Na Mwandishi Wetu.
NAHODHA wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Ally
Samatta leo ametembelea hospitali ya Mwananyamala, Manispaa ya Kinondoni
mjini Dar es Salaam na kutoa misaada ya vitu vidogo vidogo kwa akina
mama ambao waliojifungua kabla ya wakati.
Samatta anayechezea KRC Genk ya Ubeligiji amefanya zoezi hilo kwa
kushirikiana na Doris Mollel Foundation na miongoni mwa vitu alivyotoa
ni sabuni aina ya Omo.
“Nilifurahi kuona akina mama wakiwa wenye nyuso za furaha baada ya
kuniona na wengi kufurahishwa na kitendo cha mimi kupita hospitalini
hapa. Lakini pia nimebahatika kupanda miti ndani ya hospitali hii,”
amesema Samatta.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba SC
amefanya hayo siku moja tu kabla ya mechi yake ya Hisani kesho katika
tamasha la Nifuate, maalum kuchangia miundombinu ya shuke za Msingi Dar
es Salaam.
Samatta ameunda kikosi cha yeye rafiki zake ambao watamenyana na kikosi
cha mwanamuziki nyota nchini, Ally Kiba na Rafiki zake kesho jioni
Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
Hii itakuwa mara ya pili kwa Samatta kuungana na Kiba ambaye msimu huu
ameichezea Coastal Union katika Ligi Kuu kufanya tamasha hilo baada ya
mwaka jana – na fedha zilizopatikana zilikwenda kununulia madawati ya
shule za Msingi.
Samatta amerejea nchini wiki iliyopita akitoka kuipa Genk ubingwa wa
Ligi Kuu ya Ubelgiji huku naye akishinda tuzo yake Mwanasoka Bora
Mwafrika anayecheza Jupiler Pro League baada ya kumaliza na mabao 23
msimu huu.
Kwa ujumla, Samatta mwenye umri wa miaka 26, ameifungia Genk mabao 62
katika mechi 156 za mashindano yote tangu amejiunga nayo Januari mwaka
2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Katika ligi ya Ubelgiji pekee amefunga mabao 47 katika mechi 123, kwenye
Kombe la Ubelgiji amefunga mabao mawili katika mechi tisa na Europa
League amefunga mabao 14 katika mechi 24.
0 comments:
Post a Comment