METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, September 1, 2019

AFRECO KUIPA BASI HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA

******************
TAASISI ya Association of African Economy and Development in Japan (AFRECO) imeahidi kuipatia Hospitali ya Benjamin Mkapa ya Chuo Kikuu cha Dodoma basi ambalo ni hospitali kamili litakalotoa huduma za matibabu kwa Manispaa ya Dodoma, Mikoa na Wilaya zinazoizunguka Mkoa wa Dodoma.
Basi hilo litakapowasili nchini kutoka Japan linatarajiwa kuwa ni mkombozi kwa wananchi waishio vijijini na katika maeneo ambayo hayana hospitali kwani kila litakakokwenda kutoa huduma litakuwa na madaktari waliobobea katika utaalamu wa tiba mbalimbali, vifaa tiba, maabara pamoja na dawa.
Hayo yamebainishwa leo (Jumapili, Septemba 1, 2019) na Rais wa   AFRECO, Bw. Tetsuro Yano katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa yaliyofanyika kwenye hoteli ya Yokohama Bay nchini Japan.
Bw. Yano amesema wameamua kuanza kutoa misaada na huduma zao nchini Tanzania baada ya kufurahishwa na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli za kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Ameongeza kuwa anaamini siku moja Tanzania itakuwa nchi ya mfano kwa Afrika Mashariki na Afrika yote kwa kutoa huduma bora za tiba kwani itakuwa na vituo vingi vya Afya na hospitali zenye uwezo wa kutibu magonjwa kama vile ya moyo na figo. Hata  hivyo tayari wagonjwa toka nchi jirani wameanza kuja kutibiwa nchini.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu amesema mbali na kutoa basi ambalo litakuwa linatoa huduma za matibabu, pia taasisi hiyo ya AFRECO   itasaidia katika kupandisha hadhi hospitali ya Benjamin Mkapa ya Chuo Kikuu cha Dodoma kuwa Shule kamili ya tiba.
Amesema hospitali hiyo ya Benjamin Mkapa ya Chuo Kikuu cha Dodoma itapatiwa vifaa   mbalimbali vya tiba ambavyo vitaifanya hospitali hiyo kuwa ni shule bobezi   kwa utoaji wa tiba mbalimbali nchini Tanzania na Barani Afrika.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kuwa wamekubaliana na AFRECO kuanzisha kitivo maalum cha Uhandisi wa Vifaa Tiba ambacho kitafundisha uhandisi wa vifaa tiba ili nchi yetu iwe na watalaamu wa  kukarabati vifaa tiba pindi vinapoharibika badala kuvipeleka nje ya nchi au kuagiza wahandisi na watalaamu kutoka nje ya nchi kuja kuvitengeneza.
“Hivi sasa yanafanyika makubaliano ya kuanzisha   kiwanda cha kutengeneza vifaa tiba na kwa kuanzia wataanza kutengeneza maji ya drip ambayo huongezwa kwa wagonjwa kwa maeelekezo ya madaktari na baadae watengeneza dawa mbalimbali.”
Naye,Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma,  Mipango, Utawala na Fedha, Profesa Donald Mpanduji amesema wametia saini hati ya makubaliano kati ya  AFRECO na Chuo Kikuu cha Dodoma ambayo yanalenga kuboresha hospitali ya Chuo Kikuu cha Dodoma.
Awali, Dkt. Omary Ubuguyu kutoka Wizara ya Afya amesema maboresho yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika huduma za tiba yameiwezesha Tanzania kupunguza wagonjwa wanaopelekwa nchi za nje kwa matibabu kutoka 800 hadi 42  ambalo ni punguzo la  asilimia inayotajwa kuwa 200.
Amesema hatua hiyo imeongeza nafasi kwa watalaamu wetu wa tiba kujifunza zaidi pamoja na kuwapunguzia wananchi gharama za kusafiri kwenda nje ya nchi kutafuta tiba na pia imeipunguzia Serikali gharama ya fedha za kigeni ambazo zingetumika kuwatibu wagonjwa nje ya nchi.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com