Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amepongeza mshikamano uliopo
katika uongozi wa wilaya ya Nkasi unaongozwa na Mkuu wa wilaya hiyo Mh. Said
Mtanda baada ya kuona namna uongozi huo ulivyojipanga katika kuhakikisha
maelekezo na maagizo ya serikali yanatekelezwa kwa wakati hasa maendeleo ya
ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Nkasi.
Amesema kuwa mshikamano huo ni tunu kwa wanarukwa katika kuhakikisha
maendeleo yanapatikana katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo na hasa linapokuja
suala la utekelezaji wa upatikanaji wa huduma ambazo zinawagusa moja kwa moja
wananchi waliokuwa wakisubiri huduma hizo kwa muda mrefu.
“Nimeona kwamba mmejipanga kwa kuleta vifaa, na kama hakuna vifaa ujenzi
utasuasua, kuna mawe naona yanakwenda kwasababu yanahitajika kwa kasi kubwa,
basi hilo eneo liwekewe nguvu kubwa sana, ndio eneo lenye hitaji kubwa kwa sasa
na kama hakuna mawe tutashindwa kusogea hatua ya kuweka matofali hadi kufikia
hatu ile ya linta,” alisema
Aliongeza kuwa hivi sasa mvua hakuna, hivyo ni wakati muafaka wa
kuhakikisha vifaa vyote vinavyohitajika kwaajili ya ujenzi vinakuwa katika eneo
hilo la ujenzi ili kila hatua ya ujenzi isikumbane na kikwazo cha kukosa vifaa
na kutoa sababu ya mvua kuharibu barabara na hivyo vifaa kushindwa kufika.
Halikadhalika ametoa pongezi kwa namna vibarua wa ujenzi huo
wanavyolipwa kwa wakati na kufanya kazi wakiwa wameridhika na malipo wanayopewa
jambo linaloashiria kuwa ujenzi huo unakwenda bila ya dosari zozote na kuagiza
kuwa hadi kufikia tarehe 10 Mei, 2019 majengo yote saba ya hospitali hiyo yawe
yamefikia usawa wa linta ili kwenda na kasi ya utoaji huduma kwa jamii.
Mh. Wangabo ameyasema hayo alipokwenda kuona maendeleo ya ujenzi wa
hospitali ya wilaya inayojengwa katika makao makuu ya wilaya ya Nkasi mjini
Namanyere ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa juu ya kuwataka Wakuu wa Mikoa kusimamia kwa karibu
ujenzi wa hospitali hizo na hatimae kumalizika kwa wakati.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda alisema kuwa ili
kuhakikisha vibarua na wagonga kokoto wanalipwa na mafundi walioingia nao
mkataba, wameweka utaratibu wa mafundi hao kuwalipa mbele yake, zoezi
linalofanyika katika ukumbi wa ofisi yake ya wilaya na wakati huo huo wakitumia
fursa hiyo kuwapatia wagonga kokoto hao vitambulisho vya ujasiliamali.
Imeelezwa kuwa ili majengo saba ya hospitali hiyo yakamilike
yanahitajika matofali 78,000 huku hadi tarehe 18 Aprili,2019 matofali 58,000
tayari yameshafyatuliwa ili kuendelea na ujenzi huo.
0 comments:
Post a Comment