Na MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu,
Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amewataka
viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi kuanzisha viwanda ili kuinua
uchumi na kuchangia adhma ya Serikali ya kuwa na uchumi wa viwanda.
Ametoa kauli hiyo hii leo Aprili 26, 2019 Jijini Dodoma wakati wa
mkutano wake na viongozi hao uliohudhuriwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.
Philip Mpango, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora Mhe. George Mkuchika, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo pamoja na Naibu Waziri
anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana Mhe. Anthony Mavunde ili kujadili
masuala yanayohusu wafanyakazi nchini.
Waziri mhagama aliwataka viongozi hao kuwa wabunifu kwa kuanziasha
viwanda vitakavyowezesha kujikwamua kiuchumi pamoja na kuwajengea uwezo wa kujitegemea
na kukuza mapato ya vyama vyao.
“Niwaombe sana muwe na mitazamo chanya katika kuchangia adhma ya
Serikali kuwa na uchumi wa viwanda kwa kuanzisha viwanda vitakavyowawezesha
kukuza uchumi mfano viwanda vya chaki, mbao na vingine vingi”, alieleza waziri
Mhagama
Aidha aliwaeleza umuhimu wa kuanzisha viwanda hivyo ikiwa ni pamoja na
kuchangia ukuaji wa uchumi nchini, kusaidia kuboresha maslahi ya wafanyakazi na
kuongeza motisha na kutoa fursa za ajira kwa wananchi kwa ujumla.
“Hii leo nimeona niwape changamoto ya kuona umuhimu wa kuwa na viwanda
vyenu kwa kuangalia mchango wenu katika jamii na kuendelea kuwa na tija kwa
kuzingatia umuhimu wa kuwa na viwanda nchini,” alisisitiza Mhagama
Kwa upande wake rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini Bw.
Tumaini Nyamhokya alishukuru mchango wa serikali na maoni yao kwa kuwapa chachu
ya kuona umuhimu wa kuwa na viwanda na kuahidi kulifanyika kazi suala hilo.
“Kipekee nimefurahishwa na maoni na mawazo ya serikali hivyo hatuna budi
kuanza kulifanyia kazi suala hilo ili kuendelea kuwa na mchango katika ukuaji
wa uchumi wa nchi yetu”, alisema Nyamhokya
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake Shirikisho la Vyama vya
Wafanyakazi (TUCTA) Bi. Rehema Ludanga alieleza alivyopokea ushauri huo wa
serikali na kuona ni namna bora ya kujishirikihsha katika uchumi wa viwanda na
kuonesha utayari wa kufanyia kazi suala hilo.
“Binafsi nikiwa kama mwenyekiti Kamati ya Wanawake nimelichukua kwa
dhati kabisa na nitajitahidi kulifanyia kazi mapema iwezekanavyo ili wanawake
nao waweze kunufaika na fursa hii hasa upande wa sekta ya kilimo,” alieleza Bi.
Rehema.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment