METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, June 12, 2019

NDAYIRAGIJJE ASAINI MKATABA WA MIAKA 2 KUINOA AZAM FC


Na Mwandishi Wetu UONGOZI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, leo umeingia mkataba wa miaka miwili na Kocha Mrundi, Etienne Ndayiragijje, kwa ajili ya kuinoa timu hiyo kuanzia msimu ujao. Ndayiragijje, anachukua nafasi ya makocha wa wazawa, Abdul Mingange na Idd Nassor Cheche, waliokuwa makocha wa muda wa timu hiyo hadi msimu uliopita wa ligi ulipomalizika. Zoezi la kocha huyo kuingia mkataba limefanyika Ofisi za Mzizima, mbele ya waandishi wa habari, Azam FC ikiwakilishwa na Ofisa Mtendaji Mkuu, Abdulkarim Amin 'Popat', Mratibu Phillip Alando. Mara baada ya kusaini mkataba huo, Ndayiragijje alikwenda makao makuu ya timu hiyo, Azam Complex na kutembezwa maeneo mbalimbali akiwa sambamba na Ofisa Mtendaji Mkuu, Abdulkarim Amin 'Popat'.
 
 Azam FC ikiwa na changamoto ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao, imejiridhisha vilivyo hadi kumtwaa Ndayiragije, kwani ana rekodi ya kuifikisha Vital'O ya Burundi hatua ya makundi mwaka 2016. Kama ilivyo utaratibu wa Azam FC kuwapa nafasi wachezaji vijana, Kocha huyo amejipanga vilivyo kuendeleza utaratibu wa kupandisha vijana, ikiwa ndio falsafa aliyopitia pia katika timu zake za awali Mbao na KMC, alizofundisha hapa nchini. Kocha huyo anayesifika kwa soka lake la kasi na pasi fupi fupi, anatarajia kuanza kukinoa kikosi hicho kuanzia Juni 20 mwaka huu, Azam FC itakapoanza maandalizi ya msimu mpya na kujiandaa na michuano ya Kombe la Kagame ikiwa kama bingwa mtetezi.
 
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com