Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Kushoto), Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Joseph Kakunda (Katikati) pamoja na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Jackson Mwansasu wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kutatua kero za wakulima na wafanya biashara wa Viazi Mviringo katika eneo la Uyole Jijini Mbeya leo tarehe 30 Aprili 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Kushoto), Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Joseph Kakunda (Katikati) pamoja na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Jackson Mwansasu wakiwa katika mkutano wa utatuzi wa kero za wakulima na wafanya biashara wa Viazi Mviringo katika eneo la Uyole Jijini Mbeya leo tarehe 30 Aprili 2019.
Sehemu ya wakulima na wafanya biashara wa Viazi Mviringo katika eneo la Uyole Jijini Mbeya wakifatilia mkutano wa utatuzi wa kero za zao hilo leo tarehe 30 Aprili 2019.
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mbeya
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb), Waziri wa
Viwanda na Biashara Mhe Joseph Kakunda pamoja na Naibu Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Jackson wameungana kutatua kadhia za
zilizokuwa zinawakumba wakulima na wafanyabiashara wa viazi mviringo Mkoani Mbeya.
Viongozi hao wamevalia njuga kadhia za wakulima na
wafanyabiashara wa viazi mviringo ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikiwasumbua
wafanyabiashara hao.
Wakizungumza Leo tarehe 30 Aprili 2019 mbele ya
viongozi hao wakulima hao katika mkutano uliofanyika katika eneo la Uyole Jijini Mbeya, wakulima hao waliiomba serikali kutatua changamoto ambazo kwa muda mrefu zimekuwa kero bila kupatiwa majibu.
Kero zinazowakabili wakulima wa viazi mviringo ni
pamoja na faini zisizo rafiki za vifungashio, Ufungaji wa mifuko (zipu) wakati
wa kusafirisha usumbufu wa mawakala wa kilimo wakati wa kusafirisha viazi
pamoja na sheria ya vipimo kutokuwa rafiki kwani viazi hutofautiana uzito
kutokana na msimu.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Japhet Kakunda
(Mb) amepiga marufuku faini ambazo ni kinyume na taratibu za nchi sambamba na
kuzuia utozaji faini kwa wafanyabiashara hao kwa gunia badala yake amesema
utawekwa utaratibu wa kutoza faini kwa kilo ili kuepuka wizi na rushwa.
Kero nyingine ni pamoja na Rushwa kwa baadhi ya
watumishi wa viwango hususani katika vituo wakati wa kupima katika vituo vya
ukaguzi visivyo rasmi vilivyopo katika eneo la Makambako, Iringa, Morogoro,
Mikese na Kibaha.
Mhe Hasunga alisema kuwa serikali ya awamu ya tano
inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli imedhamiria kwa dhati kutatua
kero zisizo rafiki kwa wakulima na watanzania wote.
“Kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu sasa kwenye
zao hili muhimu la viazi mviringo ndio maana Leo tumeambatana na Waziri wa
Viwanda ili kupata ufumbuzi wa kadhia hizo" Alikaririwa Mhe Hasunga
Kadhalika, aliwaeleza wakulima hao waliojitokeza
katika mkutano huo kuwa Wizara yake imejipanga kuhakikisha kuwa wakulima wote
nchini wanasajiliwa ili kubaini kiwango cha mashamba wanayolima na uwezo wa
uzalishaji wa mazao.
Vilevile alieleza kuwa serikali imeanza mkakati wa kuwa
na Bima ya mazao kwani kufanya hivyo wakulima watakuwa na ahueni pindi
yanapotokea majanga katika mazao wanayolima.
Naye Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Tulia Ackson
amewapongeza wakulima hao wa viazi mviringo kwa kuwa wavumilivu wakati serikali
inatafuta ufumbuzi wa kadhia hizo zinazowakabili.
Alisema kuwa wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na
Wizara ya Viwanda na Biashara zimekutana kutatua kadhia hizo ili wakulima
mkoani Mbeya na mikoa mingine nchini waweze kuzalisha na kusafirisha mazao yao
pasina kadhia yoyote.
Pamoja na mambo mengine amewashukuru viongozi hao
kwa pamoja kwa kukubali na kuzipatia ufumbuzi kadhia hizo, huku akiahidi kwa
ushirikiano wake pamoja na wakulima hao kutaanzishwa umoja wa kudumu ili kupata ufumbuzi wa
changamoto zingine katika kilimo na viwanda.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment