Na.Alex Sonna,Kongwa
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe Deo
Ndejembi ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
wilayani humo kuchunguza mapato yanayopatikana kwenye Hospitali ya
Wilaya hiyo.
DC Ndejembi ametoa maagizo hayo
wakati alipofanya ziara ya kushtukiza kwenye Hospitali hiyo ya Wilaya na
kukagua mapato ambayo yamekua yakipatikana hasa kwenye fedha za papo
kwa papo.
Amesema ziara hiyo imekuja baada
ya kuwepo kwa taarifa za baadhi ya watumishi wa Hospitali hiyo kutokua
waaminifu kwenye uandikishaji wa wagonjwa wale wanaolipa fedha za hapo
kwa hapo.
” Nimefanya ziara hii kwenye
Hospitali yetu ya Wilaya kuangalia fedha zile za papo kwa papo. Nilikua
na ‘cashier’ hapo na tumekagua mapato na kugundua kumekua na ukusanyaji
fedha wa kutiliwa mashaka.
” Kwa taarifa tulizonazo kuna
baadhi ya watumishi huwa wanafanya ujanja pale mgonjwa anapokuja, kwa
maana akija mgonjwa ambaye analipia yeye huchukua taarifa zake kana
kwamba yupo kwenye makundi maalum yale ambayo hayakatwi tozo kama wazee,
sasa nimeagiza mara moja Takukuru wafanye uchunguzi kubaini hii hali.
” Mfano hapa tumeangalia mapato ya
siku kwa siku. Kuna siku mapato yanafika laki saba, siku nyingine
tukaona ipo 37,000 lakini leo hapa tumekuta 350,000. Ni jambo ambalo
tumelitia mashaka,” amesema DC Ndejembi.
Aidha ameitaka Takukuru kupitia
taarifa zote za kibenki za Hospitali hiyo ili kuangalia pia kiasi
ambacho kinahifadhiwa kwenye akaunti ni sahihi.
0 comments:
Post a Comment