METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, June 4, 2019

WACHEZAJI 38 WA TIMU YA TAIFA STARS WAFANYIWA UCHUNGUZI WA MOYO

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akizungumza na Daktari wa timu ya Taifa Stars Emily Urasa wakati wa kuwafanyia uchunguzi wa kina wa magonjwa ya moyo wachezaji wa timu hiyo leo Jijini Dar es Salaam. Wachezaji hao walifanyiwa  vipimo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi  (Echocardiograph) na mfumo wa umeme wa moyo unavyofanya kazi (Electrocardiography –ECG).

Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Siza Ngomero akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiogram) mchezaji wa timu ya Taifa Stars Feisal Salum wakati wa uchunguzi wa kina wa magonjwa ya moyo kwa wachezaji wa timu hiyo leo Jijini Dar es Salaam.

Fundi Sanifu wa Moyo na Mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Abuu Dalidali akimpima kipimo cha kuangalia mfumo wa  umeme wa moyo (Electricalcardiography –ECG) mchezaji wa timu ya Taifa Stars Yahaya Zaid wakati wa kuwafanyia uchunguzi wa kina wa magonjwa ya moyo wachezaji wa timu hiyo leo Jijini Dar es Salaam. Wachezaji hao wamefanyiwa uchunguzi wa kina wa magonjwa ya moyo kabla ya kwenda nchini Misri kushiriki mashindano ya AFCON yatakayoanza tarehe  21/06/2019.

Picha na: Genofeva Matemu – JKCI

………………….

Wachezaji 38 wa timu ya Taifa Stars wamefanyiwa uchuguzi wa kina wa magonjwa ya moyo kama Shirikisho la Mpira wa Miguu Africa (CAF) linavyoelekeza kabla ya kuanza kwa mashindano ya kombe la Mataifa ya Africa (AFCON) ni lazima  wachezaji wanaoshiriki mashindano hayo wapimwe afya zao.

Vipimo walivyofanyiwa wachezaji hao ni vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi  (Echocardiograph) na mfumo wa umeme wa moyo unavyofanya kazi (Electrocardiography –ECG). Upimaji huu umefanywa na madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo  wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Taasisi yetu ni Hospitali iliyothibitishwa na CAF  kuwa inakidhi vigezo vyote vya upimaji wa magonjwa ya moyo. Uthibitisho huu ulitolewa kabla ya kuanza kwa mashindano ya AFCON kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 yaliyofanyika mapema mwaka huu hapa nchini .JKCI ilikaguliwa na kuthibitishwa na wakaguzi kutoka CAF.

Matokeo ya vipimo hivyo yatasaidia kufahamu  afya za wachezaji na utimamu wao wa kimwili  kabla ya kwenda kushiriki katika  mashindano ya AFCON yanayotarajia kuanza tarehe 21/06/2019  huko nchini Misri.

Tunatoa wito kwa vilabu vya mpira hapa nchini kuwaleta wachezaji wao kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo hii itawasaidia wachezaji hao kufahamu kama wanamatatizo au la na kuepukana na vifo vya ghafla vinavyoweza kuwapata wakiwa uwanjani. Kwa  upande wa wananchi  kabla ya kujiunga na vilabu vya mazoezi ni muhimu  wakapima afya zao yakiwemo magonjwa ya moyo..

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com