Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbwamaji uliopo
Gezaulole Kata ya Somangila Wilayani Kigamboni, Yohana Luhemeja akiwa
kwenye eneo hilo la jengo la kisima.
Mkimbiza Mwenge akimtwisha na kumtua
ndoo ya maji mmoja wa akina mama wa Gezaulole kama ishara ya kuzindua
mradi wa maji Kisima cha Gezaulole. (Picha na Andrew Chale).
…………………
Na Andrew Chale, Kigamboni
WANANCHI wa Mtaa wa Mbwamaji uliopo
Gezaulole Kata ya Somangila Wilayani Kigamboni wamempongeza Mwenyekiti
wa Serikali ya Mtaa huo Yohana Luhemeja kwa juhudi zake za kusimamia
maendeleo ikiwemo suala la upatikanaji wa maji safi na salama.
Wananchi hao wametoa pongeza hizo mapema
jana Julai 23 wakati wa Mwenge wa Uhuru uliotembelea kukagua mradi huo
ambao utasaidia wakazi zaidi ya 8000 Mtaa huo wa Mbwamaji, Somangila.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye
tukio hilo la Mwenge wa uhuru uliotembelea kukagua mradi huo, Wananchi
hao walieleza kuwa maendeleo hayana Chama na kwa hatua na juhudi za
Mwenyekiti alizoahidi awali miaka kadhaa iliyopita zimeweza kutimia.
“Awali mradi huu ulikufa na hakukuwa na
mtu mwenye kutaka kuonesha nia ya kuufufua, tunashukuru Mwenyekiti wa
Serikali wetu licha ya kutoka upinzani alipoingia kushika nafasi hii
alianza na suala la hiki kisima na kwa kushirikiana na kamati yake
waliweza kuonesha juhudi na hatua zimechukuliwa na sasa kisima
kimefufuliwa. Hizi ni juhudi kubwa tunawapongeza wote ikiwemo Dawasa na
viongozi wa Halmashauri kwa pamoja kwa kumuunga mkono” alieleza Sagala
Msumi mkazi wa Mbwamaji.
Nao baadhi ya Wanawake wa Mtaa huo
akiwemo Ester Modest na Falhaty Mussa wameshukuru kwa hatua hiyo kwani
kwa sasa kero ya maji itakuwa ni historia kwao ambapo walikuwa
wakikumbwana na changamoto ya maji safi na salama ya matumizi ya
nyumbani.
“Tumekuwa tukitumia maji ya visima
ambavyo baadhi yake sio salama hivyo kukamilika kwa kisima hiki
kitatusaidia sana tunamshukuru sana Mwenyekiti wetu na Kamati yake kwa
ujumla”alieleza Bi. Ester Modest.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa huo
Yohana Luhemeja ameeleza kuwa, mradi huo wa kisima hicho utaenda
kusaidia Wananchi kwenye zaidi ya Kaya 8000 na kwa sasa tayari mabomba
yanaendelea kutandikwa ardhini na mwezi Desemba mwaka huu maji yataanza
rasmi.
“Kisima hiki ni cha muda mrefu na kwa
sasa kimefufuliwa na kipo tayari kwa kuanza kazi kwani wananchi wameanza
kusambaziwa mabomba pia mitaa mitatu itaenda kunufaika na maji haya
kuanzia Mwezi Desemba mwaka huu” alisema Mwenyekiti huyo.
Yohana Luhemeja aliongeza kuwa: mradi huo
wa kisima hicho awali ulikuwa wa Kijiji cha Gezaulole lakini ukafa na
kubaki bustani pekee hata hivyo katika moja ya ahadi zake wakati wa
kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo ya Uenyekiti wa Serikali ya Mtaa
aliahidi kufufua kisima hicho na kwa sasa ahadi imetimia huku
akiwapongeza DAWASA
na Halmashauri ya Kigamboni kwa kuweza
kumuunga mkono kwenye suala hilo la kukifufua na kwa sasa wananchi wa
Gezaulole watapata maji ya uhakika.” Alimalizia Mwenyekiti huyo, Yohana
Luhemeja.
Aidha, Mwenge huo wa Uhuru katika Wilaya
hiyo ya Kigamboni umeweza kutembelea na kukagua miradi 5 yenye thamani
ya Bilioni 14, ikiwemo kisima hicho cha Maji Gezaulole.
0 comments:
Post a Comment