METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, April 9, 2019

Kwa nini hamuwanyang’anyi Leseni Wauzaji wa Pembejeo ‘Feki’??? – Naibu Waziri Bashungwa


Mgeni Rasmi wa Mkutano huo wa Wadau wa Pembejeo, Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Innocent Bashungwa akiwahutubia Wadau wa Pembejeo kutoka Taasisi mbalimbali za Wizara ya Kilimo pamoja na Washiriki wengine kutoka Sekta Binafsi pamoja na Wasambaji na Wauzaji wa Pembejeo za Kilimo kulia kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Udhibiti wa Mbegu Bora (TOSCI) Bwana Patrick Ngwediagi
 Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Nyasebwa Chimangu akitoa neon fupi la utangulizi kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi Naibu Waziri WIzara ya Kilimo Mhe. Innocent Bashungwa kwenye kwenye Mkutano wa Wadau wa Pembejeo Jijini Dodoma katika Ukumbi wa Bwalo la Polisi


Sehemu ya Washiriki Mkutano huo wa Wadau wa Pembejeo wakimsikiliza Mgeni Rasmi, Naibu Waziri Wizara ya Kilimo, Mhe. Innocent Bashungwa katika ukumbi wa Bwalo la Polisi Jijini Dodoma

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Innocent Bashungwa amewaelekeza Wadau wote kwenye mnyororo wa pembejeo kuwa sasa ni wakati wa kusimamia ipasavyo Sheria zote zinazohusu tasnia ya pembejeo kuanzia viutatilifu, mbegu pamoja na mbolea ili kumsaidia Mkulima mnyonge wa Tanzania.

Mhe. Bashungwa ameyasema hayo leo tarehe 9/4/2019 wakati akifungua mkutano wa Wadau wa Pembejeo za kilimo ambapo Taasisi ya Udhibiti wa Mbegu Bora (TOSCI) imeandaa mkutano kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) na Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu katika Ukanda wa Kitropiki (TPRI) kwa lengo la kufanya tathmini ya maboresho ya mambo kadhaa yenye lengo la kuboresha utendaji kazi wa Taasisi hizo kwa pamoja.

Naibu Waziri Bashungwa amesema Mkulima wa Tanzania amekuwa akikabiliwa na changamoto nyingi wakati wa kuendesha kilimo chake na kuongeza kuwa changamoto hizo ni pamoja na viuatilifu ‘feki’, mbegu hafifu na ‘feki’ pamoja na mbolea ‘feki’ sasa zinapaswa kuisha kwa kuwa Taasisi zote zimepewa mamlaka ya kumkamata na kumfungulia mashitaka muuzaji yeyote atakaye kutwa akiuza au kusambaza pembejeo ‘feki’ na kuongeza kuwa amekuwa akishangazwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa jambo hilo.

“Ndugu zangu Wataalam nimekuwa nikisikia na kuona idadi ndogo ya Wasambazaji na Wauzaji wa pembejeo feki wanaokamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria, tofauti na idadi kubwa ya malalamiko ya Wakulima wetu, sasa iwe mwisho, Wasambazaji na Wauzaji wanafahamika, simamieni sheria, wakamatwe na wafikisheni kwenye vyombo vya sheria na wanapopatikana na hatia, wafungwe kwa mujibu wa sheria.” Amekaririwa Waziri Bashungwa.

“Si sawa Wasambazaji feki wa pembejeo kuendelea na mchezo huu, huu ni wakati wa kuwadhibiti na kuwafunga, kwa sababu sheria zipo na zinasema wazi wazi, adhabu ya Mtu anayefanya kosa hilo” Amekaririwa Mhe. Bashungwa.

Naibu Waziri Bashungwa ameagiza kuwa mbali na mambo mbalimbali watakayojadiliana katika mkutano huo msisitizo lazima uwekwe kwenye kutafu njia bora ya kuongeza ufanisi na kuondoa changamoto kwenye upatikanaji na utoaji wa huduma ya usambazaji wa pembejeo bora kwa Wakulima na kama kuna vikwazo vyovyote mkutano huo utoe mapendekezo kwa Wizara nini kifanyike.

Napenda mjikite katika kujadiliana  ili kuibua vikwazo vyote ambavyo mnaona kama vitaboreshwa basi vitasaidia usambazaji wa pembejeo zote kufika kwa Mkulima katika hali ya ubora ili Sekta ya Kilimo iwe na uzalishaji mkubwa na wenye tija kwenye mazao ya Kimkakati, mazao ya chakula na mazao yenye thamani kubwa.

“Naomba mtuambie kama kuna Sheria au Kanuni ambazo haziendi sambamba na mahitaji ya nyakati na zimekuwa kikwazo, ili huduma ya kufikishia Mkulima Viuatilifu sahihi, mbegu bora mtuambie na kutushauri, njia zipi zitakuwa sahihi katika kufikisha maarifa mapya kwa Wakulima kwa lengo la kuongeza tija na uzalishaji” Amekaririwa Mhe. Bashungwa.

Mkutano huo wa siku mbili unaowakutanisha Wadau mbalimbali pamoja na Taasisi kubwa tatu, ambazo zinahusika moja kwa moja udhibiti wa pembejeo za kilimo kuanza udhibiti wa viuatilifu (Madawa), mbegu na mbolea. Taasisi hizo ni pamoja na Taasisi inayojishughulisha na masuala ya Udhibiti wa Mbegu Bora (TOSCI). Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) pamoja na Taasisi ya Utafiti na Udhibiti wa Viuatilifu katika Ukanda wa Kitropiki (TPRI).
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com