METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, March 7, 2019

SIMIYU KUPATA CHUPA MILIONI TATU ZA VIUDUDU KWA ZAO LA PAMBA





Mkoa wa Simiyu utapokea chupa milioni tatu  za viuadudu katika msimu huu wa mwaka 2018/2019 lengo likiwa kukabiliana na changamoto ya wadudu  waharibifu wa zao la hilo.

Mkurugenzi Bodi ya Pamba nchini, Bw. Marco Mtunga ameyasema hayo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omari Mgumba mkoani Simiyu Machi 06, 2019 ambapo amebainisha kuwa tayari bodi imeshasambaza chupa milioni moja na laki tatu za viuadudu hivyo kwa mkoa huu na kuongeza Simiyu pekee   itapokea chupa milioni tatu za viuadudu kwa msimu huu.
  
Akiwa ziarani mkoani Simiyu Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omary  Mgumba  amesema suala la mbegu za pamba limeenda vizuri  hivyo ni vema likaenda sambamba na usambazaji wa viuadudu na kuongeza kuwa wakulima  wa zao hilo wameongezeka kutokana na zao hilo kufanya vizuri hususani mkoa wa Simiyu ambao umeongoza kwa uzalishaji ikilinganishwa na mikoa mingine inayolima pamba hapa nchini.

“Suala la mbegu lilienda vizuri lakini kubwa zaidi ni mahitaji makubwa kuliko matarajio kutokana na hamasa mliyofanya mwaka jana watu wengi walihamasika kulima pamba, hata mwaka huu wengi zaidi watakuwa wamelima, maana wakulima wengi huwa wanahamasika kulima zao ambalo limefanya vizuri msimu uliopita” alisema Mgumba.

Awali akimkaribisha Naibu Waziri wa Kilimo,  Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema kuwa lengo la mkoa ni kuongeza uzalishaji kwa ekari kuanzia kilo 500 hadi 1000 kwa ekari badala ya kuongeza idadi ya wakulima pekee.

“Tungehitaji kuongeza uzalishaji kwa ekari badala ya kuongeza uzalishaji kwenye idadi ya wakulima, mwaka 2018 tulivuna kilo milioni 113, mwaka huu uzalishaji utaongeza lakini unaweza kuongezeka kutokana na ongezeko la wakulima na ekari zilizolimwa; wakati tunaweza kupata kilo kama hizo kwenye pungufu ya ekari na idadi ya wakulima kama tutaongeza uzalishaji kwa ekari”

“Msukumo wa Mkoa ni kuona tunaongeza uzalishaji kwa ekari, ukienda Mwabusalu kuna wakulima wanazalisha kuanzia kilo 500 hadi 1000 kwa ekari , kwa hiyo kama mkoa tumejipanga kuhakikisha uzalishaji unaongezeka kwa ekari na idadi ya wakulima pia inaongeza” alisema Mtaka.

Naibu Mgumba yuko mkoani Simiyu katika ziara ya kikazi yenye lengo la kukagua shughuli za kilimo na ushirika zinavyoendelea pamoja, kukagua shughuli za miradi ya umwagiliaji akiwa Wilayani Itilima amepata nafasi ya kuzugumza na wananchi kupitia mkutano wa hadhara.

MWISHO


CAPTIONS:-
PICHA 1:-Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe.Omary Mgumba akizungumza na baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Simiyu na  wadau wa kilimo, wakati wa ziara yake mkoani Simiyu Machi 06, 2019.
PICHA 2:-Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (wa pili kushoto) akizungumza na baadhi ya viongozi wa Mkoa na wadau mbalimbali wa  kilimo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe.Omary Mgumba mkoani  humo Machi 06, 2019.
PICHA 3:-Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba, Bw. Marco  Mtunga akizungumza na wadau mbalimbali wa  kilimo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe.Omary Mgumba mkoani  humo Machi 06, 2019.
PICHA 4:- Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na baadhi ya viongozi wa Mkoa na wadau mbalimbali wa  kilimo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe.Omary Mgumba mkoani  humo Machi 06, 2019.
PICHA 5:-Baadhi ya viongozi na wadau wa Kilimo mkoani Simiyu wakiwa katika kikao na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe.Omary Mgumba wakati wa ziara yake mkoani humo Machi 06, 2019.


Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com