Mamlaka
ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imejipanga kupitia kaulimbiu yake kuifungua
Tanzania kwa ulimwengu kupitia sekta ya Utalii nchini, kwa kuimarisha usafiri
wa anga ili kuhakikisha watalii wote wanafikia vivutio vyote vya utalii kwa
haraka zaidi.
Hayo
yamebainishwa juzi na Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Richard Mayongela alipokuwa
akizumgumza na waandishi wa habari siku ya ushiriki wa Mamlaka katika Tamasha
la Urithi Wetu linaloanza leo Jumatatu (Oktoba Mosi, 2018) kwa Mkoa wa Dar es Salaam.
"Viwanja
vyetu vya ndege ndio milango mikuu wa watalii kupita, hivyo tupo hapa kuwaambia
wananchi, wadau pamoja na Jumuiya za Kimataifa kwamba sasa kuna fursa ya
kutanganza vivutio vya kitalii kupitia viwanja vyetu vya ndege kwa kuwa vinatumika
kwa usafiri wa anga lakini pia tunaweza kuvitumia kibiashara kwa kutangaza
vivutio vyetu" alisema Bw. Mayongela.
Bw
Mayongela pia amewapa wito Watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii kutangaza
vivutio vilivyopo kupitia Viwanja vya ndege lakini pia kuwaeleza wadau kwa njia
mbalimbali zilizopo Tanzania ili watalii wanapowasili waweze kupata picha
halisi ya maeneo ya kutembelea akiwa nchini.
Aidha
Bw. Mayongela ameongeza kwamba Mamlaka ina mtandao mkubwa na inasimamia viwanja
58 vilivyopo chini ya serikali, ambavyo vipo kila sehemu penye vivutio vya
utalii na wamejiimarisha kuhakikisha huduma bora ya usafiri wa anga.
"Sehemu
ya Kaskazini mwa nchi yetu ambapo ndio kuna vivutio vingi, vipo viwanja vya
ndege vya kutosha, tuna Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA),
Kiwanja cha Lake Manyara ambacho kimejengwa kwa mkakati wa kutumika kwa watalii
na kinafanya vizuri sana kwa kuingiza watalii wengi, vilevile tuna mpango wa
kujenga kiwanja kipya katika Mkoa wa Manyara,” alibainisha Bw. Mayongela.
Akizungumzia miundombinu ya Viwanja vya Ndege
kwa Kanda ya Kusini ameeleza kwamba serikali imejitoa kufanya maboresho ya
kiwanja cha Mtwara kwa lengo moja kuu la kuvutia watalii wengi zaidi ili waweze
kushuhudia vivutio vya utalii vilivyopo maeneo hayo.
“Serikali inaboresha kwa kufanya upanuzi na
ukarabati mkubwa wa Kiwanja Cha Ndege cha Mtwara, pamoja na sababu za kiuchumi
lakini pia lengo ni kuvutia watalii wengi zaidi ili waweze kushuhudia vivutio
vilivyopo, sio hivyo tu lakini pia Kilwa masoko tuna kiwanja, Lindi tuna
kiwanja, Nachingwea mpaka Masasi kote tuna viwanja” Alisema Bw. Mayongela.
Akizungumzia upande wa nyanda za juu Kusini
Bw. Mayongela amebainisha kwamba baada ya ukarabati mkubwa kukamilika kutakuwa
na kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Songwe, Njombe mpaka Iringa kutakuwa na
viwanja vizuri vya ndege ili kuhakikisha kwamba vivutio vilivyopo Tanzania vinafikika
kwa urahisi.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mkuu wa
Makumbusho ya Taifa, Prof Audax Mabula ameeleza kwamba Tamasha la Urithi Wetu lililobuniwa
na Wizara ya Maliasili na Utalii lina madhumuni makuu mawili ikiwemo ya kuwezesha
kuonyesha fursa zote zinazoizunguka tasnia hii.
“Madhumuni makuu ni kuendeleza, kutambua na
kuhifadhi urithi wetu wa utamaduni kwa ajili ya kizazi kilichopo na kinacho
kuja lakini pili ni kubadili urithi wetu wa utamaduni kuwa zao la utalii hayo
ndio malengo makuu mawili” alisema Prof Mabula.
TAA wametoa msaada wa fulana 100 kwa ajili ya
washiriki wa tamasha la Urithi Wetu, ambalo litafikia tamati Oktoba 6, 2018 kwa
kufungwa na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa.
Imeandaliwa na Idara ya Uhusiano Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA)
0 comments:
Post a Comment