Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo Tarehe 20 Septemba 2019 Jijini Dar es Salaam, (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo Tarehe 20 Septemba 2019 Jijini Dar es Salaam, (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Na
Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam
Serikali imetangaza ununuzi wa korosho wa
msimu mpya unaohusisha teknolojia ya
wanunuzi kujisajili kwenye Bodi ya Korosho kupitia mfumo wa Wizara ya Kilimo wa
kusimamia Biashara za Kilimo (Agricultural Trade Management Informataion System
– ATMIS).
Imeeleza pia kuhusu deni
la korosho msimu uliopita inalodaiwa na
wakulima wakubwa kuwa shilingi bilioni 50, ambalo linaendelea kulipwa kila siku
kulingana na shehena ya korosho zinazonunuliwa na wanunuzi.
Hayo yameelezwa na Waziri
wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo
Tarehe 20 Septemba 2019 Jijini Dar es Salaam.
“Msimu wa 2019/2020 mfumo wa ununuzi wa
korosho utakuwa kwa njia ya mnada wa wazi kwa kutumia jukwaa la Soko la Bidhaa
Tanzania (TMX) ambapo hakutakuwa na matumizi ya masanduku ya mnada,”alisema
Waziri.
Amesema
kuwa wanunuzi watakaosajiliwa na kukidhi vigezo watatakiwa kulipa Kinga ya
Dhamana (Bid Security) kutegemeana na kiasi cha korosho mnunuzi anachotaka
kununua kupitia kwenye akaunti ya usuluhishi inayomilikiwa na Soko la Bidhaa.
“Mfumo
huu utaruhusu wanunuzi mbalimbali kutoka maeneo mbalimbali duniani kushiriki
katika mnada. Wanunuzi wa nje ya nchi wataweza kushiriki katika mnada moja kwa
moja na hawatalazimika kufungua makampuni hapa nchini,” alisema Waziri.
Amesema badala yake wanunuzi hao watadhaminiwa
na benki za malipo (Settlement Bank) zinazotambuliwa na Soko la Bidhaa (TMX)
hivyo kuongeza ushindani katika minada.
“Benki za malipo zitawajibika kutoa uhakikisho
wa uwepo wa fedha kwa ajili ya malipo ya korosho kwa mujibu wa taratibu za soko,”alisema.
Akizungumzi kuhusu wanunuzi wa ndani na nje ya
nchi alisema wataruhusiwa kununua korosho
ghafi kwa mafungu (stakes) kati ya tani 50 mpaka tani 500 kulingana na
mahitaji.
“Korosho hizo katika mafungu (stake) zitapangwa
kulingana na vigezo vya ubora na daraja.
Kiwango cha korosho kitakachouzwa katika kila kikao (mnada) kitatokana
na taarifa zilizopo katika katalogi ya mauzo,” alisema.
“Mnunuzi atalazimika kununua kiasi chote cha
korosho kilichopo katika fungu katika kikao kimoja ili kuwezesha utoaji wa korosho katika ghala
kwa kutumia utaratibu wa korosho za kwanza kuingia ndizo za kwanza kutoka
(first in, first Out- FIFO),”alifafanua Waziri.
Alisema Wanunuzi wenye leseni watapewa msimbo (code)
maalumu watakazozitumia kuingia kwenye mfumo na kushiriki katika minada.
Mnunuzi atakaeshinda katika mnada atawajibika kulipia korosho alizoshinda ndani
ya siku tatu (3) baada ya mauzo kufanyika.
Malipo yote yatafanyika kupitia benki za malipo
(Settlement Bank) zinazotambuliwa na Soko la Bidhaa. Soko la bidhaa litawalipa
wadau wote kwa mujibu wa sheria ndani ya siku mbili tangu mnunuzi kukamilisha
malipo husika.
Waziri alieleza kuwa utaratibu huu utaondoa ulazima wa
wanunuzi kusafiri kutoka eneo moja kwenda lingine ili kushiriki minada ya
korosho.
“Minada ya mauzo ya korosho itafanyika siku
mbili kwa wiki katika maghala yote kulingana na upatikani wa korosho, minada
itakuwa siku ya Jumanne na Alhamisi,” alisema.
Waziri Hasunga amesema lengo la utaratibu huu
mpya ni kupanua wigo wa soko ambao wanaamini utaongeza chachu ya ushindani na
kuwezesha bei nzuri zaidi kupatikana kulingana na mwenendo katika soko la
dunia.
Kupitia jukwaa la Soko la Bidhaa kutakuwa na
wigo mpana kwa wanunuzi, kutakuwa na uwazi wa bei za korosho na wakulima
watalipwa haraka zaidi na kwa wakati.
Alisema lengo la Serikali ni kuona wakulima
wote wanalipwa fedha zao moja kwa moja
kwenye akaunti zao binafsi katika Benki zilizopo katika maeneo yao ya
uzalishaji.
“Msimu wa ununuzi
wa korosho Mwaka 2019/2020 kwa sasa umefunguliwa rasmi. Katika msimu wa
2019/2020 tunategemea kuzalisha tani 300,000 za korosho ghafi kutoka tani
224,000 zilizozalishwa 2018/2019 ikiwa ni ongezeko la asilimia 34%,” alisema
Waziri.
Alibaiisha kuwa Wizara ina mikakati mbalimbali ya kuongeza
uzalishaji ikiwa ni pamoja na Kuhamasisha matumizi sahihi ya viutilifu bora na kuhakikisha upatikanaji wa viuatilifu hivyo
kwa wakati na kwa bei nafuu pamoja na kutoa mafunzo kwa wakulima.
Waziri alisema kuwa matumizi
sahihi ya viuatilifu yataongeza tija miongoni mwa wakulima kutoka wastani wa
kilo 10 kwa mti kwa mwaka hadi kufikia kilo 35 kwa mti kwa mwaka.
Alisema Wizara yake kupitia Bodi ya korosho imeongeza
maeneo mapya yanayolima korosho kutoka mikoa mitano ya awali ambayo ni Mtwara,
Lindi, Ruvuma, Pwani na Tanga na kufikia mikoa 17.
“Mikoa mingine inayolima korosho kwa sasa ni Dodoma,
Singida, Tabora, Mbeya, Iringa, Kilimanjaro, Katavi, Morogoro, Songwe,Kigoma,
Njombe na Shinyanga,”alisema.
Katika musimu wa mwaka 2018/2019 serikali iliamua kununua
korosho zote toka kwa wakulima kutokana na kuyumba au kushuka kwa bei ya
korosho katika soko la minada.
“Hatua hii ilikuwa ni ya dharura iliyochukuliwa ili
kulinda maslahi ya mkulima, kuanza mkakati wa kubangua korosho zote hapa
nchini, kufufua viwanda vya kubangua korosho vilivyopo na kuongeza ajira kwa
watanzani,”alisema.
Lengo la Serikali
ya Tanzania chini ya Rais John Magufuli ni kuhakikisha kuwa wakulima
wananufaika na mazao yao na kupata bei nzuri kulingana na mwenendo wa soko.
Bei ya korosho ghafi katika Mwaka 2018/2019 iliyotolewa na
wanunuzi ilikuwa ndogo sana, ikilinganishwa na bei ya Msimu wa 2017/2018.
Utekelezaji wa maamuzi na maagizo hayo ulifanywa
kwa ushirikiano mkubwa kati ya wizara ya kilimo, viwanda na biashara, wizara
ya Ulinzi na Jeshi la kujenga taifa,
TAMISEMi, na wizara ya mipango na Fedha.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment