Katika muendelezo wa ziara yake Mkoani
Mwanza, leo Katibu Mkuu wa CCM Dk. Bashiru Ally amefika wilayani Magu,
ambapo katika vikao vitatu tofauti amesisitiza mabalozi nchi nzima
kutokupanga foleni katika ofisi yeyote ya Serikali ama ya CCM.
Akiambatana na viongozi wa chama na
serikali wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza Ndg. Anthony
Diallo, Katibu Mkuu amekutana na wanachama, mabalozi, na wajumbe wa
halmashauri kuu za kata zote na matawi yote wilayani Magu katika vikao
vitatu tofauti.
Katibu Mkuu ameeleza kuwa, mabalozi nchi
nzima hawatakiwi kukaa foleni katika ofisi yoyote ya serikali na chama,
kuanzia ofisi za watendaji wa mitaa, watendaji wa kata, wakuu wilaya,
wakurugenzi, wakuu wa mikoa mpaka ofisi za wizara yoyote nchini, kwa
sababu mabalozi ndio watu wanaofanya kazi kuliko kiongozi yeyote, kwa
kuhangaika na changamoto za mwananchi mmoja mmoja katika eneo lake, bila
ya mshahara na wanajitolea wakati wote.
“Nitoe rai kwa niaba ya Chama Cha
Mapinduzi nchi nzima kwa viongozi wa serikali na Chama, wakuu wilaya na
mikoa, wakurugenzi wote wa Halmashauri nchi nzima, makatibu wa wilaya na
mikoa nchi nzima, hawa viongozi wetu wajumbe wa mashina ni marufuku
kukaa foleni kwenye ofisi zenu, hawa ni viongozi na wamebeba watu nyuma
yao, wanapokuja ofisini wanakuja kueleza hisia, changamoto, na ushauri
wa watu wao wanaowaongoza. Kiongozi yeyote atakaye wadharau mabalozi
wetu huyo hatufai ndani ya Chama na serikali hii ya CCM.” Dk. Bashiru
amesisitiza.
“Wajumbe wa mashina ni watu muhimu sana
na wamekuwa wakifanya kazi hizi ngumu kwa uzalendo wao pasipo malipo ya
mshahara, wanajitoa wakati wote kusaidia watu, wanajua changamoto za
mwananchi mmoja mmoja na wakati mwingine hawalali kwa ajili ya shida za
watu wanaowaongoza, wanafanya yote haya kwa kujitolea na uzalendo kwa
nchi yetu, sitaki nisikie wanawekwa foleni katika ofisi yoyote ya umma,
hata ofisini kwangu nikisikia balozi amekuja kutaka kuongea na mimi ni
lazima nimpe kipaumbele kwa sababu najua hawa ndio wanaishi na watu.”
Katibu Mkuu amefafanua.
Katika vikao hivo Dk. Bashiru amepata
fursa ya kusikiliza kero za wananchi, ambapo wananchi wameonesha kuwa na
hamu kubwa ya kusikilizwa kero zao za muda mrefu na kutopata wasaa wa
kukutana na viongozo wa maeneo yao, kuelezwa na kufafanuliwa mambo
mbalimbali yanayohusi changamoto zao.
Katika hatua hiyo Dk. Bashiru ameendelea
kukazia maelekezo ya Mh. Rais John Pombe Magufuli kuwataka viongozi wote
kuanzia ngazi za msingi mpaka taifa kutenga muda katika maeneo yao kuwa
karibu na wananchi, kuwasikiliza kero zao, na kuwapatia ufafanua kwa
kuzingatia hali halisi kama afanyavyo Rais mara kwa mara apatapo muda
ofisini au akiwa ziarani, kama alivyofanya kwa wachimbaji wadogo,
wafanyabiashara n.k.
“Kila mmoja katika eneo lake la uongozi
asikilize watu, atoe ufafanuzi juu ya masuala yanayowatatiza wananchi,
awe karibu na wananchi. Hatuwezi kumuachia Mh. Rais aendeshe nchi hii
peke yake wakati ametupatia mamlaka ya kutenda na kusaidia watu.” Katibu
Mkuu amesisitiza.
Akiwa wilayani Magu Katibu Mkuu ameweka
jiwe la msingi la na kushiriki ujenzi wa Hosteli za CCM na kukagua mradi
wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) wa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa
ambapo amewaongezea ng’ombe mmoja ili kuimarisha mradi utakao wezeshe
shughuli za Chama na Jumuiya.
Ziara ya leo wilayani Magu ni muendelezo
wa kutekeleza jukumu la viongozi wa CCM kufuatilia utekelezaji wa
maelekezo ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.
0 comments:
Post a Comment