Meneja wa Wakala wa Vipimo Shinyanga Bw.
Elias Nyanda akihakiki mizani inayotumika katika ununuzi wa pamba kwenye
chama cha msingi cha ushirika (AMCOS)
Afisa Vipimo Shinyanga akitoa elimu ya matumizi sahihi ya mizani kwa Wakulima wa Pamba
Meneja wa Survaillance Bw. Moses Ntungi
akiwaelekeza wakulima wa Pamba namna ya kuhakiki seal zilizofungwa
katika mizani kabla ya kupima pamba zao.
Meneja wa Wakala wa Vipimo Shinyanga Bw. Elias Nyanda akitoa elimu kwa Wakulima wa Pamba
Meneja wa Wakala wa Vipimo Shinyanga Bw. Elias Nyanda akitoa elimu kwa Wakulima wa Pamba
………………………..
Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Shinyanga
inaendelea na zoezi la utoaji elimu kwa Wakulima wa pamba katika wilaya
ya Kahama kwa lengo la kuwawezesha wakulima wawe na elimu ya utambuzi wa
mizani sahihi zilizo hakikiwa na Wakala wa vipimo na kuwekewa stika
pamoja na lakiri (seal) inayofungwa katika njia za kuingilia kwenye
mizani ili kuzuia isichezewe na wafanyabiashara wasiyo waaminifu kwa
lengo la kujiongezea faida zaidi.
Wakala wa Vipimo Mkoa wa Shinyanga kabla
ya kuanza kwa msimu wa ununuzi wa pamba ilifanya uhakiki wa mizani zote
zitakazotumika katika vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) 195 zilizopo
katika Halmashauri za Ushetu, Kahama Mji, Msalala, Kishapu, Shinyanga
DC pamoja na Manispaa ili kuhakikisha Wakulima wanauza pamba kwa kutumia
vipimo vilivyo sahihi.
Akizungumza na mwandishi wetu Meneja wa
WMA Shinyanga Bw. Elias Nyanda amesema, mpaka sasa jumla ya kata 20
katika wilaya kahama zimepatiwa elimu ya matumizi sahihi ya vipimo na
ukaguzi wa mizani umeendelea kufanyika katika vituo vinavyotumiwa kuuzia
pamba ili kujiridhishsa kama mizani hizo zinafanya kazi kwa usahihi ili
kumsaidia mkulima aweze kupata fedha kulingana na thamani ya pamba
anayouza.
Bw. Nyanda amesema katika zoezi hilo la
elimu wakulima wameelimishwa wawe makini pindi wanapoenda kuuza pamba
kwa kuhakikisha mizani inasoma sufuri (0) kabla ya kuanza upimaji kwa
kutumia mizani ya digitali. Mara baada ya kupima furushi la pamba mizani
inatakiwa kurudi katika sufuri, na wahakikishe mizani haisomi hasi (-)
baada ya kutoa mzigo na ikitokea imesoma hasi mwambie karani
anayesimamia mizani aweze kuizima na kuiwasha tena mizani hiyo kisha
zoezi la upimaji liendelee.
Akizungumza na mwandishi wetu Mkulima wa
pamba Bw. Joseph Nyamwanga ameipongeza sana Wakala wa Vipimo kwa elimu
wanayowapatia kwani imewasaidia sana hasa katika kupunguza pointi
zinazojitokeza wakati wa upimaji na kubakisha namba kamili. Amesema
wataendelea kuwa makini na kuitumia elimu hiyo ili waweze kupata haki
wanayostahili kila wanapoenda kuuza pamba katika AMCOS.
Meneja Nyanda pia ameeleza kuwa kwa sasa
sheria ya Vipimo Sura Na. 340 na mapitio yake ya mwaka 2002 imeboreshwa
na imekuwa kali na endapo mnunuzi wa pamba atajihusisha na uchezeshaji
wa vipimo akakamatwa na kukuri kosa lake na kufifirishwa atatozwa faini
kuanzia shilingi laki moja (100,000/=) mpaka milioni ishirini
(20,000,000/=) kulingana na idadi ya makosa aliyotenda. Na endapo
mtuhumiwa atakataa na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kwanza atatozwa
faini isiyopungua Shillingi 300,000/= na isiyozidi millioni 50 au
kifungo kisichozidi miaka miwili (2) au vyote kwa pamoja, mujibu wa
Sheria ya Vipimo sura na. 340 na mapitio yake ya mwaka 2002.
Vilevile, endapo mtuhumiwa atakamatwa na
kosa kwa mara ya pili na kuendelea na akipelekwa Mahakamani akakutwa na
hatia adhabu ni faini isiyopungua Shillingi 500,000/= na isiyozidi
millioni 100 au kifungo kisichozidi miaka mitano (5) au vyote kwa
pamoja.
Vilevile, amewataka wananchi waweze kutoa
taarifa katika ofisi za wakala wa vipimo wanapokutana na changamoto
mbalimbali za upimaji na pia wanaweza kutumia namba ya bure kutoa
taarifa ambayo ni 0800 11 00 97.
0 comments:
Post a Comment