Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt.
Hamisi Kigwangalla akizungumza na wananchi wa Kata ya Alaitole ndani ya
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro alipofika kutatua mgogoro wa wananchi
wa Kata hiyo kuzuiwa kujenga shule ya Wasichana ya bweni na Mamlaka ya
Hifadhi ya Ngorongoro katika eneo la Esere, wilayani Ngorongoro. Hata
hivyo Waziri Kigwangalla ameumaliza mgogoro huo kwa kuagiza wakazi hao
wapewe kibali cha ujenzi na mamlaka hiyo katika eneo lililopendekezwa.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt.
Hamisi Kigwangalla (kushoto) akisikiliza maoni na hoja za wananchi wa
Kata ya Alaitole alipofika kutatua mgogoro wa wananchi wa Kata hiyo
kuzuiwa kujenga shule ya Wasichana ya bweni na Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro katika eneo lao la Esere, wilayani Ngorongoro jijini Arusha.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia na Mbunge wa jimbo la Ngorongoro Mhe.William Ole Nasha
akizungumza na wakazi wa Kata ya Alaitole iliyo ndani ya Eneo la Mamlaka
ya Hifadhi ya Ngorongoro ambayo ilizuiwa kujenga shule ya bweni ya
wasichana na mamlaka hiyo zuio ambalo limeondolewa na Waziri wa
Maliasili na Utalii aliyefika katika kata hiyo kutatua mgogoro huo
Mkutano wa Waziri wa Maliasili na
Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla na wananchi wa Kata ya Alaitole katika
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Mhe. Kigwangalla alifika kutatua
mgogoro uliohusisha wananchi wa Kata hiyo kuzuiwa kujenga shule ya
Wasichana ya bweni na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt.
Hamisi Kigwangalla akizungumza na wananchi wa Kata ya Alaitole ndani ya
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro mara baada ya kupitishwa na katika
eneo lilipoonekana fuvu linalosadikiwa kuwa ni la binadamu wa kale
ambalo bado taarifa zake zinaendelea kufanyiwa utafiti katika eneo la
Esere, wilayani Ngorongoro
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt.
Hamisi Kigwangalla akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi
na Teknolojia ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Ngorongoro Mhe.William
Ole Nasha na askari wa uhifadhi wakiangalia eneo itakapojengwa shule ya
wasichana ya bweni ya kata ya Alaitole.
Waziri wa Maliasili na Utalii
Dkt. Hamisi Kigwangalla, viongozi na wananchi wa Kata Alaitole
wakitazama eneo lilipoonekana fuvu linalosadikiwa kuwa ni la binadamu wa
kale lililogunduliwa na wakazi hao katika eneo la Esere, wilayani
Ngorongoro. Taarifa kuhusu fuvu hilo zinaendelea kufanyiwa utafiti na
watalaam.
********************************
WMU – Ngorongoro, ARUSHA.
11/6/2019.
Waziri wa Maliasili na Utalii,
Dkt. Hamisi Kigwangalla, ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro uwaruhusu wananchi wa Kata ya Alaitole wajenge shule ya
wasichana ya bweni katika eneo la Esere lililo ndani ya Mamlaka hiyo
wilayani Ngorongoro, ili waweze kupata elimu kufuatia wananchi hao
kuzuiwa kwa muda mrefu kutekeleza ujenzi huo.
Aidha, ameutaka uongozi wa Mamlaka
hiyo utoe kibali cha kuwawezesha wananchi kata hiyo kuanza ujenzi
haraka iwezekanavyo ili fedha zilizotolewa na Serikali shilingi milioni
298 zianze kutumika.
Dkt. Kigwangalla ametoa maagizo
hayo alipokuwa akizungumza na kusikiliza kero za wananchi wa Kata
Alaitole wilayani Ngorongoro kwenye mkutano wa hadhara uliowashirikisha
viongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, viongozi serikali wa kata
hiyo, viongozi wa mila wa kabila la Masai na madiwani na Mbunge wa jimbo
la Ngorongoro Mhe. William Ole Nasha.
” Jambo hili ninalifunga rasmi,
shule itajengwa pale eneo lisizidi ekari 15 ili shule hii ijengwe karibu
na shule yenu ya msingi ili watotowapate fursa ya kusoma,changamoto za
hapa ikiwemo ya ongezeko la watu, uharibifu wa mazingira na mahusiano
kudorora tunazifahamu na tunazifanyia kazi” Amesisitiza Dkt.
Kigwangalla.
Amesema Serikali inaunga mkono
juhudi zote za wananchi za kujiletea maendeleo akifafanua kwamba hatua
ya wananchi hao kuamua kujenga shule ya Sekondari ya Bweni ni jambo
linalopaswa kupongezwa na kila mpenda maendeleo.
“Mnacho kitaka kiko wazi, mnataka
maendeleo ya watoto wenu, katika hili mmesema kila baba anatoa elfu
hamsini na wanawake wanatoa elfu ishirini, hili ni jambo kubwa achilia
mbali nguvu kazi mnayojitolea na tayari serikali imeshaleta milioni 298,
haiingii akilini eneo linalochangia kuleta na kuingiza mapato mengi
Serikalini kiasi cha bilioni 126 likose shule” Amesisitiza Dkt.
Kigwangalla.
Dkt. Kigwangalla ameeleza kuwa
ujenzi shule hiyo utawaondolea wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu
akibainisha kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono wananchi hao kwenye
mipango yao ya utekelezaji miradi ya maendeleo.
Amesema jamii hiyo pamoja na
mazingira wanayoishi kuwa ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro wanahitaji
elimu. Aidha, amesema pia ni muhimu katika sekta ya utalii kupitia
utamaduni wao akiongeza kuwa kazi ya Wizara ni kuona mafanikio ya sekta
ya utalii yanakuwa kwa kuongeza mapato na sio migogoro.
Dkt. Kigwangalla amesema Hifadhi
ya Ngorongoro ni hifadhi mseto inayoruhusu binadamu na wanyama kuwepo
katika eneo moja na kwamba hiyo ipo kwa mujibu wa sheria akiitaka
Mamlaka hiyo kuyatazama vizuri majukumu yake ya kuendeleza Utalii,
Kulinda rasilimali zililizopo kwa maana ya kuhifadhi na kuhudumia jamii
iliyo ndani ya hifadhi hiyo.
Katika hatua nyingine ameutaka
uongozi wa Mamlaka hiyo uendelee kufanya mazungumzo na wananchi hao
badala ya kujielekeza katika matumizi ya nguvu ili kupata uelewa wa
pamoja akitolea mfano wa eneo la Loliondo ambalo hivi sasa lina utulivu.
“ Viongozi wa Mamlaka mnalo jukumu
la kuwasikiliza wananchi na kuamua kwa pamoja, eneo la Ngorongoro lina
thamani ya kipekee ni Urithi wa dunia lakini pamoja na uthamani wake
kitaifa na Kimataifa haiondoi uthamani wa wananchi wetu wanaoishi hapa
katika eneo hili, hapa ni kwao walipozaliwa wamezika babu, baba zao na
watoto wao ni lazima tujifunze kuheshimu na kuthamini maslahi ya walio
walio wengi” Amesisitiza Dkt. Kigwangalla.
Kuhusu mahusiano baina ya wananchi
na wahifdhi Dkt. Kigwangalla amesema kuwa kupitia mkutano wake na
wananchi amebaini kuwepo kwa tatizo la mawasiliano na mahusiano baina ya
wananchi wa eneo hilo na watumishi wa Serikali walio chini ya Mamlaka
ya Hifadhi ya Ngorongoro akibainisha kwamba tayari serikali imeliona
jambo hilo na inaendelea kulifanyia kazi.
Amewataka wakazi wa eneo hilo
waheshimu sheria zinazosimamia uhifadhi katika eneo la Mamlaka hiyo ili
kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza akifafanua kwamba yapo maeneo
ambayo wakazi hao hawaruhusiwi kufanya shughuli za kibinadamu
yaliyohifadhiwa kwa ajili ya shughuli za utalii
Naye Naibu Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Ngorongoro Mhe.
William Ole Nasha akizungumza wakati wa mkutano huo amempongeza na
kumshukuru Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla kwa
kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha ulinzi wa rasilimali za Taifa
katika maeneo mbalimbali nchini.
Amemwomba aeendelee kutembelea
maeneo mengine ya jimbo hilo kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi wa
kata za wilaya hiyo kwa lengo la kudumisha mahusiano mema.
Mhe. Ole Nasha ameeleza kuwa hatua
ya Wizara kutafutia ufumbuzi mgogoro huo wa ujenzi wa shule ya
wasichana ya bweni, vile vile uamuzi wa serikali kutoa eneo na fedha
kiasi cha shilingi milioni 298 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo katika
eneo lililokubaliwa ni ishara tosha kwamba Serikali inawalinda na
kuwajali wananchi wake.
Amesema wananchi wa jimbo la
Ngorongoro pamoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili wako ni
wasikivu na wako tayari muda wote kushirikiana na Serikali ikiwemo
ulinzi wa rasilimali zilizopo na kuendeleza uhifadhi katika hifadhi ya
Ngorongoro.
Kwa upande wao wananchi wa Kata ya
Alaitole wakizungumza kwa nyakati tofauti wamemshukuru Dkt. Kigwangalla
kwa kuamua kuwafuata na kuzungumza nao katika makazi yao wakimpongeza
kwa juhudi zake za kutatua changamoto mbalimbali kwa maslahi ya wananchi
na uhifadhi.
Aidha, wamemwomba kuendelea
kuisimamia sekta ya uhifadhi nchi wakitoa wito wa kudumisha mahusiano
mema baina ya wananchi na wahifadhi.
0 comments:
Post a Comment