Serikali ya awamu ya tano imefanikiwa kuvuka kiwango
cha upatikanaji wa dawa muhimu kwa binadamu kilichowekwa na Shirika la Afya Duniani
(WHO) katika ngazi ya Hospitali ya Wilaya kwa kuwa na idadi kubwa ya dawa
muhimu zinazopatikana kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu alipotembelea Hospitali Teule
ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe kujioinea hali ya utoaji wa huduma.
Waziri Ummy Mwalimu aliyeongozana na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula pamoja na watendaji walio chini ya Wizara
yake, amesema kuwa Serikali ya awamu ya tano imeendelea kuboresha upatikanaji
wa dawa kwa wananchi huku ikipitiliza kiwango kilichowekwa na WHO kwa kuwa na
dawa muhimu 312 huku kigezo kilichowekwa na Shirika la Afya Duniani kikiwa ni
dawa 30.
“Tuna mfumo wa ukusanyaji wa taarifa kuanzia ngazi
ya zahanati, kituo cha afya mpaka hospitali unaotuwezesha Serikali kutambua
mahitaji na matumizi ya dawa katika vituo vya kutolea huduma” amesema Waziri
Ummy wakati akifafanua namna ya Serikali ilivyojipanga kupata takwimu sahihi za
dawa.
Waziri Ummy amesema kuwa zipo propaganda
zinazoendeshwa na watu wenye ushawishi ambao wamekuwa wakiwahadaa wananchi kwa
kusema kuwa dawa hakuna ili hali dawa zipo na zinapatikana katika vituo vya
kutolea huduma.
“Ni lazima tumtendee haki Rais wetu DKt. John Pombe
Magufuli, amefanya makubwa kwenye Sekta ya Afya kwa kuboresha upatikanaji wa
Dawa, tunaposema tumeongeza upatikanaji wa dawa maana yake dawa zinapatikana
kwa urahisi hata kwenye vituo binafsi” amesema Waziri Ummy,
Waziri Ummy amezitaja dawa zenye kipaumbele kikubwa
zikiwemo Dawa za kudhibiti maambukizi ya bakteria (Antibiotics), Dawa za
kudhibiti Malaria, Dawa za magonjwa yasiyo ya kuambukiza, Dawa za uzazi salama
pamoja na Dawa za maumivu.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt.
Zainab Chaula amesema kuwa Ofisi yake kupitia Waziri wa Afya wako mbioni
kuwasilisha muswada wa Bima ya Afya ambao utawawezesha wananchi wote sasa kuwa
na bima ya afya.
Aidha, Dkt. Chaula amewataka watumishi katika
Hospitali hiyo kuwahamasisha zaidi wagonjwa kujiunga na huduma za bima ya afya
ili kuwa na uhakika wa matibabu pindi wanapougua.
“Niwaombe watendaji wote hapa kuwasisiza wagonjwa
wanaofika hapa kupata matibabu kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya”
Alisema Dkt. Chaula.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Winfred
Kyambile amesema kuwa hali ya upatikanaji wa huduma imeimarika kutokana na
mapato kuongezeka hivyo kuiwezesha Hospitali kutoa huduma bora kwa wananchi.
Dkt. Kyambile amesema kuwa kuongezeka kwa
upatikanaji wa dawa imesaidia kuongezeka kwa mapato hospitalini hapo,
amesema kuwa hapo awali mapato ya hospitali hiyo kwa mwezi yalikuwa Shilingi
Milioni 12 huku sasa mapato hufikia Shilingi milioni 90 mpaka 100, fedha ambazo
amesema wanazitumia kuboresha huduma za afya katika hospitali hiyo.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment