Halmashauri kuu ya chama cha mapinduzi
CCM mkoa wa Njombe iliyokutana Julai mosi 2019 katika ukumbi wa TURBO
Njombe mjini, ilitoka na maazimio mbalimbali pamoja na kuipongeza
Serikali mkoani humo kwa Utekelezaji wa ilani ya uchaguzi katika Miradi
ya Afya, Barabara na Elimu.
Hayo yamesemwa na Katibu wa Siasa na
Uenezi wa chama cha mapinduzi CCM mkoa wa Njombe Ndg, Erasto Ngole,
wakati akizungumza na Waandishi wa Habari Ofisini kwake na kuongeza
kuwa, kikao hicho kimeielekeza Serikali mkoani humo kuhakikisha Kasi ya
Ujenzi wa Barabara ya Lami kutoka Njombe kwenda Ludewa inaongezeka.
Amesema chama kimeielekeza Serikali
kuhakikisha Ujenzi wa Barabara ya kutoka Njombe kupitia Lupembe hadi
Madeke unaanza maramoja, ili kuwapunguzia Wananchi wa maeneo hayo tatizo
la usafiri hasa kipindi cha Masika.
Ameongoza kuwa Kikao kimeelekeza Mkuu wa
mkoa na Mkuu wa Wilaya ya Njombe, wakutane na Wadau mbalimbali ili
kujadili namna bora ya uendeshaji wa Kituo kipya cha Mabasi kilichopo
eneo la Mjimwema Njombe mjini, kwa lengo la kujadili na kuondoa kero
zilizopo katika kituo hicho.
Kuhusu Vitambulisho vya Wajasiriamali
Ngole amesema kuwa Kikao kilimpongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt, John Pombe Magufuli, kwa ubunifu wa kuwasaidia
Wajasiriamali kote nchini ili wasikutane na usumbufu katika Biashara
zao.
Katibu huyo wa Siasa na Uenezi wa CCM
Mkoa wa Njombe ameeleza kuwa Kikao kimebaini kuwa, baadhi ya Wadau
mkoani Njombe hawana ufahamu wa kutosha juu ya Vitambulisho hivyo na
Kikao kimeielekeza Serikali kutoa waraka utakao ainisha kundi
linalostahili kupata vitambulisho hivyo.
“Tukiwa na waraka utasaidia Watendaji wa
Serikali kuwa na uelewa wa pamoja juu ya utekelezaji wa swala hili, ili
lengo la Taifa lisipotoshwe na watu wachache, pia kikao kimekubaliana
kuwa wana siasa wote wanatakiwa kushirikiana na Serikali katika
kutekeleza hoja hii muhimu” Ameeleza Erasto Ngole.
Aidha kuhusu Taarifa ya Viongozi na
Wanachama kutoka vyama vingine vya siasa wanaohamia chama cha mapinduzi
mkoa wa Njombe, Ndg, Erasto Ngole amesema kuwa Hadi sasa chama
kimewapokea Viongozi na Wanachama 237 kutoka vyama vya upinzani kuanzia
ngazi ya Vijiji hadi mkoa.
“CCM inaamini kuwa ifikapo October 2019
wale wote waliokuwa wanaipinga CCM, watakuwa wanajiunga na chama hiki
kutokana na uelekeo sahihi wa chama na Serikali wa utekelezaji wa Ilani
ya uchaguzi na kutatua kero za Watu” Erasto Ngole.
Akiendelea kutoa Taarifa kwa vyombo vya
Habari Ngole amesema, Kikao cha Halmashauri kuu ya CCM mkoa kilipongeza
maendeleo ya zoezi la kusajili Wanachama kupitia mfumo mpya wa
Kielectronic linaloendelea katika wilaya zote za mkoa wa Njombe.
Kufuatia Changamoto ya huduma ya Maji
katika baadhi ya maeneo ya Miji ya Njombe, Makambako na Ilembula, kikao
chini ya Mwenyekiti Mzee Jassel Mwamwala, kiliitaka Serikali kuharakisha
ukamilishaji wa Miradi katika maeneo hayo pamoja na huduma ya Umeme wa
REA katika Wilaya ya Wanging’ombe.
Katika hatua nyingine Katibu wa siasa na
uenezi wa CCM mkoa wa Njombe amesema kuwa chama kinaitambua na
kuithamini Sekta ya michezo, hivyo kikao kimeielekeza Serikali mkoani
Njombe kuiboresha Sekta hiyo kwakuwa mkoa bado upo nyuma katika suala
zima la michezo.
*Imetolewa na Ofisi ya Siasa na Uenezi CCM, mkoa wa Njombe.*
0 comments:
Post a Comment