Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh.Joachim Wangabo akipita katika sehemu ya kukaushia samaki ambayo haijawahi kutumika tangu soko hilo lizinduliwe mwaka 2012
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo
amwemuagiza katibu tawala wa Mkoa wa Rukwa kuhakikisha anaunda timu kwaajili ya
kufanya uchunguzi juu ya matumizi ya fedha iliyotumika kwenye ujenzi wa soko
hilo uliokamilika mwezi Novemba mwaka 2011 na kuzinduliwa mwaka 2012 na
aliyekuwa makamu wa rais Dkt. Gharib Bilal.
Mh. Wangabo amesema kuwa hali ya soko ilivyo ni
tofauti na thamani inayotajwa ambayo ilitumika kwaajili ya ujenzi wa soko hilo
na tangu kuzinduliwa kwake halijaanza kutumika kama ilivyotarajiwa ambapo
walengwa ni wakazi wapatao 35,205 waishio mwambao wa ziwa Tanganyika.
“Bilioni moja nukta imekwisha lala hapa, RAS unda
timu ije ifanye tathmini ya fedha iliyotumika hapa, hiyo ni fedha ya serikali
na tunakatisha tamaa wenzetu wanaotusaidia Jumuiya ya Ulaya wametoa zaidi ya
milioni 700 na wengine MIVRAF wametoa milioni karibui 300, hawa wawili tu ni
bilioni moja jumlisha milioni 100 za halmashauri bado hapa mahali
hapajakamilika na mapungufu yapo,” Alifafanua.
Halikadhalika alieleza kuwa mfumo wa meko yaliyopo
katika soko hilo sio rafiki wa mazingira hivyo aliwataka watakaotumia soko hilo
wafikirie namna ya kutengeneza mkaa mbadala kwa kutumia makaa ya mawe
yanayopatikana kwa wingi katika kijiji cha Nkomolotu, Wilayani nkasi mkoani
humo.
Wakati akisoma taarifa ya soko hilo afisa uvuvi wa
halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Nicholas Mrango alisema kuwa wananchi wa
mwambao huo wana fursa ya kuvua samaki kwa wastani wa tani 167,000 kwa mwaka na
kuongeza pato la halmashauri na serikali kuu na kutaja malengo ya mradi huo na
changamoto zake.
“Malengo ya mradi ni kuboresha hali ya uchumi wa
wananchi, kupata wanunuzi wa samaki wa uhakika ndani nan je ya nchi lakini ili
soko lianze kutumika linahitaji miundombinu ya umeme, chumba cha kukaushia
samaki, mtambo wa kugandisha barafu, meza za kuuzia samaki na chanja za
kuanikia ili kukidhi kiwango cha kimataifa,”Alibainisha.
Soko kuu la samaki hao ni pamoja na ndani ya wilaya
ya Kalambo, mkoa wa Rukwa kwa ujumla, Mikoa ya Mbeya, Iringa,Njombe na Ruvuma
na pia nchi za jirani za Zambia, Demokrasia ya Watu wa Congo, Rwanda na
Burundi.
0 comments:
Post a Comment