Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na Waziri Mkuu) Bi.Maimuna Tarishi akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha ya kupunguza madhara ya maafa nchini na kuimarisha uthabiti kwa nchi na jamii dhidi ya majanga ya asili katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara iliyofanyika katika Ukumbi wa Mazengo Dodoma hoteli Januari 28, 2019.
Mwakilishi Mkazi wa Taasisi za Umoja wa Mataifa nchini Tanzania Bw.Alvaro Rodriques akiwasilisha hotuba yake wakati wa warsha hiyo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na Waziri Mkuu) Bi.Maimuna Tarishi (wa tano kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe walioshiriki katika warsha hiyo.
NA MWANDISHI WETU
Serikali kwa ushirikiana na wadau wengine
imejipanga kuendelea kukabiliana na majanga yanayoikumba nchi ili kuhakikisha
inashughulikia na kutatua majanga hayo pindi yanapotokea.
Hayo
yameelezwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Bunge na Waziri
Mkuu, Maimuna Tarishi Januari 28, 2019 wakati akifungua warsha ya kupunguza madhara ya maafa nchini na
kuimarisha uthabiti kwa nchi na jamii dhidi ya majanga ya asili katika ukanda
wa Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Tarishi alibainisha jitihada zinazofanywa na
Serikali ili kukabili maafa ikiwa ni pamoja na kuendelea kuelimisha umma juu ya
umuhimu wa kuimarisha ustahimilivu wa majanga ya asili kwa kuongeza idadi ya
wilaya zenye mipango ya kupunguza madhara ya maafa, kuboresha mifumo ya
tahadhari za awali, kuongeza utoaji wa elimu kwa umma na kuimarisha shughuli za
kujiandaa, kukabili na kuimarisha mfumo wa uratibu wa masuala ya maafa.
“Kwa kuzingatia Mpango wa Pili wa Maendeleo
wa Miaka wa Mitano, 2016/17- 2020/21 tutaendelea kuimarisha ustahimilivu wa
majanga ya asili pamoja na kukabili majanga kwa kuzingatia utekelezaji wa
malengo ya msingi ya Mfumo wa Sendai wa Kupunguza Madhara ya Maafa wa mwaka
2015 – 2030, tumedhamiria kuhakikisha tunakabiliana na majanga ili kujiletea
maendeleo,”alisema Tarishi
Aliongezea kuwa, kwa kuzingatia majanga
yanayoikabili nchi ikiwemo mafuriko nchi haina budi kuwa mikakati hiyo ili
kuhakikisha inakabili na kuweka mikakati yenye tija katika masuala ya
menejimenti ya maafa nchini.
Tarishi alibainisha kuwa, mafuriko yamekuwa
na athari nyingi kwa kulinganisha na majanga mengine yanayoikabili nchi mara
kwa mara kwa kuzingatia takwimu zilizopo kwa sasa.
“Takwimu zinaonesha kuwa kwa kipindi
cha Januari hadi Desemba, 2018 mafuriko yameathiri wilaya 50 na kusababisha
vifo kwa watu 71, majeruhi kwa watu 64, kuharibiwa nyumba 15,802 kwa viwango
tofauti, kuathiri miundombinu katika shule 43, mashamba ya mazao mbalimbali, na
vituo vya afya,”alisisitiza Tarishi
Alieleza kuwa, takwimu zilizopo tangu tupate uhuru nchi imeathiriwa na
ukame zaidi ya mara 18 ikimo yale ya mwaka 2006/2007 na 2007/2008 ambayo yaliathiri
zaidi mikoa ya Arusha, Dodoma, Iringa, Kilimanjaro, Manyara, Shinyanga, Lindi,
Singida, Tabora na Mwanza.
Sambamba na hilo Ukame mwingine mkubwa
ulitokea mwaka 2008/2009 ulioathiri zaidi mikoa ya kaskazini ya nchi hasa
Arusha na Manyara. Mikoa ambayo mara nyingi huathiriwa na ukame ni Dodoma,
Singida, Tabora na Shinyanga, ambayo kawaida hupata mvua ya chini kwa kiwango
cha kati ya milimita 200 - 600 kwa mwaka.
Naye Mkuu wa Sekretarieti ya Kupunguza
Madhara ya Maafa ya Umoja wa Mataifa kwa Kanda ya Afrika, Amjad Abbashar,
alieleza mipango mikakati ya kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali kwa
kuzingatia ongezeko la madhara yatokanayo ya maafa ikiwemo vifo, upotevu wa
makazi, pamoja na uharibifu wa mali za watu.
“Tutaendelea kushirikiana na kuhakikisha
tunakabili na kuzuia maafa yasitokee pale itakapotokea ili kuendelea kuwa na
maendeleo endelevu katika mazingira tuliyonayo,”alieleza Abbashar
Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Taasisi
za Umoja wa Mataifa nchini Tanzania,Alvaro Rodriques, aliwataka wajumbe
kuitumia fursa ya warsha hiyo kwa kuzingatia mada zitakazowasilishwa ili
kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na wataalam na mikakati yenye kutatua madhara
yatokanayo na majanga na kuahidi kuendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa
na Serikali ya Tanzania katika kushughulikia maafa.
Awali, Warsha ya kupunguza madhara ya maafa nchini na
kuimarisha uthabiti kwa nchi na jamii dhidi ya majanga ya asili katika ukanda
wa Kusini mwa Jangwa la Sahara imeratibiwa na Idara ya Usimamizi wa shughuli za
Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa
kushirikiana na Sekretarieti ya Kupunguza Madhara ya Maafa ya Umoja wa Mataifa
na Taasisi ya Utafiti ya CIMA kupitia ufadhili wa Umoja wa Ulaya. Aidha warsha
inatarajiwa kudumu kwa siku tano hadi Februari 01, 2019 Jijini Dodoma. Warsha hiyo
ni sehemu ya utekelezaji wa programu ya Umoja wa Ulaya (EU) katika nchi za
Africa, Caribbean na Pacific (ACP), ambayo inalenga kupunguza majanga katika
nchi hizo.(PICHA ZOTE
NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
0 comments:
Post a Comment