Waziri wa Kilimo Dkt Charles Tizeba (Mb), akisisitiza mpango wa serikali kukabiliana na njaa wakati akihutubia wananchi waliojitokeza kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Chakula Duniani Kitaifa ambayo yamefanyika kwenye viwanja vya JK Nyerere katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma jana tarehe 16 Octoba 2018. (Picha Na Mathias Canal, WK)
Waziri wa Kilimo Dkt Charles Tizeba (Mb), akikagua banda la Bima ya mazao wakati wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya Chakula Duniani Kitaifa ambayo yamefanyika kwenye viwanja vya JK Nyerere katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma jana tarehe 16 Octoba 2018.
Na Mathias Canal-WK,
Tunduma-Mbeya
Katika kukabiliana na upungufu wa
chakula unaoweza kujitokeza pindi nchi itakapokuwa kwenye majanga, Serikali
imetoa jumla ya shilingi Billioni 15.0 za Kitanzania kwa ajili ya ununuzi wa
mahindi kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi Chakula (NFRA) katika mwaka wa fedha
2018/2019.
Tayari Wakala wa Taifa wa
Hifadhi Chakula (NFRA) umeanza msimu wa ununuzi tangu mwezi Agosti 2018 ambapo
nafaka wanayonunua ni kutoka kwa wakulima na vikundi vya wakulima kote
nchini.
Waziri wa Kilimo Dkt Charles
Tizeba (Mb), amebainisha hayo jana tarehe 16 Octoba 2018 wakati akihutubia
wananchi waliojitokeza kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Chakula
Duniani Kitaifa ambayo yamefanyika kwenye viwanja vya JK Nyerere katika
Halmashauri ya Mji wa Tunduma.
Vilevile, NFRA inaendelea
kuboresha uwezo wake wa kuhifadhi nafaka kwa kuimarisha kanda zake kupitia
mradi wa ujenzi wa vihenge na maghala ya kisasa ili Kuongeza uwezo wa kuhifadhi
nafaka.
Dkt Tizeba alisema kuwa Kupitia
mradi huo miundo mbinu ya kisasa ya hifadhi ya chakula zikiwemo maghala na
vihenge vya kisasa vinajengwa katika Halmashauri za Wilaya za Babati (Tani
40,000), Mpanda (Tani 25,000) , Sumbawanga (Tani 40,000), Mbozi (Tani 20,000),
Songea (Tani 50,000), Shinyanga (Tani 35,000), Dodoma (Tani 20,000) na
Makambako (Tani 30,000).
Alisema, Hifadhi hizo zitatumia
teknolojia ya kisasa ya kuhifadhi mazao na hivyo kupunguza upotevu wa mazao
ghalani kwa kiasi kikubwa.
Aliongeza kuwa, Kukamilika kwa
mradi huo kutawezesha NFRA kuongeza uwezo wake wa kuhifadhi nafaka kutoka Tani
251,000 hadi kufikia Tani 501,000 ifikapo mwaka 2019/2020.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment