Asteria Muhozya
na Rhoda James, GEITA
Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Madini imeanza kufanya
mazungumzo na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ili iweze kujenga
Kiwanda cha Kuchenjua madini ya Colbat nchini.
Hayo yalibainishwa Oktoba 19, mkoani Geita na Waziri wa Madini wa Tanzania Angellah
Kairuki wakati wa kuhitimisha ziara ya siku Nne ya Waziri wa Madini wa Kongo (DRC), Martin
Kabwelulu aliyoifanya nchini kwa mwaliko wa Waziri Kairuki.
Kairuki alisema kuwa, nchi ya Kongo ndiyo mzalishaji mkubwa wa
madini ya Colbat duniani ambapo asilimia 70 ya madini hayo duniani yanazalishwa
nchini humo.
Aliongeza kuwa, kwa sasa nchi hiyo inayo changamoto ya kusafirisha
madini hayo yakiwa ghafi ikiwemo ukosefu wa umeme wa kutosheleza kwa ajili ya
ujenzi wa viwanda hivyo.
“Tumekubaliana kuendelea na mazungumzo na Kongo ili shughuli za uchenjuaji na
uyeyushaji wa madini hayo ufanyike nchini
kwa kuwa tumeshaanza kuwekeza kwenye Vinu/viwanda vya Kuchenjua na kuyeyusha madini mbalimbali.
Hivyo, tunataka wayasafirishe makinikia ya Colbat hapa na tuyachenjue hapa,” alisisitiza
Kairuki.
Akizungumzia matumizi ya madini hayo, Kairuki alisema kuwa, madini
ya Colbat yanatumika kutengeneza betri na vihifadhi nishati (capacitor) ambazo zinahitajika sana
hususan, kwenye magari yanayotumia umeme.
Mbali na makubaliano ya ujenzi wa kiwanda hicho, pia Waziri
Kairuki alisema kuwa nchi hizo zimekubaliana masuala kadhaa ikiwemo kuendelea kubadilishana
uzoefu wa usimamizi wa sekta ya Madini ili kuweza kunufaisha wananchi hasa wale
wanaozunguka maeneo ya migodi.
“Nchi ya Kongo DRC imefurahishwa na hatua za Mkoa wa Geita kwenye
usimamizi wa mapato yatokanayo na madini pia mchango wa migodi kwa maendeleo ya
wananchi wanaozunguka mgodi,”alisema Kairuki.
Vilevile, alisema kuwa nchi hizo zimekubaliana kuboresha
mahusianao ya kimkakati ambapo Kongo imeahidi kuiunga Mkono Tanzania katika
masuala ya Mashtaka dhidi ya makampuni za uwekezaji.
Pia, alisema Kongo imeahidi kukitumia Chuo Cha Madini Dodoma (MRI)
kupata mafunzo mbalimbali yanayohusu sekta ya madini yanayotolewa kituoni hapo;
“Kongo imepanga kuja kujifunza mfumo mpya wa utoaji wa leseni za
madini (cadaster) ambao umebuniwa na
kusanifiwa na watanzania,” alisema Kairuki.
Kairuki aliongeza kuwa, nchi hizo zimekubaliana kuendelea
kuboresha mifumo ya udhibiti utoroshaji wa madini yanayotoka Kongo na Tanzania
kwa manufaa ya nchi zote mbili.
Aidha, Waziri Kairuki alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji
wa Kongo wenye nia ya kuwekeza nchini kwenye migodi, viwanda vya uchenjuaji,
uongezaji thamani madini (ukataji, unga’rishaji).
“Lakini pia tumewakaribisha kutumia bandari yetu kupitisha madini
yao pamoja na kukubaliana kuwa na Mining
Forum kati ya nchi hizi mbili tu ukiachia Forum nyingine ambazo tumelenga kuziandaa na kushirikisha wadau
kutoka nchi mbalimbali,” alisema Kairuki.
Aidha, alisema nchi hiyo
imeahidi kurudi nchini katika kipindi
kifupi kijacho kwa ajili ya kujifunza zaidi kuhusu namna Taasisi ya Jiolojia na
Utafiti wa Madini Tanzania (GST)
inavyofanya kazi zake za utafiti na maabara.
Kwa upande wake, Waziri wa DRC, Martin Kabwelulu alisema atawatuma
Wataalam wake kurudi nchini kwa ajili ya kujifunza mfumo mpya wa utoaji wa
leseni za madini (cadaster) wa
Tanzania na kuongeza ni mfumo mzuri ambao utaliwezesha taifa hilo kusimamia
vema rasilimali madini na kuhakikisha kwamba zinawanuifaisha wananchi wake.
Pia, alisema kuwa nchi hiyo inao
ukosefu wa umeme wa kutosha jambo ambalo linafanya nchi hiyo kusafirisha madini
hayo nje yakiwa ghafi ikiwemo madini ya Colbat na dhahabu na kuongeza kuwa,
Rais wa nchi hiyo, Joseph Kabila katika
ujumbe wake amemweleza kuwa, anataka madini yote ya Kongo yasafirishwe kupitia
Tanzania.
“Tunataka tusafirishe madini yetu
kupitia bandari ya Tanzania. Lakini pia nimeona njia ya kupitishia madini yetu
kupitia reli ya Kati ya Kigoma –Dar es Salaam ni fupi sana,” alisema Kabwelulu.
Akizungumzia mabadiliko ya Sheria ya
Madini yaliyofanywa nchini humo hivi karibuni, alisema nchi hiyo iliamua
kubadili sheria yake kutokana na kutokunufaika kabisa na rasilimali hiyo
hususan kwa wananchi wanaozungukwa na
rasilimali hizo na kuongeza kuwa, sheria ya sasa inapigania zaidi maslahi
ya nchi na wananchi wake.
“Nafurahi nimepokelewa vizuri sana
Tanzania, nimejifunza mengi kweli hii ni nchi rafiki. Sisi tunao uzoefu wa
miaka mingi kwenye sekta hii lakini bado hatujanufaika kabisa,” alisema
Kabwelulu.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi
Robert Luhumbi alisema kuwa, amemwomba Waziri wa Madini wa Kongo kujenga
kiwanda cha Colbat nchini kwa kuwa nchi hiyo iko jirani sana na mkoa huo na
kwamba mkoa huo umejipanga kwa mazingira ya uwekezaji mkubwa.
Akiwa nchini, Waziri Kabwelulu alipata
fursa ya kukutana na Menejimenti ya Wizara ya Madini na Taasisi zake ambapo
pande zote zilibadilishana uzoefu wa namna zinavyosimamia sekta ya madini,
ikiwemo masuala ya uchimbaji mdogo wa madini.
Aidha, Waziri Kabwelulu na mwenyeji
wake Waziri Kairuki walitembelea Mgodi wa Mfano wa Lwamgasa ambao umejengwa
mahsusi kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP)
unaosimamiwa na wizara. Lengo la mgodi huo ni kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo
kuhusu uchimbaji sahihi na uchenjuaji
bora wa madini dhahabu.
Pia, walitembelea migodi ya Wachimbaji wa Kati
inayomilikiwa na watanzania ya Buswola Mining Ltd na Nsangano Gold Mine mkoani Geita
kujifunza walikotokea katika uchimbaji mdogo hadi kuwa wa Kati na pia
walitembelea mgodi wa Almasi wa Mwadui (WDL) mkoani Shinyanga.
Ziara ya Waziri Kabwelulu nchini
ililenga katika kubadilishana uzoefu na utaalamu katika masuala ya uendelezaji
na usimamizi wa Sekta ya Madini ikiwemo kuimarisha zaidi ushirikiano uliopo baina
ya hizo mbili, kuangalia fursa za ushirikiano wa kibiashara na kiuwekezaji
kupitia rasilimali madini madini, kubadilishana uzoefu kuhusu Mabadiliko ya
Sheria za Madini yaliyofanywa na nchi hizi mbili hivi
karibuni pamoja na kudumisha undugu na urafiki baina ya nchi hizo mbili.
koani
Geita.
0 comments:
Post a Comment