Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe.Angellah Kairuki akisalimiana na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Sarah Cooke, ofisini kwake Jijini Dodoma Machi 13, 2019 alipokutana naye na kufanya mazungumzo.
Balozi wa Uingereza nchini, Sarah Cooke akizungumza jambo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe.Angellah Kairuki alipomtembelea Ofisini kwake Machi 13, 2019 Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe.Angellah Kairuki akiteta jambo na balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Sarah Cooke mara baada ya kumaliza mazungumza yao, kulia ni Beth Arthy aliyeambatana na balozi huyo.
NA.MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Uwekezaji Mhe.Angellah Kairuki amekutana na kufanya mazungumzo
na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Sarah Cooke mapema hii leo Machi 13,
2019 katika ofisi zake Jijini Dodoma
Lengo la mazungumzo hayo ilikuwa ni
kujadili maeneo muhimu yanayohusu masuala ya uwekezaji ambapo Waziri
Kairuki alieleza vipaumbele muhimu vya uwekezaji vitakavyochangia adhma
ya Serikali ya kuwa na uchumi wa viwanda ikiwemo kuwekeza katika maeneo ya
kilimo, elimu, afya, viwanda vya nguo pamoja na ujenzi wa Miundombinu ya
barabara.
“Ninafarijika kwa ujio wako na ni
ishara nzuri ya mahusiano mazuri yaliyopo baina ya nchi hizi mbili naamini
yatasaidia katika fursa za uwekezaji hasa kwa namna Uingereza ilivyochangia
katika maeneo muhimu nchini ikiwemo elimu,”alisema Kairuki
Waziri aliongezea kuwa, Serikali
itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji kwa kuzingatia mchango
unaotokana na wawekezaji hasa katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo
nchini.
Waziri Kairuki alieleza kuwa, kuwepo
kwa Idara ya uwekezaji katika Ofisi ya Waziri Mkuu ni hatua muhimu kwani
itasaidia kuongeza nguvu ya ufuatiliaji na utekelezaji wa masuala hayo na
kuendelea kuleta mabadiliko katika kutatua changamoto zilizozikabili sekta
hiyo.
Aidha alimshukuru balozi huyo kwa hatua
ya mazungumzo yenye tija pamoja na kuendelea kuunga mkono nchi ya Tanzania na
kuwataka kuendeleza urafiki huo kwa kuwekeza zaidi katika maeneo aliyoyaainisha
ikiweko yale ya vipaumbele.
Naye Balozi wa Uingereza Nchini
Tanzania, Sarah Cooke aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuwa na sera
zinazovutia wawekezaji pamoja na maboresho yanayofanywa kuwavutia wawekezaji
nchini ikiwemo maeneo ya ulipaji wa kodi.
“Tunaelewa kuwa Serikali inafanya
jitihada kubwa katika kuboresha mazingira ya biashara ikiwa ni pamoja na
mazingira ya ulipaji wa kodi tunaahidi kuendelea kutoa ushirikiano ili kuwa na
mchango katika maendeleo ya nchi pamoja na kuimarisha mahusiano
yaliyopo,”alisisitiza Cooke.
=MWISHO=
0 comments:
Post a Comment