Mkuu wa Mkoawa Ruvuma Mhe. Christina
Mndeme akihutubia Kikao cha Baraza La Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya
ya Nyasa Mkoani Ruvuma jana akiwa katika ziara ya kikazi ya Siku moja
Wilayani Nyasa
(Picha na Ofisi ya DED Nyasa)
……………..
Na Neto Credo- Nyasa
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Christina
Mndeme ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa Kwa kupata hati safi
kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo.
Akizungumza wakati akihutubia baraza la
Madiwani la Halmashauri ya Wilaya hiyo lililofanyika jana katika Ukumbi
wa Kepten John Komba uliopo mjini Mbamba-Bay ikiwa ni sehemu ya ziara
yake ya Siku moja.
“Ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu Za Serikali ni matakwa ya Kikatiba ya Jamhuri ya Muungano
waTanzania ya mwaka 1977 na kufanyiwa marekebisho ya mwaka 2005 kanuni
namba 10 ya sheria ya ukaguzi namba 11 ya mwaka 2008”. Alisisitiza Mhe
Mndeme
Aliongeza kuwa ukaguzi huo upo kisheria
na ni haki ya Halmashuri kukaguliwa na isipokaguliwa ina haki ya kuhoji
kwa nini hamjakaguliwa, kwani hoja zinawahusu wote yaani Madiwani na
watendaji kwa vile Halmashauri ina undwa na pande zote mbili.
Aidha alimpongeza Mhe. Mbunge wa Jimbo la
Nyasa, Mhandisi Stella Martin Manyanya, Madiwani na Wataalam wote wa
Wilaya ya Nyasa kwa kusimamia vema matumizi ya fedha za miradi na kupata
Hati safi katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali kwa Mwaka 2017/2018, na kwa miaka mitano mfululizo kuanzia
mwaka wa fedha 2013/2014 hadi 2017/2018.
“Halmashauri hii imeshakaguliwa na CAG
kwa miaka mitano kuanzia mwaka wa Fedha 2013/2014-2017/2018 katika
kipindi hiki chote Halmashauri imepata Hati safi mara nne (4)na kupata
hati yenye mashaka mara moja Hongereni sana kwa hati mnazoendelea
kupata.haya ni matokeo ya utendaji kazi mzuri wenye mshikamano na
ushirikiano.Inapotokea mmefanya vizuri hata sisi viongozi katika ngazi
ya Mkoa tunafarijika sana kuona Halmashauri zetu zinafanya vizuri. Pia
niwakumbushe pia msibweteke na kuona mmefika mwisho bali kwa mwaka
unaofuata mzuie hoja sio kuzalisha hoja”.Alisisitiza Mhe. Mndeme
Katika Hatua nyingine Alimpongeza
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Nyasa Jimson Mhagama kwa kuteuliwa
kwake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli kuwa Mkurugenzi wa Wilaya ya Nyasa na kumtaka ashirikiane na
Madiwani, Wataalumu na Wananchi ili Wilaya iweze kuwa na Maendeleo.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya
ya Nyasa Mh. Alto Komba alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kwa kufanya
ziara ya siku moja Wilayani Nyasa na kuhudhuria Baraza la Madiwani na
kusema kuwa wananyasa wamefarijika sana kwa ujio wake na wanamkaribisha
siku nyingine akipata nafasi.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Christina
Mndeme alifanya ziara ya siku moja wilayani hapa na kuhudhuria kikao cha
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa na kukagua Miradi
Mitatu ya Maendeleo .Miradi hiyo ni Jengo Ofisi na nyumba ya Mkuu wa
Wilaya ya Nyasa, Jengo la Hosteli ya wasichana katika shule ya Sekondari
Limbo ,na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Nyasa.
0 comments:
Post a Comment