Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaagiza
Wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wananfunzi wa shule zote za serikali
katika halmashauri za mkoa huo zinaandikwa ujumbe wa “Niache Nisome” kwa herufi
kubwa mbele ya flana zao za shule ili kuufikisha ujumbe huo kwa wale wote wenye
nia na dhamira ya kukwamisha masomo ya wanafunzi hao kuanzia kidato cha kwanza
hadi kidato cha sita.
Amesema kuwa kwa kufanya hivyo kutapunguza idadi ya
wanafunzi wa kike kupata mimba pamoja na kumaliza utoro kwani ujumbe huo
utawalenga wazazi pamoja na vijana wenye tabia ya kuwanyemelea wanafunzi wa
kike na kuwalaghai kwa kuwanunulia chipsi pamoja na kuwapakiza bure katika
usafiri wa pikipiki maarufu kama Bodaboda ili waweze kuwapa mimba na hatimae
kukatisha masomo yao.
“shule zote ziandikwe maneno “niache Nisome”
Mkurugenzi kama kuna “T-shirt” imeandikwa maneno mengine zifutwe, ziandikwe
“Niache Nisome” tena ziwe na herufi kubwa nzuri, ujumbe huu ufike mbali, ujumbe
kwa watanzania, ujumbe wa watu wote wa mkoa wa Rukwa “Niacheni Nisome”
Msitusumbue, vichipsi chipsi vile hakuna kwa Watoto wa kike, sijui bodaboda,
utoro utoro, “Niacheni Nisome””, Alisema.
Aliyasema hayo alipotembelea katika shule ya
sekondari Kate, iliyopo Kata ya Kate, Wilayani Nkasi na kupokea taarifa ya
shule hiyo iliyoonyesha ufaulu mzuri kwa wananfunzi wa kidato cha sita na
ufaulu mbovu kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne jambo
lililopelekea Mkuu wa Mkoa kushtushwa na hali hiyo ya wanafunzi kuwa katika
shule moja na kuwa na ufaulu tofauti.
Halikadhalika alielezea kuwa kitendo cha wanafunzi
wa kidato cha kwanza kushindwa kufika shuleni kwa wakati na kuwa watoro ni
sababu mojawapo ya kupelekea kushindwa mitihani ya kidato cha pili kutokana na
kuwakuta wanafunzi wenzao wakiwa wamekwishapiga hatua katika masomo na
ukizingatia kuwa lugha ya kufundishia ni ya kigeni hivyo hupelekea mwanafunzi
huyo kushindwa kuwa sawa na wanafunzi wenziwe na hatimae kukata tamaa, hali
inayopelekea kushindwa kidato cha nne.
Kwa upande wake makamu mkuu wa shule ya sekondari
Kate alisema kuwa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa
mwaka 2019 katika shule hiyo, wa kiume ni 144 na wa kike ni 155 na kufanya
jumla yao kuwa 299 huku walioripoti wa kiume wakiwa 27 na wa kike 19 na kufanya
jumla yao kuwa 46 na hivyo wanafunzi 253 bado kuripoti shuleni hapo tangu shule
kufunguliwa tarehe 7.1.2019.
0 comments:
Post a Comment