METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, July 1, 2019

MBUNGE KOLIMBA AHAMASISHA WANAWAKE KUUNDA VIKUNDI VYA KITARAFA MKOANI NJOMBE





Na Maiko Luoga Ludewa

Mbunge wa Viti maalumu kupitia chama cha mapinduzi CCM mkoa wa Njombe, Dkt, Susan Kolimba amesimamia zoezi la kuunda Vikundi vitano vya Wanawake wa chama hicho kutoka Tarafa tano za Wilaya ya Ludewa kwa lengo la kuimarisha uchumi.

Zoezi la Kuunda vikundi hivyo kutoka Tarafa tano za Liganga, Mawengi, Mlangali, Mwambao na Masasi limefanyika katika ukumbi wa CCM wilaya ya Ludewa, wakati kikao cha Baraza la Wanawake wa chama cha mapinduzi UWT wilayani humo likiendelea na Mgeni Rasmi alikuwa Dkt, Susan Kolimba Mbunge wa Viti maalumu mkoa wa Njombe.

Akizungumza katika Kikao cha Baraza la kawaida la UWT wilaya ya Ludewa kilichofanyika June 29/2019, Mgeni Rasmi Dkt, Susan Kolimba aliwapongeza Viongozi wa UWT wilayani Ludewa kwa kufanyakazi kwa bidii huku akiwashauri kuendelea kuonesha umoja na mshikamano na jamii ili kujenga umoja, na upendo

Aidha Mbunge huyo ametoa Fedha kiasi cha  Tsh, 2,500,000/= kwaajili ya kuviunga mkono Vikundi hivyo ambavyo kila kimoja kimepata Kiasi cha Tsh, 500,000/= huku akitoa Wito kuwa, fedha hiyo itumike katika kuibua miradi ambayo itawasaidia kujiletea maendeleo ya kweli na kuongeza chachu ya maendeleo ya kiuchumi.

“Mmesema kuwa hamna vyanzo vya Mapato kwaajili ya kujiimarisha kiuchumi, mimi nadhani leo hii mnatakiwa kuunda Vikundi kila Tarafa kikundi kimoja ili muweze kufanya shughuli zenu za uzalishaji mali, mimi leo nawakabidhi kiasi cha Tsh, 500,000/= kwa kila kikundi” Amesema Dkt, Susan Kolimba Mbunge wa Viti maalumu CCM mkoa wa Njombe.

Dkt, Susan Kolimba kupitia kikao hicho ameahidi kuendelea kusaidia Vikundi mbalimbali vya Wanawake vilivyopo katika Tarafa zote za Mkoa wa Njombe, sambamba na kuwataka Wanawake hao kuonesha Umoja na mshikamano katika kutekeleza majukumu yao ili kukuza vipato vyao.

Kikao hicho cha Baraza la UWT wilaya ya Ludewa kilifunguliwa na Mwenyekiti wake Bi, Leah Mbilinyi na kuhudhuriwa na Mbunge mwingine wa Viti Maalumu mkoa wa Njombe kupitia CCM Mh, Neema Mgaya pamoja na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ludewa Ndg, Stanley Kolimba.

Viongozi wengine Walioshiriki Kikao hicho ni pamoja na Katibu wa CCM wilaya ya Ludewa Ndg, Bakari Mfaume, Katibu wa UWT wilayani humo Bi, Flora Kapalia, Katibu wa UV,CCM wilaya Ndg, Hassani Kapolo pamoja na Wajumbe wa UWT kutoka Kata zote 26 za Wilaya ya Ludewa.

Baadhi ya Wajumbe walioshiriki Kikao hicho wamempongeza na Kumshukuru Dkt, Susan Kolimba kwa mchango wake wa mawazo, fedha na vifaa mbali mbali katika sekta ya afya, elimu na uchumi anavyoendelea kutoa kwa wanawake na wananchi wote katika Mkoa wa Njombe ili kuwasaidia waweze kuboresha huduma za kijamii, na vipato vyao.
Share:

Related Posts:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2025 WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com