Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akizungumza na washirika mbalimbali wa Maendeleo pamoja na watendaji wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake katika Ofisi za Wizara ya Nishati jijini Dodoma
Waziri wa Nishati, Dkt Medard
Kalemani amekutana na washirika wa maendeleo wanaofadhili miradi ya nishati ili
kujadiliana nao kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo miradi wanayoifadhili na
miradi mipya inayohitaji fedha za uwekezaji.
Kikao hicho kimefanyika jijini Dodoma
katika Ofisi za Wizara ya Nishati na kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati,
Subira Mgalu, Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt Hamisi Mwinyimvua, Kaimu Kamishna wa
Umeme na Nishati Jadidifu, Kaimu Kamishna wa Petroli na Gesi na watendaji
kutoka Taasisi zilizo chini ya Wizara.
Baadhi ya washirika wa maendeleo
waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Umoja wa Ulaya (EU), Shirika la
Maendeleo la Ufaransa (AFD), Benki ya Dunia (WB), Shirika la Maendeleo la Japan
(JICA), Ubalozi wa Ujerumani na Ubalozi wa Urusi nchini Tanzania.
“Serikali haiwezi kufanya kazi
peke yake hasa katika kutekeleza mipango ya muda mrefu ya kuzalisha megawati
10,000 ifikapo mwaka 2025 na mipango ya muda mfupi ya kuzalisha megawati
5000 ifikapo mwaka 2020,” amesema Dkt. Kalemani.
Amesema kuwa, washirika hao
wanahitajika katika kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya usambazaji na
usafirishaji umeme ambapo ameeleza kuwa sehemu kubwa ya nchi ina miundombinu ya
umeme ya kV 33 na 132kV lakini kwa sasa msisitizo unawekwa katika kupata fedha
ya kujenga miundombinu ya msongo wa kV 220 hadi kV 400 ili kupeleka umeme
mwingi na wa uhakika kwa wananchi.
Ameongeza kuwa, kwa sasa uwezo
wa mitambo ya kufua umeme ni megawati 1500 lakini bado inahitajika mitambo
itakayozalisha megawati 3500 ili kuweza kufikia megawati 5000 ifikapo mwaka
2020, hivyo zinahitajika juhudi za pande zote mbili ili kuweza kufikia
lengo husika.
Dkt Kalemani pia, amewaeleza
washirika hao kuwa, Tanzania bado ina fursa za uwekezaji katika uzalishaji wa
umeme kwa kutumia maji ambapo kuna vyanzo vya maji vinavyoweza kuzalisha
megawati 4700 lakini kwa sasa zinazalishwa megawati chini ya 600 kwa kutumia
chanzo hicho.
Kuhusu umeme wa makaa ya mawe amesema
kuwa, Tanzania ina mashapo ya makaa ya mawe ya kiasi cha tani 1.2 bilioni
lakini hazijaanza kuzalisha umeme hivyo eneo hilo pia linahitaji ushirikiano
ili makaa hayo yatumike katika kuzalisha umeme.
Aidha, amewaeleza washirika wa
maendeleo kuwa, Tanzania ina upepo wenye kasi ya 8-9 kilometa kwa sekunde ambao
unaweza kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 5000 lakini kwa sasa umeme wa
upepo unaozalishwa nchini ni chini ya megawati 1.
Vilevile amewaeleza kuhusu fursa za
uwekezaji katika uzalishaji umeme kwa kutumia Jotoardhi na kusema kuwa nchi
inaweza kuzalisha umeme wa megawati 5000 kutokana na chanzo hicho ambacho
hakijaanza kutumika tofauti na nchi ya Kenya ambayo inazalisha takriban
megawati 200.
Kwa ujumla, Waziri wa Nishati
amewaeleza Washirika hao wa maendeleo kuhusu maeneo yote yanayohitaji
ushirikiano ambayo ni miradi ya uzalishaji, usafirishaji, usambazaji umeme na
kuongeza ujuzi kwa wataalam nchini.
Akizungumza kwa niaba ya washirika
hao wa maendeleo, Mwakilishi kutoka Umoja wa Ulaya, Jenny Correia Nunes,
amemshukuru Waziri wa Nishati kwa kuitisha kikao hicho ambacho kimejenga uelewa
wa pamoja kati ya pande hizo mbili na kushauri kuwa utaratibu wa vikao vya
pamoja uwe ni endelevu.
0 comments:
Post a Comment