Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana
na Balozi wa Kenya nchini, Mhe. Dany Kazungu, ofisini kwa Waziri Mkuu
Magogoni jijini Dar es salaam, Julai 2, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza
na Balozi wa Kenya nchini, Mhe. Dany Kazungu, ofisini kwa Waziri Mkuu,
Magogoni jijini Dar es salaam, Julai 2, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea
ujumbe maalum wa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kwa naiba ya Rais Dkt.
John Pombe Magufuli, kutoka kwa Balozi wa Kenya nchini, Mhe. Dany
Kazungu, ofisini kwa Waziri Mkuu jijini Dar es salaam Julai 2, 2019.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………………………….
*Ni kuhusu kuchukizwa kwake na kauli ya Jaguar
RAIS wa Kenya, Uhuru Kenyatta amemtumia
ujumbe maalumu Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli unaoelezea msimamo
wa Serikali yake kuhusu kukerwa na matamshi yaliyotolewa hivi karibuni
na Mbunge wa jimbo la Starehe, Charles Njagua Kanyi maarufu kwa jina la
Jaguar.
Ujumbe huo wa maandishi umewasilishwa
leo (Jumanne, Julai 02, 2019) na Balozi wa Kenya nchini, Mhe. Dany
Kazungu na kupokelewa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais
Dkt. Magufuli, ofisini kwa Waziri Mkuu Magogoni jijini Dar Es Salaam.
Akipokea taarifa hiyo Waziri Mkuu amesema
Watanzania wamefurahishwa na hatua mbalimbali zilizochukulia na
Serikali ya Kenya dhidi ya mbunge huyo zinazodhihirisha kwamba matamshi
hayo hayakuwa msimamo wa Serikali ya Kenya wala wananchi wake
bali ulikuwa ni msimamo binafsi wa mbunge huyo.
Amesema siku zote Watanzania na Wakenya
wamekuwa huru kuishi na kufanya kazi au biashara katika nchi za Afrika
ya Mashariki na pale yalipotokea matatizo au kutokukubaliana serikali
husika zilikaa mezani na kumaliza tofauti hizo.
“Uhusiano kati ya Kenya na Tanzania ni wa
karibu mno na wa kidugu kwani kuna baadhi ya makabila yapo katika nchi
mbili hizi kama vile Wamasai na Wakurya na Wajaluo hivyo ushirkiano
katika masuala ya mbalimbali yakiwemo ya kabiashara na ya kijamii
haukwepeki.”
Hivyo, Waziri Mkuu ametoa wito kwa
viongozi na wananchi wa nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki
kujiepusha na kauli zenye viashiria vya kujenga chuki, uhasama na
migongano miongoni mwa wananchi kwani kauli hizo zisipodhibitiwa mapema
zinaweza kusabisha hofu na kutokuelewana miongoni mwao.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi
Watanzania kuendelea kuishi kwa amani na upendo na ndugu zao wa Kenya
na wageni wote kutoka nchi za Afrika ya Mashariki na duniani kwa ujumla
ambao wapo nchini wakifanya shughuli mbalimbali kwa mujibu wa sheria za
nchi.
“Mambo yetu yote katika nchi za Afrika ya
Mashariki hasa ya biashara na ya kiuchumi kwa ujumla yataenda vizuri
endapo tutalinda na kudumisha amani, bila amani tutaogopana na
tutashindwa kabisa kushirikiana”, amesisitiza Mheshimiwa Majaliwa.
Waziri Mkuu ameahidi kuwa Serikali ya
Tanzania kamwe ahaitaruhusu wala kufumbia macho kauli au vitendo
vyovyote vyenye viashiria vya uchochezi dhidi ya nchi jirani ili na
kulinda na kuunga mkono juhudi mbalimbali za ushirikiano wa kisiasa na
kiuchumi zinazofanywa na viongozi wakuu wa Mataifa ya Afrika.
Kwa upande wake Balozi Kazungu
amemshukuru Waziri Mkuu kwa kauli yake aliyoitoa Bungeni jijini Dodoma
iliyowataka Watanzania kuwa watulivu na wayachukulie matamshi ya Mbunge
wa jimbo la Starehe nchini Kenya, Njagua kuwa ni msimamo wake binafsi na
siyo msimamo wa Wakenya na Serikali yao.
Balozi Njagua mesema Msimamo wa Rais
Kenyatta siku zote umekuwa ni kuwapokea na kuwakubali ndugu zao wote
wanaotoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki walioamua kuishi au
kufanya biashara nchini Kenya.
Mwanzoni mwa wiki iliyopita Mbunge wa
jimbo la Starehe nchini Kenya Njagua alitoa matamshi ya kichochezi
akiwataka raia wa kigeni kutoka Mataifa mbalimbali wanaofanya shughuli
za kibiashara nchini Kenya wakiwemo Watanzania waondoke ndani ya muda wa
saa 24.
0 comments:
Post a Comment