Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Mhe. Angela Kairuki akizungumza na Wanachama wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania(ATAPE), wakati wa kufunga mkutano mkuu wa 20 wa Chama hicho Mjini Bariadi, Aprili 20, 2019.
Baadhi ya Wanachama wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania(ATAPE), wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji Mhe. Angela Kairuki wakati wa kufunga mkutano mkuu wa 20 wa Chama hicho Mjini Bariadi, Aprili 20, 2019.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na Wanachama wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania(ATAPE), wakati wa kufunga mkutano mkuu wa 20 wa Chama hicho Mjini Bariadi, Aprili 20, 2019.
Na Stella Kalinga, Simiyu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Uwekezaji, Mhe. Angela Kairuki ametoa wito kwa chama cha
wanataaluma na wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania
(ATAPE) na wawekezaji wengine wazawa kuchangamkia fursa mbalimbali za uwekezaji
zilizopo nchini na kusajili miradi yao ya Uwekezaji katika Tume ya
uwekezaji ya Taifa (TIC).
Kairuki ameyasema hayo wakati
akifunga Mkutano wa 20 wa chama cha wanataaluma na wajasiriamali wa Kanisa la
Waadventista Wasabato Tanzania (ATAPE) Mjini Bariadi, ambapo amebainisha
kuwa kwa mwaka huu 2019 wawekezaji wazawa zaidi ya asilimia 72 wamesajili
miradi yao ya uwekezaji TIC.
“ Kwa mwaka huu peke yake tumepata
wawekezaji wazawa waliosajili miradi yao ya uwekezaji TIC zaidi ya asilimia 72,
hii inanipa faraja sana kama waziri wa nchi ninayesimamia uwekezaji ninapoona
Watanzania wenzangu wanachangamkia fursa”
"Naomba mchangamkie fursa hizo
kwa sababu wawekezaji wa nje tunapenda waje tu endapo watakuja kuungana nasi
kwenye mtaji, kubadilishana nasi ujuzi na uzoefu " alisema Kairuki.
Ameongeza kuwa Serikali imeendelea
kuboresha mazingira ya biashara, uwekezaji na kuweka vipaumbele kwa ajili ya
kuvutia wawekezaji katika sekta ambazo zitakuwana athari na tija kubwa kiuchumi
kwa wananchi, ili kuimarisha minyororo ya thamani katika kilimo,uvuvi, na
mifugo ambayo ni maeneo yanayoajiri Watanzania wengi zaidi.
Aidha, Waziri Kairuki amezitaja sekta
nyingine za kipaumbele kuwa ni uzalishaji wa mafuta ya kula kwa kutumia
mbegu zinazozalishwa nchini, uzalishaji wa sukari, uzalishaji wa dawa za
binadamu, vifaa tiba na kemikali, ujenzi wa miundombinu ya uvuvi wa kisasa,
viwanda vya kuchakata samaki, kusindika nyama, viwanda vya kubangua korosho,
viwanda vitakavyotumia pamba na viwanda vya pembejeo na mbolea.
Katika hatua nyingine Waziri Kairuki
ameipongeza ATAPE kwa jinsi inavyoshirikiana na Serikali katika kutoa huduma
mbalimbali za kijamii ikiwemo sekta ya afya, elimu, maji pamoja na huduma
nyingine.
Kairuki amesema serikali pekee
haiwezi kutatua changamoto zote hivyo kwa kushirikiana na wadau ikiwemo
taasisi za dini wanaweza kuwahudumia wananchi na kuleta mabadiliko chanya ikiwa
ni pamoja na kuhubiri amani, huku akisisitiza kuwa masomo ya ujasiriamali
yanayotolewa kwa wana ATAPE wayatumie kwa manufaa ya kanisa na jamii kwa
ujumla.
Awali akimkatibisha waziri Kairuki,
mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema mkutano huo
umewasaidia watu wa Simiyu kukutana na watu wa maeneo mengine
hatua iliyopelekea kubadilishana uzoefu sambamba na kuongeza na kupata
masoko mapya .
‘’watu wetu wameongeza wigo wa
masoko, mmebadilishana uzoefu ....huu ni mkoa wa kibiashara na ni mkoa wenye
fursa nyingi; tunajenga tawi la chuo cha usimamizi wa fedha (IFM) hivyo
ninawaalika wafanyabiashara na Watanzania wote kuja kuwekeza ujenzi wa hosteli
eneo lile linalojengwa tawi hilo"alisisitiza Mtaka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa ATAPE
Freddie Manento amesema kwa miaka mitatu ATAPE imewekeza miradi ya bilioni 1.2
katika miradi yenye manufaa kwa kanisa, wanajamii na wana ATAPE.
Alisema wamewekeza kwenye miradi ya
maji kwenye maeneo yenye uhitaji mkubwa, miradi ya miti ya matund), korosho na
miradi ya mashamba ya mihogo kwa kutengeneza ajira na faida katika vijiji
walivyolima mashamba yao.
‘’Wana ATAPE wamejitoa kwelikweli na
wameitikia dhana yetu ya kutumia vipaji na rasilimali zetu kwa ajili ya kazi ya
MUNGU, hii iko katika mathayo 28;19, 20…hii ndio dhana yao’’ alisema Manento.
Mkutano wa Wanataaluma na
Wajasiriamali (ATAPE) kutoka kanisa la Waadventista Wasabato umefanyika mkoani
Simiyu kwa muda wa siku sita ambapo umehudhuriwa na wananchama zaidi ya 1500.
0 comments:
Post a Comment