
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akikagua darasa wakati alipotembelea Shule ya Sekondari ya Liuguru
wilayani Ruangwa Julai 29, 2019. Wa pili kushoto ni Mkurugenzi wa
Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Andrew Chezue. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akisalimiana na viongozi wakati alipowasili kwenye Shule ya Sekondari ya
Liuguru wilayani Ruangwa kukagua majengo ya Shule hiyo na kuzungumza na
wananchi, Julai 29, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza na wananchi kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari ya Liuguru
wilayani Ruangwa, Julai 29, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akitembelea jengo la wazazi wakati alipokagua ujenzi wa hospitali ya
wilaya ya Ruangwa, Julai 29, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akikagua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Ruangwa kwenye eneo la
Nachingwea , Julai 29, 2019. Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Ruangwa,
Hashim Mgandilwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akisalimiana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Andrew
Chezue, wakati alipowasili kwenye eneo la Nachingwea kukagua ujenzi wa
Hospitali ya wilaya ya Ruangwa, Julai 29, 2019. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
****************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa na ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo.
Waziri Mkuu ambaye ni mbunge
wa jimbo la Ruangwa na yuko jimboni kwake kwa mapumziko mafupi, alikagua
ujenzi huo jana jioni (Jumatatu, Julai 29, 2019). Jengo hilo
linalojengwa na SUMA JKT, linahitaji sh. bilioni 3.77 hadi kukamilika
kwake.
Akiwa kwenye eneo la ofisi
hizo, Waziri Mkuu alielezwa kwamba Halmashauri hiyo imepokea shilingi
milioni 500 kutoka Serikali Kuu kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili
ya ujenzi wa ofisi mpya ya Halmashauri hiyo.
Ujenzi wa ofisi hiyo ambayo
ikikamilika itakuwa na ghorofa moja, ulianza Juni mosi, 2019 na
unatarajiwa kukamilika Julai, mwakani. Jengo litakuwa na ofisi 33 za
chini, ofisi 26 za ghorofa ya kwanza na kumbi mbili za mikutano.
Kazi ambazo zimeshafanyika
hadi sasa ni usafishaji wa eneo kwa ajili ya ujenzi; upimaji wa sampuli
ya udongo (Geotech Survey); uingizaji wa maji eneo la ujenzi; uchimbaji
wa kisima kikubwa cha kuhifadhia maji na uvutaji wa umeme eneo la
ujenzi.
Kazi zinazoendelea kwa sasa ni
ufyatuaji wa tofali ambapo hadi sasa jumla ya matofali 10,000
yamekwishafyatuliwa ambayo ni sawa na asilimia 50 ya mahitaji ya
matofali yote. Pia ukusanyaji wa vifaa vya ujenzi eneo la ujenzi
unaendelea.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu
jana alikagua ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo na kukiri kwamba
ameridhishwa na kazi iliyokwishafanyika hadi sasa.
Akiwa hospitalini hapo, Waziri
Mkuu alielezwa na Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dkt. Mahela Njile kwamba
hadi kukamilika kwake, hospitali hiyo itakuwa na majengo 22 yanayokisiwa
kugharimu jumla ya sh. bilioni 7.5 kulingana na maksio ya OR-TAMISEMI.
Dkt. Njile alisema katika
awamu ya kwanza Serikali imetoa sh. bilioni 1.5 na kuelekeza yajengwe
majengo saba ya kipaumbele ambayo ni jengo la uzazi, la wagonjwa wa nje
(OPD), maabara, la X-ray, la utoaji dawa, la kufulia nguo na la
utawala.
“Serikali imeelekeza ujenzi huu ufanyike kwa kutumia njia ya manunuzi inayoitwa ‘Force Account’
ambapo Halmashauri inanunua vifaa vya ujenzi na kuajiri mafundi wa
kujenga majengo yaliyoelekezwa wakisimamiwa na wataalam wa halmashauri
na kamati mbalimbali,” alisema.
Akizungumza na wakazi
waliojitokeza kumsikiliza hospitalini hapo, Waziri Mkuu aliwapongeza
viongozi wa Halmashauri hiyo kwa kusimamia vizuri ujenzi na kwa kuamua
kutumia force account ambayo alisema inapunguza sana gharama za manunuzi.
Aliitaka Halmashauri hiyo
isisubiri hadi kazi ya ujenzi ikamilike, na badala yake wahusika
wajipange na kuanza kufanya usafi wa eneo linalozunguka hospitali hiyo.
“Halmashauri tusikae tu kusubiri ujenzi uishe. Tufanye usafi kuzunguka
eneo lote, tupande miti na maua ili mandhari ianze kupendeza,” alisema.
Kuhusu muda wa kukamilisha
kazi hiyo, Waziri Mkuu aliwashauri mafundi wazidishiwe muda wa kufanya
kazi. “Badala ya kufanya kazi mchana peke yake, bora waongezewe muda
wafanye hadi usiku ili kufidia muda uliopotea, na uliobakia ni mfupi
mno,” alisema.
Alisema anaamini kazi hiyo
itakamilika ndani ya muda mfupi ili huduma zianze kutolewa hapohapo
Ruangwa na kuwapunguzia wananchi adha ya kwenda hadi hospitali ya
Ndanda.
0 comments:
Post a Comment