Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akitoa tahadhari kuhusu kuzuka kwa ugonjwa wa Dengue nchini. Kushoto ni Mganga mkuu wa Serikali Prof. Mohammed Kambi
Na WAJMW-DODOMA
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa tahadhari ya kuwepo kwa ugonjwa wa Dengue nchini ambao umebainika katika mikoa ya Dar Es Salaam na Tanga.
Akitoa tahadhari hiyo mbele ya waandishi wa habari jijini Dodoma leo, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amesema hadi kufikia April 2 2019 kati ya watu 470 waliopimwa, wagonjwa 307 wamethibitishhwa kuwa na virusi vya ugonjwa wa Dengue, na kati ya hao 252 ni kutoka Dar Es Salaam na 55 ni kutoka Tanga.
Dkt. Ndugulile amesema ugonjwa wa homa ya Dengue unasababishwa na virusi vinavyoenezwa na mbu wa aina ya “Aedes” ambao ni weusi wenye madoadoa meupe yenye kung’aa.
Aidha, Dkt. Ndugulile ametaja dalili za ugonjwa huu kuwa ni homa ya ghafla, kuumwa kichwa hususani sehemu za macho, maumivu ya viungo na uchovu. Dalili hizi huanza kujitokeza kati ya siku 3 hadi 14 tangu mtu alipoambikizwa virusi vya ugonjwa huu.
Naibu Waziri huyo amewataka wananchi kuwa makini pindi wapatapo homa na wahakikishe wanakwenda kupata huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya ili waweze kupimwa na kupatiwa tiba sahihi.
Dkt. Ndugulile amewataka wananchi kusafisha mazingira na kufukia madimbwi ambayo mbu aina ya Aedes hupendelea kuzaliana kwenye maji yaliyotuama karibu na makazi ya watu au hata ndani ya nyumba, kuondoa vitu vyote vinavyoweza kuweka mazalia ya mbu kama vile vifuu vya nazi, makopo, magurudumu ya magari. Pia wanatakiwa kufyeka vichaka na kusafisha gata za mapaa ya nyumba ili kutoruhusu maji kutuama.
Pamoja na hayo, Dkt. Ndugulile amesema mbu hawa huwa na tabia ya kuuma Zaidi wakati wa mchana hasa wakati wa asubuhi jua linapochomoza na jioni jua linapozama na hivyo wananchi wanatakiwa kujihadhari.
0 comments:
Post a Comment