kuhimiza, kukuza na kuwezesha uwekezaji.

Kwa upande wake Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Innovation Africa Bi Sivan Ya’ari akizungumza katika kikao kazi hicho aliridhia ombi la Waziri Hasunga la kuongeza uwezekano wa kuisaidia Tanzania na kusema kuwa mwanzoni mwa mwezi wa tisa atawasili nchini Tanzania kwa ajili ya kuainisha maeneo ya uwekezaji.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza na Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Innovation Africa Bi Sivan Ya’ari mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo tarehe 4 Septemba 2019 Jijini Tel Aviv nchini Israel akiwa katika ziara ya kikazi ya siku 6. Mwingine pichani ni Balozi wa Tanzania nchini Israel Balozi Job Daud Masima.

Vilevile Mhe Hasunga alitembelea shamba la utafiti wa kilimo na kukutana na Mkuu wa Mradi wa Umwagiji Afrika wa kampuni ya Netafim Ndg Shay Haxter ambapo alimualika kutembelea nchini Tanzania kwa ajili ya uwekezaji kwenye sekta ya kilimo.

Mhe Hasunga alisema kuwa Tanzania kuna maeneo makubwa yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji ikiwemo eneo la Rufiji ambako ujenzi wa mradi wa umeme wa Bwawa la Nyerere unaendelea na punde utakapokamilika kuna matarajio ya kuwa na wastani wa hekta 150,000 zinazofaa kwa kilimo.

Waziri Hasunga pia alikutana na kuzungumza na baadhi ya wanafunzi wa Tanzania walioshiriki mafunzo ya Kilimo nchini Israel kwenye shamba la mifugo la Jacob's Farm na kujionea jinsi walivyonufaika na mafunzo hayo.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Kulia) akizungumza na Mkuu wa Mradi wa Umwagiji Afrika kampuni ya Netafim Ndg Shay Haxter mara baada ya kutembelea katika shamba la utafiti wa kilimo wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku sita nchini Israel. Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Israel Mhe Job Daud Masima.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza na baadhi ya wanafunzi wa Tanzania walioshiriki mafunzo ya Kilimo nchini Israel kwenye shamba la mifugo la Jacob's Farm, Mwingine pichani ni Balozi wa Tanzania nchini Israel Mhe Job Daud Masima (Kulia),tarehe 3 Septemba 2019.

Katika ziara hiyo ya kikazi Waziri wa Kilimo wa Tanzania Mhe Japhet Hasunga alikutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Wakurugenzi 6 wa Taasisi ya Mashav wa Wizara ya Mambo ya nje ya Israel. Ambapo mkutano huo ulihudhuriwa pia na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya agrostudies Ndg Yaron Tamir.

Katika mkutano huo wa kazi uliofanyika katika Ofisi za wizara ya Mambo ya nje ya Israel iliyopo mtaa namba 9 Yitzhak Rabin Jijini Jerusalem Waziri Hasunga aliishukuru serikali ya Israel kwa kukubali ombi la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli la kuongeza idadi ya wanafunzi wanaoshiriki mafunzo ya Kilimo ya Agro Studies katika kipindi cha mwaka mmoja kutoka 45 ambapo imefikia idadi ya wanafunzi 100.

Kadhalika kikao hicho kilijadili kwa kina namna ya kuboresha zaidi mahusiano baina ya nchi ya Tanzania na Israel hususani katika kuimarisha ushirikiano kwenye nyanja za utafiti, uongezaji thamani wa mazao, na namna ya kuongeza ukubwa wa mashamba ya kilimo na tija.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya MASHAV Balozi Gil Haskel alisema kuwa serikali ya Israel imeridhia maombi ya Waziri wa Kilimo wa Tanzania Mhe Japhet Hasunga na kusema kuwa Israel ipo tayari kushirikiana na Tanzania ili kuboresha sekta ya kilimo kutoka kwenye kilimo cha kujikimu kuwa kilimo cha kibiashara.
Waziri wa Kilimo wa Tanzania Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Israel Balozi Job Daud Masima wakati wakizungumza na ujumbe wa Wakurugenzi 6 wa Mashav wa Wizara ya Mambo ya nje ya Israel katika mkutano wa kazi uliofanyika katika Ofisi za wizara ya Mambo ya nje ya Israel iliyopo mtaa namba 9 Yitzhak Rabin Jijini Jerusalem nchini Israel, tarehe 5 Septemba 2019.
Waziri wa Kilimo wa Tanzania Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Israel Balozi Job Daud Masima wakisindikizwa na Mkurugenzi Mkuu wa MASHAV Balozi Gil Haskel mara baada ya mkutano wa kazi uliofanyika katika Ofisi za wizara ya Mambo ya nje ya Israel iliyopo mtaa namba 9 Yitzhak Rabin Jijini Jerusalem nchini Israel, tarehe 5 Septemba 2019.

Alisema Serikali ya Israel imekubali kufikiria kuongeza idadi ya vijana kutoka Tanzania wanaozuru Israel kwa ajili ya kujifunza ambapo pia wataongeza uwezekano wa wataalamu mbalimbali wakiwemo maafisa ugani nchini Tanzania kuzuru Israel kwa ajili ya kujengewa uwezo katika utendaji.

Aidha, Balozi wa Tanzania nchini Israel Balozi Job Daud Masima alisema kuwa vikao alivyovifanya Waziri wa Kilimo kwenye ziara ya kikazi ya Waziri huyo nchini Israel ambapo aliongeza kuwa vikao hivyo vimetoa taswira ya kutafakari kwa pamoja kuona namna mafunzo hayo yanavyowasaidia vijana wa kitanzania.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya agrostudies Ndg Yaron Tamir alisema kuwa wanafunzi walioshiriki mafunzo hayo kutoka Tanzania walitoa ushirikiano mzuri kipindi chote cha masomo hivyo mafunzo hayo waliyoyapata wanapaswa kuyaendeleza ili kuboresha kilimo nchini Tanzania.

Alisema kuwa Tanzania kupitia nafasi za kimasomo zinazotolewa na Israel, itazidi kunufaika kwani nchi ya Israel ni moja ya nchi zinazoongoza katika utafiti wa maendeleo ya Kilimo na Teknolojia (Agriculture Research and Development).

Katika hatua nyingine Waziri Hasunga aliwapokea vijana wa kitanzania 60 waliowasili nchini Israel kwa ajili ya kushiriki mafunzo ya Kilimo ya Agro Studies katika kipindi cha mwaka mmoja huku wengine 40 wakitarajiwa kuwasili tarehe 11 Septemba 2019 kukamilisha idadi ya vijana 100.
Waziri wa Kilimo wa Tanzania Mhe Japhet Hasunga (Mb) pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Israel wakiwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Ben Gurion Jijini Tel Aviv nchini Israel tarehe 5 Septemba 2019 mara baada ya kuwapokea vijana kutoka Tanzania waliowasili nchini Israel kwa ajili ya mafunzo ya kilimo ya Agrostudies.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Katikati) Tarehe 3 Septemba 2019 akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Israel Mhe Job Daud Masima (Kulia) katika Ofisi za Ubalozi huo zilizopo katika mtaa wa 12, Abba Hillel Silver Jijini Tel Aviv nchini Israel. Mwingine ni Mwambata Jeshi Brigedia Jenerali Kahema Juni Mziray.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com