Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Dkt. Bashiru Ally,leo ametoa wito kwa wanachama wa chama hicho kuwapuuza
wale watu wanaoendeleza mjadala usiokuwa na tija ndani ya chama hicho,
na akawahakikishia kwamba chama hicho kiko imara.Dk. Bashiru ameyasema hayo wakati akitoa pongezi kwa hatua
ya wanaCCM Mkoa wa Dodoma, kutaka Kanali Abdulrahman Kinana na Yusuf
Makamba, makatibu wastaafu wa CCM kuchukuliwa hatua. Hii ni baada ya makatibu hao wastaafu wiki iliyopita,
kumwandikia barua Pius Msekwa, Katibu wa Baraza la Viongozi Wastaafu wa
CCM wakilalamikia kuchafuliwa na Cryspian Musiba, anayejitambulisha kuwa
mtetezi wa Rais John Magufuli. Kwenye barua hiyo, Makamba na Kinana wamelalamika kuchafuliwa
na kuzushiwa huku wakidai serikali imeshindwa kuchukua hatua. Hata
hivyo,wamehoji ‘ulinzi’ anaopewa Mtu huyo anayewachafua.
“Wapuuzeni, hatuogopi kukosolewa, lakini hatuko tayari
kudharauliwa, kutukanwa na kubezwa na majina yaliyo na kebehi na watu
wasio na shukrani. Hatujafunzwa hivyo, hatujazoea hivyo,” amesema
Dk.Bashiri bila kutaja jina lolote. Aidha, Dk. Bashiru amesema, uongozi wa CCM hautaruhusu
malumbano ndani ya chama hicho, huku akieleza kwamba mwenyekiti wake,
Dk. Magufuli yuko tayari kuwasamehe, ili kukijenga chama. “Msijifanye majasiri wa kupambana na malumbano, hakuna ruksa hiyo kwenye chama chetu. Waacheni waseme watachoka wenyewe. “Ole wake mwanaCCM yeyote atakayetaka kutumia fursa ya
malumbano hayo kutafuta kiki, ya kisisasa ili achaguliwe kwenye Serikali
za mtaa, hapana msifanye hivyo. “Jifunzeni kutoka kwa kiongozi wetu ambaye wakati wote hana
muda wa malumbano. Amevumilia, wanaomtusi wengine wana umri wa watoto
wake amewavumilia na yuko tayari kuwasamehe pia. Lakini kwa kufanya
hivyo si kwamba ni muoga. “Mwalimu Julius Nyerere alishatuasa tujisahihishe, kujisahihisha ni kujiimarisha,
tujikosoe, tukosoane kwa adabu kwa nidhamu tuache utoto.Kisiwe chama
cha siasa za kipuuzi, sababu majira haya ni ya uchaguzi,” amesema Dk.
Bashiru.
0 comments:
Post a Comment