Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa uzinduzi wa mashindano ya michezo ya SHIMMUTA jijini Dodoma. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwasalimia wachezaji wa timu ya mpira wa pete (Netball) ya Geita Gold Mine wakati wa uzinduzi wa mashindano ya SHIMMUTA kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka Wakuu wa Mashirika na Taasisi kutenga fedha kwa ajili ya michezo.
Makamu wa Rais ameyasema hayo leo kwenye uzinduzi wa Mashindano ya SHIMMUTA uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
“Kwa Wakuu wa Taasisi, kwa kuwa kalenda za michezo hii inajulikana ni vyema mkahakikisha bajeti zinapangwa mapema” alisema Makamu wa Rais.
Akiwa Mlezi wa SHIMMUTA Makamu wa Rais amesema angependelea kuiona SHIMMUTA ya 2019 ikiwa sawa na ya miaka ya 60 ambapo timu zaidi ya 60 zilishiriki.
Makamu wa Rais ametoa rai kwa Taasisi, Mashirika na Makampuni kuwajibika kikamilifu kuhakikisha mashindano haya yanakuwa endelevu ikiwa pamoja na kupata mbinu mbadala za kupata washirika zaidi wa kugharamia michezo hii.
Kaulimbiu ya mwaka huu inasema ‘ufanisi katika utendaji kazi hutegemea afya bora ya wafanyakazi, tuhumize michezo sehemu za kazi’
Timu 21 zinashiriki SHIMMUTA ya mwaka huu na michezo yote itachezwa kwenye viwanja vya michezo vya chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Kwa upande mwingine Naibu Waziri wa Michezo, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Julliana Shonza amesema Wizara yake inatambua uwepo wa mashindano hayo na kutoa pongezi kwa kamati iliyoanda michezo hiyo mwaka huu.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa SHIMMUTA Dkt. Hamis Mkanachi amesema michezo hiyo ilianzishwa mwaka 1967 ikiwa na lengo la kuhimiza michezo sehemu za kazi na kuwaweka Watendaji, Taasisi na Mashirika na kudumisha mahusiano na kutangaza shughuli za Taasisi zao.
Katika ufunguzi wa leo timu ya mpira wa miguu TPDC na Geita Goldmine walifungua dimba wakati kwa upande wa mpira wa pete (netball) timu ya Chuo Kikuu Dodoma na Geita Goldmine zilifungua dimba.
0 comments:
Post a Comment