Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Wiliam Ole Nasha akizungumza na viongozi na wafanyakazi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe wakati wa ziara yake ya kukagua
maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya sekta a elimu wilayani humo.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Wiliam Ole Nasha akisikiliza maelezo kuhusu utekelezaji wa
mradi wa ujenzi na ukarabati wa Chuo cha Ufundi cha Halmashauri ya
Wilaya ya Karagwe
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Wiliam Ole Nasha akizungumza na wanafunzi wa wanaosoma katika
Chuo cha Ufundi cha Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, ambapo
amewasisitiza kusoma kwa bidii na kuwataka kuthamini mafunzo
wanayoyapata kwani muhimu katika kujiletea maendeleo na kushiriki katika
kukuza uchumi wa nchi.
Baadhi ya majengo yanayojengwa
katika Chuo cha Ufundi cha Halmashauri ya Wilaya yaa Karagwe, ambapo
serikali kupitia wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetenga zaidi
ya shilingi bilioni nne kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu
ya majengo katika chuo hicho.
…………………….
Serikali kupitia Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia imetoa zaidi ya shilingi bilioni 4.6 kutekeleza
mradi wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya majengo ya Chuo cha
Ufundi cha Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe.
Hayo yamesemwa Wilayani Karagwe na
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha katika
ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya sekta ya elimu
katika wilaya hiyo, ambapo amesema lengo la kutekeleza mradi huo ni
kuongeza udahili wa wanafunzi wanaochukua masomo ya ufundi.
Ole Nasha amesema serikali imeweka
mkakati wa kukarabati na kujenga vyuo vya ufundi katika kila wilaya,
kwani ili kufikia uchumi wa viwanda ni muhimu kama nchi kuwa na vijana
wenye maarifa na stadi mbalimbali za ufundi zitakazowawezesha kuajiriwa,
kujiajiri na kushiriki katika uchumi wa viwanda.
“Rais ameweka nguvu nyingi katika
kuinua uchumi wa nchi yetu, mnaona sasa miradi mikubwa inakuja,
hospitali zinajengwa, barabara za lami nyingi zinajengwa, kwa hiyo kuna
mambo mengi yanafanyika katika ujenzi na miradi yote hii yote yanahitaji
ufundi, hivyo mtambue ufundi ni kitu muhimu sasa” ameongeza Ole Nasha.
Wakati huo huo, Naibu Waziri
ametoa miezi mitatu kwa wakala wa majengo Tanzania (TBA) kuhakikisha
wanamaliza ujenzi na ukarabati wa chuo hicho, ambapo amesema
hajaridhishwa na sababu zilizotolewa na mhandisi msanifu kutoka TBA
zilizopelekea kutokamilika kwa mradi kwa wakati.
Ole Nasha anesisitiza kuwa hakuna
wakati wowote ambao fedha iliyopaswa kutolewa imeshindwa kutolewa na
VETA kwani mpaka sasa TBA imeshalipwa zaidi ya shilingi bilioni moja
ambayo ni asilimia 25 ya fedha yote iliyopaswa kulipwa wakati ujenzi
umefikia asilimia 44 tu.
Awali Mhandisi Msanifu wa Wakala
wa Majengo Tanzania (TBA), Kelvin Joas alimweleza Naibu Waziri kuwa
kutokukamilika kwa mradi huo kwa wakati nikutokana na changamoto
mbalimbali zilizojitokeza ikiwemo za kimkataba na kuwapelekea kuomba
kuongezewa muda wa miezi sita baada ya muda wa mkataba kuisha Julai
26,2019.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya, Godwin Kitonka amesema Halmashauri yake
inaishukuru serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa
kutenga fedha zaidi ya bilioni 4.6 kwa ajili ya kujenga majengo mapya
ambayo ni pamoja na jengo la utawala, ukumbi mdogo, vyoo vya nje, bweni
la wasichana na kukarabati karakana ya ushonaji na uchomeleaji chuma.
Mwanafunzi Masau Josephat,
ameishukuru serikali kwa kuboresha mazingira ya kufundishia na
kujifunzia pamoja na kuongeza majengo ambayo awali hayakuwepo kwani
mwanzoni hayakuwa yakiidhisha, huku wakiiomba serikali kuongeza baadhi
ya kozi ambazo hazipatikani chuoni hapo ili kupanua wigo wa upatikanaji
wa maarifa na stadi kwa vijana wa Karagwe na maeneo ya jirani.
0 comments:
Post a Comment