Na Mwandishi Wetu,MAELEZO
DAR ES SALAAM
MWENYEKITI Mpya wa Baraza la
Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, Prof. Palamagamba
Kabudi amezitaka Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)
kuendelea kushikamana katika Umoja na Mshikamano baina yao ili kujenga
Uchumi imara na kuleta Maendeleo ya wananchi wake.
Akizungumza katika hafla ya
kukabidhiwa nafasi hiyo leo Jijini Dar es Salaam, Prof. Kabudi ambaye
pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Afrika Mashariki wa
Tanzania, alisema wakati umefika kwa Nchi za SADC kuungana pamoja katika
kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika taasisi mbalimbali za
kikanda na kujenga msingi imara wa ushirikiano.
Prof. Kabudi alisema kwa miaka
mingi Nchi za SADC zimekuwa na ushirikiano mkubwa baina yao hivyo wakati
umefika kwa wananchi wa Mataifa hayo kushuhudia manufaa ya ushirikiano
huo yakileta manufaa makubwa katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na
kiutamaduni.
Aliongeza kuwa Tanzania kwa upande
wake imeendelea kuwa nchi rafiki na mshirika wa karibu kwa mataifa yote
ya SADC kama inavyojidhihirisha katika historia ya mapambano ya uhuru
wa Nchi nyingi za Kusini mwa Afrika, ambapo mataifa mbalimbali yaliweka
kambi kwa ajili ya wapigania uhuru wake katika harakati zao za kudai
uhuru kutoka kwa wakoloni.
“Mwaka huu tunatimiza miaka 20
tangu kufariki wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Kiongozi shupavu
aliyejitoa pamoja na viongozi wengine wa SADC katika kupigania harakati
za ukombozi wa Afrika, tunapaswa kumuenzi kwa kuhakikisha tunaimarisha
umoja na ushirikiano uliopo kwa maslahi ya wananchi wetu” alisem Prof.
Kabudi.
Prof. Kabudi aliwataka Viongozi wa
SADC kuimarisha Umoja kwa kuwa ndiyo silaha kubwa ya ushindi katika
kujenga mazingira bora ya uwekezaji na biashara ndani ya Nchi za SADC
pamoja na kutoa ushirikiano wa karibu zaidi kwa sekta binafsi kwa ajili
ya kuibua na kujenga fursa za uchumi jumuishi.
Naye Katibu Mtendaji wa SADC, Dkt.
Stegomena Tax alisema jumuiya hiyo imekuwa ikitekeleza programu na
miradi mbalimbali ya ushirikiano wa kikanda ndani ya jumuiya hiyo ambayo
tayari imeleta mafanikio makubwa kupitia utekelezaji wa Mpango Mkakati
wa Jumuiya hiyo ambao umeweza kutumia rasilimali mbalimbali ikiwemo
madini na nishati kwa ajili ya kujenga uchumi jumuishi.
Anaongeza kuwa katika Mkutano huo
wa 39 unaotarajiwa kuhitimishwa na Mkutano Mkuu wa Marais wa Nchi za
Jumuiya hiyo tarehe 17-18 Agosti mwaka huu, Sekretarieti ya Baraza hilo
imeweza kuzindua Baraza la Biashara la SADC ambalo litakuwa chachu ya
kuunganisha sekta binafsi na ile ya umma katika kujenga uchumi jumuishi
kupitia ajenda ya viwanda pamoja na usimamizi wa rasilimali mbalimbali
ndani ya jumuiya hiyo.
Akizungumzia kuhusu majanga ya
kibinadamu ndani ya SADC. Dkt. Tax alisema kati ya Mwezi Machi-April
Jumuiya hiyo ilipata majanga ya kibinadamu katika Nchi za Msumbiji,
Malawi na Zimbabwe, ambapo pamoja na changamoto hiyo Wakuu wa Jumuiya
hiyo waliungana pamoja na kuweza kuzisadia nchi hizo kwa kutoa misaada
mbalimbali ya kibinadamu ikiwemo madawa na vyakula.
Kwa upande Mwenyekiti wa Baraza
hilo anayemaliza muda wake, ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Mambo ya Nje wa Namibia, Netumbo Ndaitwah alisema Umoja na mshikamano
wa Jumuiya hiyo umeendelea kuimarika kwa kuwa nchi nyingi zimeendelea
kuwa katika hali ya umoja, amani na utulivu.
0 comments:
Post a Comment