
Waziri wa Madini, Doto Biteko
akizungumza na wachimbaji wadogo (hawapo pichani) wa madini katika
ukumbi wa mkutano wa Uvinza alipofanya ziara ili kusikiliza changamoto
zao na kuzitafutia ufumbuzi tarehe 29/July, 2019.

Waziri wa Madini, Doto Biteko
akisikiliza jambo kutoka kwa wachimbaji walioshiriki mkutano baina yake
na wachimbaji wadogo wa Madini wa Uvinza kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya
ya Uvinza Bi. Mwanamvua H. Mrindoko.

Wachimbaji wadogo wa Madini
Uvinza, wakimsikiliza waziri wa Madini Doto Biteko (hayupo pichani)
wakati wa kikao baina ya waziri Biteko na wachimbaji wadogo wilayani
Uvinza mkoani Kigoma.

Afisa Madini Mkazi wa Kigoma
akitoa taarifa fupi ya madini wakati wa Mkutano baina ya Waziri wa
Madini Doto Biteko na wachimbaji wadogo (hawapo pichani) wa madini
katika ukumbi wa mkutano wa Uvinza alipofanya ziara ili kusikiliza
changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi tarehe 29/July, 2019.

Meneja wa kiwanda cha chumvi cha
uvinza Ben Mwaipopo wa kwanza kushoto na Meneja Mkuu wa kuwanda hicho
Mukash Mamlani Wa pili kulia wakimwonesha kitu Waziri wa Madini Doto
Biteko wa kwanza kulia alipokuwa akikagua shamba la chumvi la uvinza.

Waziri wa Madini, Doto Biteko
ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Uvinza ukishirikiana na kiwanda cha
chumvi cha Uvinza, pamoja na ofisi ya Madini Mkoani Kigoma kujadili
namna ya kuanzisha soko la chumvi katika halmashauri hiyo.
Maelekezo hayo yametolewa
kufuatia maombi ya wananchi wa halmashauri hiyo ya uvinza kulalamikia
ukosefu wa soko la kuuzia bidhaa hiyo na kuiomba serikali kufanya
utaratibu wa kufungua soko ili kuwawezesha kufanya biashara yao mahali
salama.
Agizo hilo limetolewa tarehe 29
July, 2019 katika ofisi za Kiwanda cha Chumvi cha Uvinza mara baada ya
Waziri Biteko na ujumbe alioambatana nao kuwasili kwa lengo la
kuzungumza na uongozi wa kiwanda hicho ili kuweka sawa mambo mbalimbali
yaliyowasilishwa na wananchi wakati wa mkutano baina ya Waziri Biteko na
Wachimbaji wadogo pamoja na wananchi wa Uvinza.
Moja kati ya malalamiko
yaliyomfikia waziri Biteko ni malipo duni ya ujira kwa wafanyakazi wa
kiwanda hicho ambapo aliutaka uongozi wa kiwanda hicho kujadili na
kufikia maamuzi ya kuongeza ujira kwa wafanyakazi wa kiwanda hicho
waliodai kulipwa ujira mdogo.
Aidha, Biteko aliutaka uongozi wa
kiwanda hicho kufanya marekebisho hayo mpaka ifikapo tarehe mosi mwezi
Agosti, 2019 mara baada ya Kiwanda kufanya mahesabu na kujiridhisha juu
ya kiasi kinachobaki baada ya kutoa gharama za uwekezaji kiongezwe
katika malipo hayo ya ujira.
Akijibu hoja ya baadhi ya
wananchi wa Uvinza waliolalamikia uongozi wa kiwanda hicho kuuza chumvi
inayozalishwa kiwandani hapo hiyo bei kubwa inayowafanya walanguzi hao
kupata faida kidogo, Biteko aliutaka uongozi wa kiwanda hicho na
wachimbaji wengine wa chumvi wilayani humo kupunguza bei hiyo ili
kuiwezesha jamii inayowazunguka kunufaika na uwepo wa chumvi katika mji
wao.
Biteko aliutaka uongozi wa
kiwanda cha chumvi kuwapa wananchi sababu ya kuwapenda kwa kuwatendea
mema. Aliendelea kwa kusema mtu mwenye kurekebisha bei ya chumvi kwa
manufaa ya wafanyabiashara wadogo ni mwekezaji mkubwa. “ifanye jamii hii
iugue siku ukiwa haupo, Ifanye jamii ikukumbuke kwa mema yako” Biteko
alisisitiza.
Pamoja na hayo Waziri Biteko,
aliutaka uongozi wa Halmashauri ya Uvinza, Ofisi ya Madini ya Mkoa wa
Kigoma pamoja na uongozi wa kiwanda kukutana na kujadili namna na mahali
patakapofaa kwa ajili ya kuanzisha soko la madini ili kuwaondolea adha
ya soko la chumvi wananchi wa Uvinza.
Kufuatia malalamiko ya wananchi
wa Uvinza ya kutozwa kiasi cha Tzs 500 ya ushuru kwa kila kilo 25 za
chumvi, Waziri Biteko aliiagiza halmashauri ya Uvinza kufuta tozo hiyo
na kueleza kuwa tozo hiyo haipo chini ya mamlaka yake na hivyo
haitambui.
Akijibu kero ya mwananchi wa
uvinza aliyejulikana kwa jina la Yona William Gwagula kwa niaba ya
wanakikundi wa Twikome Salt Kinyo Chakuru juu ya watu waliokuwa
wakiwatoza kodi kwa madai kuwa leseni iliyokuwa ikichimbwa na
wanakikundi hao ni ya kwao jambo lililobainika kuwa si kweli, Waziri
Biteko alimtaka Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kigoma David William
Ndosi, kuifuta leseni hiyo mara moja na kuwapa wachimbaji hao wadogo ili
waweze kuendeleza shughuli zao.
Kwa upande wake, Katibu wa
Wachimbaji Wadogo wa Wilaya ya Uvinza, Hamisa Omari Kambi akiwasilisha
changamoto wanazokumbana nazo alisema ni pamoja na maeneo yao kuvamiwa,
ukosefu wa vitendea kazi, halmashauri kutowapa kipaumbele wamiliki wa
leseni kwenye tenda za Serikali pamoja na kuomba kurahisishwa kwa
utolewaji wa vibali vya kusafirisha Madini nje ya nchi ambapo
changamoto zote zimepatiwa ufumbuzi.
Waziri Biteko atakuwepo Mkoani
Kigoma kwa ziara ya siku mbili ambapo atafanya majadiliano na ofisi ya
Mkoa wakishirikiana na Ofisi ya Tume ya Madini ili kujadili namna bora
ya kuimarisha soko la Madini litakalowezesha kuweka mazingira rafiki na
salama kwa ajili ya nchi jirani ya Kongo, kutokana na kuonesha nia ya
kushirikiana na Tanzania katika biashara ya Madini kupitia masoko
yaliyoanzishwa hususani mkoani Kigoma.
0 comments:
Post a Comment