METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, August 31, 2019

TANZANIA IMEAMUA KUENDELEA KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO

Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo jijini Dodoma wakati wa kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo kupitia miradi mbalimbali inayofanywa na Rais Dkt.Pombe Magufuli
……………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi,amesema kuwa Tanzania imeendelea kupanda kutokana na nia njema na shughuli kubwa  inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika kuwaletea  wananchi  Maendeleo kupitia miradi mbalimbali.
Hayo ameyasema leo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na utekelezaji wa Serikali kwa mwezi Agosti 2019.
Dkt.Abbasi,amesema kuwa kwa mujibu wa Ripoti iliyotolewa Julai 12, 2019 kwa pamoja kati ya Transparency International na Afro-Barometer, Tanzania imeongoza katika nchi 35 kwa kuonesha juhudi za wazi katika kupambana na rushwa.
“Mafanikio haya yanatokana na msimamo thabiti wa Mhe. Rais Magufuli na Serikali yake katika kuimarisha taasisi muhimu kama vile TAKUKURU, Kuanzisha Mahakama ya Ufisadi na Uhujumu Uchumi, mfumo wa udhibiti wa rushwa katika manunuzi kupitia PPRA”, amesisitiza Dkt. Abbasi.
Hata hivyo ametolea mfano kwa TAKUKURU kuwa  imeokoa jumla ya shilingi bilioni 86 zilizotokana na mishahara hewa na ukwepaji kodi.
Dkt.Abbasi amefafanua  kuwa jumla ya shilingi bilioni 25.5 zimerejeshwa Serikalini kwa mchanganuo ufuatao; bilioni 14.6 ikiwa ni urejeshwaji wa mali zilizopatikana kwa njia ya uhalifu na bilioni 10.9 zilizotokana na thamani ya mali zilizotaifishwa yakiwemo magari, vituo vya mafuta, nyumba nane, magari nane na Bilioni 20 ambazo ni mali zilizozuiwa kesi zikiendelea.
Amesema kuwa kwa upande wa Mamlaka ya Usimamizi wa Manunuzi ya Umma (PPRA) imeokoa takribani shilingi bilioni 46.9 zilizokuwa zipotee kutokana na kutofuatwa taratibu za ununuzi, malipo ya zaidi ya mkataba kwa wakandarasi au baadhi kutorudisha fedha walizopewa kama dhamana na uzembe na rushwa.
Aidha ameelezea utekelezaji katika sekta ya uchukuzi, Dkt. Abbasi amesema kuwa Serikali imeanza zabuni ya kuagiza vichwa 22 (vitano vya mafuta yaani Diesel Locomotive na 17 vya umeme yaani Electrical Locomotive) na mabehewa ya abiria 60 na 1430 ya mizigo.
Aidha ameongeza kuwa, Serikali imeanza zabuni ya treni tano (5) zilizokamilika (Electrical Multiple Unit) za abiria zenye mabehewa nane (8) kila moja na vichwa viwili kwa ajili ya uendeshaji wa treni za abiria kwa kipande cha Dar es salaam hadi Morogoro na kisha Dodoma.
Dkt.Abbasi ameongelea kuwa, Serikali imetenga fedha za ndani shilingi Bilioni 71.4 kwa ajili ya ujenzi wa Daraja jipya la Mto Wami lenye urefu wa Mita 513.5 litakalojumuisha ujenzi wa barabara za KM 4.3 kwa kila upande ambapo kazi ya ujenzi huo imeshaanza.
Pia, Serikali imesaini mkataba wa shilingi bilioni 699.9 kwa ajili ya ujenzi wa Daraja refu zaidi Afrika Mashariki na Kati la Kilometa 3.2 kuunganisha mikoa ya Mwanza na Geita kwenye eneo la Kigongo-Busisi katika Ziwa Victoria.
Katika Sekta ya Afya, Dkt Abbasi amesema kuwa, Serikali imeshatoa shilingi bilioni 30 kwa ajili ya Ujenzi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa (RHH) na sehemu nyingi ujenzi umekamilika. Mikoa husika ni; Mwanza, Simiyu, Njombe, Songwe, Katavi, Geita na Dar es Salaam (Mwananyamala) na kuna Bilioni 3 imetolewa Kujenga Hospitali ya Kanda ya Wazazi Mbeya na shilingi bilioni 6.32 kujenga Hospitali ya Kanda Mtwara.
katika kuwekeza katika maisha ya watu ngazi ya Wilaya, Serikali mapema mwaka huu ilitoa shilingi Bilioni 105 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya 67 ambapo katika miaka zaidi ya 50 ya Uhuru tumekuwa na Hospitali katika Wilaya 77 tu; ndani ya mwaka huu mmoja zinajengwa 67 ambapo ujenzi umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90.
Hata hivyo Dkt.Abbasi amewahakikishia Watanzania kuwa azma yetu ya kuiendeleza nchi kwa kasi chini ya Rais Dkt. Magufuli inaendelea kushika kasi na katika hili hakuna mwanadamu wa kuzuia wala kuirudisha nyuma.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com