Eneo la Gati linaloendelea kujengwa katika Bandari ya Kabwe iliyopo Wilayani Nkasi Mkoani Rukwa.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh.Joachim Wangabo (wa tatu toka kulia) alipotembelea ujenzi wa bandari ya Kabwe, Wilayani Nkasi.
……………
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo
ametoa wito kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuhusu
kuharakisha ukarabati wa meli ya MV Liemba ili kurahisisha usafirishaji
wa mizigo na wananchi wanaoishi katika mwambao wa Ziwa Tanzganyika.
Mh. Wangabo amesema kuwa wananchi hao
wamekuwa wakiweka maisha yao hatarini kwa kutumia vyombo kama mitumbwi
na boti ambavyo usalama wake ni mdogo ukilinganisha na meli kubwa ya MV
Liemba ambayo usalama wake ni wa uhakika.
“Nitoe wito kwa wizara husika hii meli ya
MV Liemba nimeambiwa hapa kwamba ikipita kwenda Zambia inaitwa ‘Our
Baby’ mtoto wetu, sasa huyu mtoto wetu anaulizwa yuko wapi, Zambia
wanauliza, sasa Wizara husika twende haraka isimamie hili jambo, MV
Liemba itengenezwe, watu maisha yao yapo kwenye hatari kubwa ndani ya
hili ziwa Tanganyika”
Mh. Wangabo ameyasema hayo alipotembelea
mradi wa usanifu na ujenzi wa bandari ya Kabwe iliyopo kata ya Kabwe
katika Wilaya ya Nkasi ili kujionea maendeleo ya ujenzi huo ulioanza
tarehe 1 Aprili,2018 ambapo hadi sasa mradi huo umetekelezwa kwa
asilimia 52 katika miezi 14 na unatarajiwa kukamilika tarehe 1 Aprili
2020 na kugharimu Shilingi Bilioni 7.49 ambazo ni fedha za Mamlaka ya
Bandari nchini.
Naye Mbunge wa jimbo la Nkasi Kaskazini
Mh Ali Kessy alieleza kuwa meli hiyo ya MV Liemba ilitakiwa kukamilishwa
ukarabati wake tangu mwaka wa fedha 2017/2018 lakini fedha za ukarabati
hazikutengwa na kudai kuwa Waziri wa Fedha Mh. Filipo Mpango
amemuhakikishia kuwa fedha za ukarabati wa meli hiyo zimetengwa katika
bajeti yam waka 2018/2019.
Kwa upande wake Meneja wa Bandari za Ziwa
Tanganyika Pasivo Ntetema amesema kuwa mradi huo unahusisha ujenzi wa
gati, jengo la kupumzikia abiria, jengo la mgahawa, ofisi, ghala la
kuhifadhia mizigo, nyumba za wafanyakazi na uzio na kuongeza kuwa kwa
Bandari ya Kabwe peke yake wastani wa usafirishaji kwa mwezi ni tani
1500 hadi 2000 na mwaka wa fedha 2018/2019 zimesafirishwa tani 20,000
“Pamoja na changamoto za miundombinu
lakini utaona kuna ‘access’ nzuri ya watu kupita hapa kwahiyo
kukishaboreshwa bandari hii ikakamilika lakini pia miundombinu ya
barabara ya kuingia hapa ikakamilika ni Imani yetu watu wa bandari ya
kwamba kupitia uongozi wako, kupitia mheshimiwa mbunge na mamlaka zote
zinazotawala mkoa wa Rukwa pamoja na serikali kuu, tutaangalia sasa
uwezekano wa kuboresha barabara hii kwa kiwango cha lami ili shehena
kubwa iweze kupita hapa
Mamlaka ya Bandari inatekeleza miradi
mitatu katika Mkoa wa Rukwa ambayo ni Mradi wa uboreshwaji wa bandari ya
Kasanga iliyopo Wilaya ya Kalambo, Ujenzi wa barabara katika Bandari ya
Kipili na Mradi wa Usanifu na Ujenzi wa Gati Bandari ya Kabwe zilizopo
katika Wilaya ya Nkasi ambapo miradi yote itagharimu shilingi bilioni
12.7
0 comments:
Post a Comment