METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, January 11, 2019

MAKAMU WA RAIS ATEMBELEA MRADI WA NYUMBA ZA MAKAAZI YA POLISI MFIKIWA PEMBA


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akikagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba za makaazi ya askari Polisi  Mfikiwa Pemba. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na askari polisi wa kike waliokuwa wakijiandaa kwa ajili ya gwaride la maadhimisho ya sherehe za miaka 55 ya Mapinduzi Takatifu ya Zanzibar mara baada ya kuwaliza kukagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba za makaazi ya askari Polisi  Mfikiwa Pemba. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipata maelezo kutoka kwa Kamishina wa Polisi Zanzibar (CP) Mohamed Hassan Haji wakati wa kukagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba za makaazi ya askari Polisi  Mfikiwa Pemba. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo ametembelea na kujionea maendeleo ya ujenzi wa nyumba za makaazi ya Askari Polisi Mfikiwa Chake Chake Pemba.

Makamu wa Rais ambaye yupo Pemba kwa ajili ya kuhudhuria sherehe za miaka 55 ya Mapinduzi ambapo jana tarehe 10 Januari 2019 aliweka jiwe la msingi la Ujenzi wa Makaazi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar eneo la Pagali Chake Chake Pemba.

Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo Makamu wa Rais aliwataka Viongozi wa Vikosi kuongeza nguvu na kuhakikisha usimamizi wa shughuli za ujenzi wa makaazi ya askari unakamilika kama ulivyopangwa.

“Mwaka jana tarehe 20 Machi 2018 niliweka jiwe la msingi wa ujenzi wa nyumba za makaazi wa askari wetu hivyo basi lazima lengo litimie kama tulivyozungumza siku ya uwekaji jiwe la msingi” alisema Makamu wa Rais.

Kwa upande mwingine Kamishna wa Polisi Zanzibar (CP) Mohamed Hassani Haji amesema kuwa mipango ya kumalizia ujenzi wa makaazi bora ya askari polisi bado inaendelea na kuahidi kuikamilisha kwani ni dhamira ya jeshi la polisi kuhakikisha askari wake wanaishi sehemu salama.

Pamoja na mambo mengine Makamu wa Rais aliwasalimia Askari wa Kike waliokuwa kwenye maandalizi ya gwaride maalum la siku ya maadhimisho ya kilele cha miaka 55 ya Mapinduzi Takatifu ya Zanzibar yatakayofanyika kesho kwenye uwanja wa Gombani, Chake Chake Pemba.

“Mtapanda vyeo kwa jitihada ya kazi si vinginevyo hivyo Askari unatakiwa ufanye kazi kwa bidii sana”aliwahusia Makamu wa Rais.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com