Mhasibu Mkuu wa
Serikali Bw. Francis Mwakapalila, akiwahimiza washiriki wa mafunzo ya
Mfumo mpya wa Ulipaji Serikalini- MUSE, kutoka Wakala wa Barabara za
Vijijini na Mijini- TARURA, kuhakikisha wanauelewa na wanautumia ili
kuiwezesha Serikali kupata taarifa za Fedha kwa wakati, katika ukumbi wa
Hazina Ndogo mkoani Morogoro.
Mtaalamu wa Mfumo wa
Ulipaji Serikalini kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Ndewingia
Mashauri, akitoa mafunzo kwa wahasibu na wahandisi wa Wakala wa Barabara
za Vijijini na Mijini- TARURA, kutoka maeneo mbalimbali nchini, mafunzo
yaliyofanyika katika ukumbi wa Hazina Ndogo mkoani Morogoro.
Mtendaji Mkuu wa
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini- TARURA, Mhandisi Victor Seff,
akieleza uhitaji wa Mfumo wa ulipaji Serikalini katika Taasisi
anayoiongoza ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa za fedha kwa
urahisi, wakati wa mafunzo ya mfumo huo yaliyofanyika katika ukumbi wa
Hazina Ndogo mkoani Morogoro.
Washiriki wa mafunzo
ya Mfumo wa Ulipaji Serikalini- MUSE, kutoka Wakala wa Barabara za
Vijijini na Mijini- TARURA, wakifuatilia mada zilizotolewa na wataalamu,
katika ukumbi wa Hazina ndogo, mkoani Morogoro.
Mhasibu Mkuu wa Serikali kutoka Wizara ya
Fedha na Mipango, Bw. Francis Mwakapalila (katikati), Mtendaji Mkuu wa
TARURA, Mhandisi Victor Seff (wa pili kushoto), wakiwa katika picha ya
pamoja na baadhi ya viongozi kutoka Wakala wa Barabara za Vijijini na
Mijini- TARURA na Wizara ya Fedha na Mipango, baada ya ufunguzi wa
mafunzo ya Mfumo mpya wa ulipaji Serikalini kwa wahasibu na wahandisi wa
TARURA, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Hazina ndogo mkoani Morogoro.
(Picha na Geofrey Kazaula, TARURA)
…………………….
Na. Geofrey Kazaula, TARURA, Morogoro
Mfumo wa Ulipaji Serikalini (MUSE)
umeanzishwa na wataalamu wa ndani ili kuunganisha mifumo mingine
iliyopo, lengo likiwa ni kupunguza gharama na kurahisisha upatikanaji wa
taarifa za fedha.
Hayo yameelezwa na Mhasibu Mkuu wa
Serikali, Bw. Francis Mwakapalila, ambaye alikuwa mgeni Rasmi katika
ufunguzi wa mafunzo ya Mfumo wa Ulipaji Serikalini- MUSE kwa wahasibu na
wahandisi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini- TARURA mkoani
Morogoro.
Bwana Mwakapalila alisema kuwa mfumo huo
umetengenezwa na wataalam wa ndani kutoka Wizara ya Fedha na Mipango na
utaanza kutumiwa na TARURA kisha kutumiwa na Taasisi zote za Serikali
pamoja na Wizara baada ya kujiridhisha na ufanisi wake.
“Nitoe wito kwa
washiriki wote wa mafunzo haya kuhakikisha wanauelewa vizuri mfumo na
kuwa tayari kuutumia mara tu baada ya mafunzo kukamilika kwa kuwa mfumo
huu ni muhimu kutoka na mabadiliko ya teknolojia katika mifumo ya fedha
duniani”, alisema Bw. Mwakapalila .
Naye Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi
Victor Seff, amewataka wataalam wa Wakala huo wanaoshiriki mafunzo,
kutokuwa na mtazamo hasi kuhusu mfumo na badala yake changamoto watakazo
kutana nazo waziwasilishe mahali husika ili kuweza kutafutiwa ufumbuzi
kwa kuwa mfumo huo ndio suluhisho la matumizi bora ya fedha za Serikali.
Aidha ameeleza kuwa Wizara ya Fedha na
Mipango imetoa wataalam wa kutosha ili kuhakikisha wahasibu wote wa
TARURA wanapatiwa mafunzo na kuuelewa mfumo kwa kina.
Kwaupande wake Mkurugenzi wa Mifumo ya
Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. John Sausi, alieleza kuwa mfumo
huo utaiwezesha Serikali kuangalia malipo yanayofanyika Katika Taasisi,
Kampuni na wadau wengine wanaotoa huduma Serikalini .
Alisema kuwa mfumo huo ulianza baada ya
kukusanya mahitaji kutoka kwa wadau mbalimbali zikiwemo Taasisi Ishirini
za Serikali na kwamba Taasisi ya TARURA itakuwa ya kwanza kutumia mfumo
huo kupitia wahasibu wake na wahandisi watakao kuwa wakiidhinisha
malipo.
Bwana Sausi, alisema mafunzo hayo
yanawahusisha wahasibu na wahandisi wa TARURA nchi nzima kuanzia ngazi
ya Halmashauri lengo likiwa ni kumwezesha Mtendaji Mkuu wa TARURA kuona
malipo yote yanayofanyika na Wakala huo katika sehemu mbalimbali kwa
wakati.
Wizara ya Fedha na Mipango imekuwa
ikitumia Mifumo ya Fedha tangu miaka ya Sitini na kutokana na ukuaji wa
teknolojia imeamua kufanya maboresho ya mifumo hiyo ili kuendana na
mahitaji ya sasa na kurahisisha kupata hesabu sahihi za fedha kwa
wakati.
0 comments:
Post a Comment